Bunge la umma la China
Utaratibu wa Bunge la umma la China ni utaratibu wa kisiasa wa kimsingi wa China. Bunge la umma la China ni chombo chenye madaraka ya juu kabisa la taifa, ambalo linaundwa na wajumbe waliochaguliwa kutoka mikoa, mikoa inayojiendesha, miji inayotawaliwa moja kwa moja na serikali kuu, mikoa ya utawala maalum na jeshi. Chombo hicho kinaendesha madaraka ya taifa ya utungaji wa sheria na kuamua masuala makubwa ya maisha ya siasa ya taifa.
Madaraka makuu ya Bunge la umma la China ni: Kurekebisha katiba, kusimamia utekelezaji wa katiba, kutunga na kurekebisha sheria za makosa ya jinai, mambo ya raia, idara za taifa na sheria nyingine za kimsingi; kuthibitisha na kuidhinisha mipango ya maendeleo ya uchumi na jamii na ripoti kuhusu hali ya utekelezaji wa mipango, pamoja na bajeti ya taifa na ripoti kuhusu hali ya utekelezaji wa bajeti ya taifa; kuidhinisha kuanzishwa na kuwekwa kwa mikoa, mikoa inayojiendesha na miji inayotawaliwa moja kwa moja na serikali kuu, na kuamua uanzishaji wa mkoa wa utawala maalum na mfumo wake; kuamua masuala kuhusu vita na amani; kuchagua na kuamua viongozi wa chombo chenye madaraka ya juu kabisa cha taifa, yaani kuchagua wajumbe wa Halmashauri ya kudumu ya Bunge la umma la China na wajumbe wa bunge hilo, kuwachagua rais, makamu wa rais wa nchi, kuamua waziri mkuu wa serikali na viongozi wengine, kuchagua mwenyekiti wa kamati kuu ya kijeshi na viongozi wengine wa kamati hiyo, kumchagua mkuu wa mahakama kuu ya umma na kumchagua mkuu wa Idara kuu ya uendeshaji wa mashitaka. Bunge la umma la China lina madaraka ya kuwaondoa madarakani viongozi wote hao waliotajwa.
Muda wa Bunge la umma la China la kila awamu ni miaka mitano, bunge hilo linafanya mkutano wa wajumbe wote kila mwaka. Wakati mkutano huo unapofungwa, Halamshauri yake ya kudumu inaendesha madaraja ya juu kabisa ya taifa. Halamshauri ya kudumu ya Bunge la umma la China linaundwa na spika, manaibu maspika, katibu mkuu na wajumbe.
Utungaji sheria wa China ni pamoja na utungaji sheria wa Bunge la umma la China na halmashauri yake ya kudumu, utungaji sheria wa Baraza la serikali na wizara zake, utungaji sheria wa kawaida wa mikoa mbalimbali, utungaji sheria wa mikoa inayojiendesha ya makabila madogomadogo, utungaji sheria wa sehemu maalum za kiuchumi na mikoa ya utawala maalum.
Baraza la mashaurinao ya kisiasa la umma la China
Baraza la mashauriano ya kisiasa la umma la China ni jumuia ya wazalendo wanaopenda nchi ambalo ni baraza muhimu la kufanya ushirikiano wa vyama vingi na mashauriano ya kisiasa chini ya uongozi wa Chama cha kikomunisti cha China, ambapo wajumbe wa jumuia hiyo wanaweza kuenzi demokrasia ya ujamaa katika maisha ya siasa ya China. Mshikamano na demokrasia ni mada kubwa mbili za baraza hilo.
Halmashauri ya nchi zima ya Baraza la mashauriano ya kisiasa la umma la China inaundwa na wajumbe wa Chama cha kikomunisti cha China, vyama mbalimbali vya kidemokrasia, watu wasio na vyama, makundi ya umma, wajumbe wa makabila madogomadogo na wajumbe wa sekta mbalimbali, ndugu wa mikoa ya utawala maalum ya Hong Kong na Makau, ndugu wa Taiwan na wachina walioishi nchi za nje pamoja na watu walioalikwa maalum. Muda wa kila awamu ya halmashauri hiyo ni miaka mitano.
Jukumu kubwa la halmashauri hiyo na ya ngazi mbalimbali ni kufanya mashauriano ya kisiasa, usimamizi wa demokrasia, kutoa maoni na mapendekezo kuhusu sera za nchi na maazimio ya serikali.
Mashariano ya kisiasa
Kabla ya serikali kuu na serikali za mikoa kutoa sera na maazimio kuhusu masuala makubwa ya siasa, uchumi, utamaduni na jamii, Halmashauri ya nchi nzima ya Baraza la mashauriano ya kisiasa na halmashauri ya mikoa zinaweza kuitisha mikutano inayohudhuriwa na wakuu wa vyama mbalimbali na makundi mbalimbali pamoja na wajumbe wa makabila na sekta malimbali ili kufanya mashauriano na kutoa maoni na mapendekezo yao.
Usimamizi wa kidemokrasia:
Kutoa maoni na mapendekezo au ukosoaji kwa kufanya usimamizi kuhusu utekelezaji wa katiba ya nchi, sheria na kanuni, sera na hatua kubwa, kazi za ofisi za serikali na watumishi wake.
Kushiriki mambo ya siasa
Kufanya uchunguzi na utafiti na kufanya majadiliano kwa kutoa maoni ya wananchi kuhusu masuala muhimu ya siasa, uchumi, utamaduni na maisha ya jamii pamoja na masuala yanayofuatiliwa na umati wa watu. Kutoa ripoti na miswada ya mapendekezo au kupitia njia nyingi kwa kutoa maoni na mapendekezo kwa chama cha kikomunisti cha China na idara za serikali ya China.
Mwezi Septemba mwaka 1949, Mkutano wa kwanza wa wajumbe wote wa Baraza la mashauriano ya kiasiasa la umma la China uliendesha madaraka badala ya Bunge la umma la China na kuwakilisha nia ya wananchi wa taifa zima, ukitangaza kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China, hii ni kazi muhimu ya historia iliyofanywa na baraza hilo. Baada ya kufanyika kwa mkutano wa kwanza wa Bunge la umma la China mwaka 1954, Baraza la mashauriano ya kisiasa haliendeshi tena madaraka ya Bunge la umma la China, lakini limeendelea kuwepo likiwa jumuiya ya wazalendo wanaoipenda nchi, ambalo limefanya kazi nyingi na kutoa mchango mkubwa katika maisha ya kisiasa ya taifa na maisha ya jamii pamoja na shughuli za urafiki kwa nchi za nje. Ilipofika mwezi Machi mwaka 2004, baraza hilo limeanzisha mawasiliano na idara 170 za nchi 101 na jumuia 8 za kimataifa au kikanda, na kuanzisha mawasiliano ya kirafiki.
Baraza la serikali la China na wizara zake
Baraza la serikali
Baraza la serikali la China yaani serikali kuu ya umma, ni chombo kikuu cha mambo ya utawala cha nchi. Baraza hilo linatekeleza sheria na maazimio yaliyopitishwa na Bunge la umma la China na halmashauri yake ya kudumu, na kuwajibika pia kutoa ripoti ya kazi kwa Bunge la umma la China na halmashauriano yake ya kudumu,. Baraza la serikali lina madaraka ya kuweka hatua za utawala, kubuni sheria na kanuni za utawala, na kutoa maazimio na maagizo ndani ya madaraka yake. Baraza la serikali linaundwa na waziri mkuu, manaibu mawaziri, wajumbe wa kitaifa, mawaziri wa wizara mbalimbali, wakurugenzi wa kamati mbalimbali, mkaguzi mkuu wa uhasibu, na katibu mkuu. Waziri mkuu wa hivi sasa ni Bwana Wen Jiabao.
Hivi sasa Baraza la serikali la China linaundwa na wizara na kamati 28 kama vile Wizara ya mambo ya nje, Wizara ya ulinzi wa taifa, Kamati ya maendeleo na mageuzi ya taifa, Wizara ya elimu, Wizara ya sayansi na teknolojia, Kamati ya viwanda vya sayansi na teknolojia za ulinzi wa taifa, Kamati ya mambo ya makabila madogomadogo, Wizara ya usalama wa umma, Wizara ya usalama wa nchi, Wizara ya mambo ya kiraia, Wizara ya sheria, Wizara ya fedha, Wizara ya ajira, Wizara ya kazi na huduma za jamii, Wizara ya reli, Wizara ya mawasiliano, Wizara ya maliasili ya ardhi ya taifa, Wizara ya ujenzi, Wizara ya shughuli za upashanaji habari, Wizara ya maji, Wizara ya utamaduni, Wizara ya afya, Wizara ya Kilimo, Wizara ya biashara, Kamati ya idadi ya watu na uzazi wa mpango, Benki ya umma ya China na Idara kuu ya ukaguzi wa uhasibu.
Wizara ya mambo ya nje
Wizara ya mambo ya nje ni wizara ya Baraza la serikali inayowajibika na utekelezaji wa sera za China kwa nchi za nje na kushughulikia kazi ya kiplomasia ya kila siku. Jukumu kuu la wizara hiyo ni kuwakilisha taifa na serikali kusimamia mambo ya kidiplomasia kama vile kutangaza sera na maamuzi ya taifa kwa nchi za nje, kutangaza nyaraka na taarifa kuhusu mambo ya kidiplomasia; kushughulikia mambo ya kidiplomasia na kufanya mawasiliano ya kidiplomasia, kusaini mikataba, makubaliano na nyaraka nyingine za kidiplomasia; kuhudhuria mikutano ya kimataifa ya Umoja wa Mataifa na kati ya serikali na serikali na kushiriki kwenye shughuli za jumuiya za kimataifa; kushughulikia kazi ya kuanzisha ubalozi na ofisi husika za wawakilishi katika nchi za nje, kuwasimamia watumishi wa serikali wanaofanya kazi katika idara hizo, kuelekeza, kushirikisha na kuratibu shughuli za kidiplomasia kati ya idara za mambo ya nje katika wizara mbalimbali za Baraza la serikali na mikoa, mikoa inayojiendesha na miji inayotawaliwa moja kwa moja na serikali kuu, na kushughulikia kazi ya kuwaandaa na kuwasimamia makada wa kidiplomasia.
Kamati ya maendeleo na mageuzi ya nchi
Jukumu la kamati hiyo ni kubuni na kutekeleza mikakati ya maendeleo ya uchumi na jamii, mipango ya muda mrefu na wastani na mipango ya mwaka; kufanya utafiti na uchambuzi kuhusu hali ya uchumi wa nchini na ng'ambo na maendeleo ya hali hiyo, kufanya makadirio na kutoa tahadhari kuhusu uchumi wa taifa; kufanya utafiti kuhusu masuala muhimu yanayohusika na usalama wa uchumi wa taifa, kutoa mapendekezo kuhusu sera za marekebisho na udhibiti wa uchumi, kufanya usawazishaji wa maendeleo ya uchumi na jamii; kufanya mipango kuhusu miradi mikubwa na nguvu kazi nchini; kufanya mipango kuhusu fedha za ujenzi za taifa, kuelekeza na kusimamia matumizi ya fedha za mikopo kutoka nchi za nje kwa ujenzi wa China, na kuelekeza na kusimamia mwelekeo wa matuizi ya mikopo ya kisera; kuelekeza mwelekeo wa fedha za raia katika uwekezaji wa mali zisizohamishika; kufanya utafiti na kutoa malengo na sera za kimkakati kuhusu matumizi ya mitaji na uwekezaji kutoka nje; kupanga miradi ya ujenzi inayogharimiwa na serikali na miradi mikubwa ya ujenzi, miradi mikubwa ya uwekezaji wa nje, miradi ya uendelezaji wa maliasili na miradi ya uwekezaji mkubwa katika nchi za nje; kubuni na kutunga sheria na kanuni husika za utawala kuhusu maendeleo ya uchumi na jamii ya taifa pamoja na mageuzi ya mfumo wa uchumi, kuzifungulia mlango nchi za nje, na kushiriki kazi za kutunga sheria na kanuni za utawala na utekelezaji.
Wizara ya biashara
Wizara hiyo ilianzishwa rasmi mwezi Machi mwaka 2003.
Jukumu lake kuu ni kubuni mikakati, mwongozo na sera kuhusu maendeleo ya biashara nchini na ng'ambo na ushirikiano wa kimataifa wa sekta ya uchumi, kutunga sheria na kanuni kuhusu biashara ya nchini na ng'ambo, ushirikiano wa kiuchumi wa kimataifa na uwekezaji wa wafanyabiashara kutoka nje; kubuni mipango ya maendeleo ya biashara ya nchini, kufanya utafiti na kutoa maoni kuhusu mageuzi ya utaratibu wa mzunguko wa bidhaa, kuandaa na kuendeleza soko mijini na vijijini; kufanya utafiti kwa kubuni sera kuhusu utaratibu kamili wa uendeshaji wa soko, utaratibu wa mzunguko wa bidhaa na kuvunja ukiritimba wa soko na vikwazo vya kisehemu, kujenga mfumo wa soko wenye utaratibu kamili, wa kufunguliwa mlango na wa ushindani; kufuatilia na kuchambua hali ya uendeshaji wa soko na hali ya utoaji wa bidhaa sokoni, kutekeleza hatua za marekebisho na udhibiti kuhusu bidhaa muhimu za matumizi sokoni na usimamizi wa mzunguko wa raslimali muhimu za uzalishaji; kufanya utafiti na kubuni njia za usimamizi wa bidhaa ziagizwazo kutoka nje na ziuzwazo kwa nje pamoja na orodha ya bidhaa hizo, kutekeleza mipango ya mgao wa kuagiza bidhaa na kuuza bidhaa, kuthibitisha kiasi cha mgao na kutoa kadi za kibali; kutunga na kutekeleza sera kuhusu zabuni ya mgao wa bidhaa ziagizwazo kutoka nje na ziuzwazo kwa nje; kuratibu kazi ya kupinga mauzo ya bidhaa nyingi za bei chini, kupinga utoaji ruzuku, kutoa hatua za uhakikishaji na kazi nyingine zinazohusika na biashara ya haki, kuanzisha utaratibu wa utoaji tahadhari kuhusu biashara ya haki, kufanya uchunguzi kuhusu hasara za mashirika; kuelekeza na kuratibu kazi ya kujibu mashitaka kuhusu bidhaa za China zilizouzwa nje na kazi nyingine zinazohusika.
Kamati ya kijeshi ya kamati kuu ya chama
Kamati ya kijeshi ya kamati kuu ya Chama cha kikomunsti cha China ni idara kuu ya uongozi wa kijeshi chini ya uongozi wa Chama cha kikomunisti cha China, kamati hiyo inaundwa na mwenyekiti, naibu mwenyekiti na wajumbe. Kamati hiyo inaamuliwa na kamati kuu ya Chama cha kikomunisti cha China, ambayo inatekeleza utaratibu wa mwenyekiti kubeba wajibu. Jukumu lake kuu ni kuongoza moja kwa moja nguvu za majeshi ya nchi nzima.
Kamati kuu ya kijeshi ya Jamhuri ya Watu wa China ni idara ya uongozi wa kijeshi wa taifa, ambayo inaongoza nguvu za majeshi ya nchi nzima. Kamati hiyo inaundwa na mwenyekiti, manaibu wenyekiti kadhaa, na wajumbe kadhaa. Kamati hiyo inatekeleza utaratibu wa mwenyekiti kubeba wajibu. Mwenyekiti wa kamati hiyo huchaguliwa kwenye mkutano wa Bunge la umma la China, ambaye anawajibika kwa Bunge la umma la China na halmashauri yake ya kudumu. Muda wa kamati kuu ya kijeshi ya kila awamu ni miaka mitano, lakini hakuna kikomo kuhusu kiasi cha awamu.
Nguvu za majeshi ya China zinaundwa na Jeshi la ukombozi wa umma la China, Kikosi cha askari polisi cha umma cha China na wanamgambo. Jeshi la ukombozi wa umma ni jeshi la kudumu la taifa; kikosi cha askari polisi kinabeba jukumu la taifa la kulinda usalama na utaratibu wa jamii; wanamgambo ni wa kundi la umati wa watu wasiojitenga na shughuli za uzalishaji mali.
Mwenyekiti wa sasa wa Kamati ya kijeshi ya Kamati kuu ya Chama cha kikomunisti cha China na Kamati kuu ya kijeshi ya Jamhuri ya watu wa China ni Bwana Xi Jinping.
Mahakama kuu ya umma
Mahakama kuu ya umma ni idara ya taifa ya kushughulikia kesi. Serikali inaweka mahakama kuu ya umma, mikoa, mikoa inayojiendesha na miji inayotawaliwa moja kwa moja na serikali kuu inaweka mahakama kuu ya ngazi ya juu, mahakama ya umma ya ngazi ya kati na mahakama ya umma ya shina. Mahakama kuu ya umma ni chombo cha taifa cha hukumu cha ngazi ya juu kabisa, ambayo inaendesha madaraka ya uhukumu bila kuingiliwa, vilevile ni mamlaka ya juu kabisa ya usimamizi wa kazi ya mahakama ya umma ya ngazi mbalimbali. Mahakama kuu ya umma inawajibika kwa Bunge la umma la China na kutoa ripoti kuhusu kazi yake kwa bunge la umma, mkuu na naibu mkuu wa Mahakama kuu ya umma pamoja na wajumbe wa Kamati ya utoaji hukuma wa Mahakama kuu ya umma wote wanateuliwa na kuamuliwa na Bunge la umma la umma la China.
Jukumu la Mahakama kuu ya umma ni kushughulikia kazi ya utoaji hukumu kuhusu kesi zilizotolewa rufaa juu ya hukumu zilizotolewa na mahakama za ngazi ya Chini au Idara kuu ya uendeshaji wa mashitaka ya umma kwa kufuata utaratibu wa usimamizi wa hukumu; kuthibitisha hukumu za vifo; kama kugundua makosa katika hukumu zilizotolewa na mahakama ya umma ya ngazi mbalimbali, mahakama kuu ya umma ina madaraka ya kuhukumu au kuagiza mahakama ya ngazi ya chini kuhukumu tena; kuthibitisha uhalifu; na kutoa ufafanuzi kuhusu namna ya kutumia sheria halisi katika mchakato wa hukumu na kadhalika.
Idara ya uendeshaji wa mashitaka ya umma
Idara ya uendeshaji wa mashitaka ya umma ni mamlaka ya taifa ya usimamizi wa sheria. Idara hiyo inakamilisha jukumu lake kwa kuendesha madaraka yake ya uendeshaji wa mashitaka. Idara hiyo inaendesha madaraka yake katika kesi ya kuhaini nchi, kufarakanisha taifa na kesi nyingine kubwa; kufanya ukaguzi na uthibitishaji kuhusu kesi zilizoshughulikiwa na idara za usalama wa umma, kuamua kuwakamata watuhumiwa, kuwashitaki au kutowashitaki; kufanya usimamizi kuhusu shughuli za idara za usalama wa umma, mahakama ya umma, magereza na idara husika za utekelezaji wa sheria.
Idara kuu ya uendeshaji wa mashitaka inaendesha madaraka yake bila kuingiliwa kwa mujibu wa sheria, kazi yake hairuhusiwi kuingiliwa na idara za utawala, makundi ya jamii au watu binafsi; na inatekeleza sheria kwa raia wote kwa usawa. Serikali kuu inagawanyika katika Idara kuu ya uendeshaji wa mashitaka ya umma, idara za uendeshaji wa mashitaka za mitaa za ngazi mbalimbali na idara ya kijeshi ya uendeshaji wa mashitaka. Idara za uendeshaji wa mashitaka za umma za China zinagawanyika katika ngazi nne, yaani idara za shina, idara ya ngazi ya kati, idara ya ngazi ya juu na idara kuu ya uendeshaji mashitaka. Idara kuu ya uendeshaji wa mashitaka ni idara ya juu kabisa ya taifa yenye madaraka ya kuendesha mashitaka, ikiwakilisha taifa kuendesha madaraka ya uendeshaji wa mashitaka kwa kujiamulia, inawajibika moja kwa moja kwa Halmashauri ya kudumu ya Bunge la umma la China. Jukumu lake kuu ni kuongeza idara za uendeshaji mashitaka za ngazi mbalimbali za mitaa na idara maalum za uendeshaji wa mashitaka kutekeleza wajibu wake wa usimamizi wa kisheria, na kuhakikisha kuwa sheria za pamoja za taifa na utekelezaji wake sahihi.
|