mfumo wa Mtihani
Mhitani wa Kujiunga na Sekondari ya Juu
Nchini China wanafunzi wanapaswa kufanya mtihani wa kujiunga na sekondari ya juu baada ya kumaliza masomo ya sekondari ya chini. Kwa kuwa ni asilimia 60 tu ya wanafunzi wanaomaliza masomo ya sekondari ya chini wanaweza kuendelea na masomo ya sekondari ya juu, kiasi hicho hata ni chini ya kile cha wanafunzi wanaohitimu sekondari ya juu kujiunga na chuo kikuu, hivyo mtihani huo ni mmoja wa mitihani migumu kabisa nchini China.
Mtihani wa kujiunga na sekondari ya juu hutolewa na idara za elimu za sehemu mbalimbali. Masomo ya mtihani huwa ni Kichina, lugha ya kigeni, hisabati, fizikia na kemia. Mtihani hufanyika mwezi wa Juni kila mwaka.
Wanafunzi hawawezi kujiunga na katika sekondari ya juu bila kuwa na matokeo mazuri katika mtihani huo, halafu watapata fursa ya kujiunga na chuo kikuu, na kuwa na mustakabali mzuri wa kupata ajira bora. Kama wakishindwa katika mtihani huo, basi hawawezi kusoma katika sekondari ya juu, na wataanza kufanya kazi wakiwa na hali duni ya elimu. Kwa hivyo Wachina wengi wanaona kuwa mtihani huo unaamua mustakabali wa maisha ya watoto.
Mtihani wa Kujiunga na Chuo Kikuu
Mtihani huo hutolewa na idara za kitaifa au kimkoa kutokana na maelekezo ya muongozo wa mtihani unaotolewa na wizara ya elimu ya China. Mtihani huo unaofanyika kwa siku mbili au tatu, huanzia tarehe 7 Juni ya kila mwaka.
Hivi sasa, mambo yaliyomo katika mtihani wa kujiunga na chuo kikuu ni "3+X", 3 inamaanisha Kichina, hisabati na lugha ya kigeni, "X" inaweza kuwa mtihani wa masomo tofauti katika mitihani tofauti ya kitaifa na kimkoa. Katika baadhi ya sehemu "X" inawakilisha mtihani wa mseto wa sanaa na sayansi. Baadhi ya sehemu "X" inawakilisha masomo ya fizikia, kemia, biolojia, historia na kadhalika wanafunzi wanaochagua wenyewe.
Mtihani wa kujiunga na chuo kikuu unafuatiliwa sana na jamii ya China, lakini katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na vyuo vikuu kuongeza wanafunzi, shinikizo la watahiniwa na wazazi limepungua kidogo.
Mtihani wa Shahada ya Pili na ya Udaktari
Mtihani wa shahada ya pili nchini China hugawanya katika sehemu mbili ya mtihani wa maandishi na mtihani wa maongezi. Mtihani wa maandishi wa kozi za kawaida hutolewa na wizara ya elimu ya China, na kupanga maksi za chini kabisa za kuandikisha watahiniwa, kwa mfano watahiniwa wa kozi za fani hiyo wanatakiwa kufanya mtihani wa siasa na lugha ya kigeni, ambapo watahiniwa wa sayansi lazima wafanye mtihani wa siasa, lugha ya kigeni na hisabati. Mtihani wa somo maalum huamuliwa na vyuo vikuu au mashirika ya utafiti. Watahiniwa wakifikia maksi zinazokubalika, basi wataendelea kufanya mtihani wa maongezi. Vyuo vikuu na mashirika ya utafiti yatawaandikisha watahiniwa kutokana na matokeo yao katika mtihani wa maandishi na maongezi.
Mtihani wa shahada ya udaktari hutolewa na vyuo vikuu au mashirika ya utafiti yanayowaandikisha wanafunzi. Watahiniwa wa shahada ya pili wakitaka kuendelea na masomo ya shahada ya udaktari ya kozi wanayojifunza, basi wanatakiwa tu kufanya mtihani wa maandishi na maongezi ya lugha ya kigeni na masomo mengine mawili au tatu. Ama sivyo wanatakiwa kufanya mtihani wa maandishi na maongezi ya masomo matano au sita.
Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na shinikizo la kupata ajira, idadi ya watahiniwa wanaofanya mtihani wa shahada ya pili na ya udaktari imeongezeka kwa haraka. Isitoshe, kutokana na mageuzi ya mfumo wa elimu, mashirika yanayowaandikisha wanafunzi yana haki zaidi ya kujiamulia katika mtihani.
Mtihani wa Vyeti
Licha ya mtihani wa elimu ya diploma, China pia inafanya mitihani mingi kwa ajili ya kujipatia vyeti vya aina mbalimbali. Vyeti hivyo vinathibitisha kiwango cha ufundi wa watahiniwa katika kutafuta ajira.
Hivi sasa mitihani ya vyeti inayowaandikisha watu wengi ni kama mtihani wa kiwango cha lugha ya kigeni, mtihani wa kiwango cha kompyuta, mtihani wa daraja ya muziki na dansi, na mitihani ya kiwango cha viwango cha fani mbalimbali kama vile sheria na uhasibu. Zaidi ya hayo, kutokana na uchumi wa China kuelekea wa kimataifa, baadhi ya mitihani ya kimataifa ya sifa ya ajira pia imeingia nchini China.
Mitihani mingi ya vyeti nchini China huwa na madaraja mbalimbali ili kuonesha kiwango tofauti cha watahiniwa. Hivyo mtihani wa vyeti vingi unawataka watahiniwa kuendelea kujifunza ili kuinua kiwango chao.
|