Tiba ya Kichina
Historia ya Tiba ya Kichina
Tiba ya kabila la wahan ina historia ya miaka mingi zaidi kati ya tiba za jadi za kichina, hususan inajulikana kwa uzoefu na nadharia iliyojengwa katika miaka mingi iliyopita.
Tiba ya kichina ilianzia sehemu ya bonde la mto Manjano, na kujenga mfumo wa elimu yake tangu miaka mingi iliyopita. Katika maendeleo ya miaka mingi iliyopita, tiba ya kichina iliendelezwa kwa mfululizo na kuibua madaktari wengi mashuhuri pamoja na mifumo mingi ya tiba na kutungwa vitabu vingi ya tiba.
Yamegunduliwa maelezo kuhusu tiba na ugonjwa wa aina zaidi ya 10 katika maandishi yaliyochongwa kwenye magamba ya kobe ya enzi ya Yin Shang miaka zaidi ya 3,000 iliyopita. Ilipofika enzi ya Zhou, madaktari walianza kutibu wagonjwa kwa mbinu ya kuangalia, kunusa, kuuliza na kupima mapigo ya moyo pamoja na kutumia dawa, upasuaji na akyupancha. Katika enzi ya Qin na Han, kilitungwa kitabu cha nadharia ya tiba kilichojulikana kwa "Huangdineijing", ambacho ni kitabu cha kwanza cha nadharia ya tiba ya kichina.
Mbinu ya kuchunguza hali ya ugonjwa kwa kupima mapigo ya moyo ni maendeleo makubwa yaliyopatikana toka enzi ya Weijin iliyokuweko kutoka mwaka 220 hadi mwaka 589 hadi enzi ya Suitang iliyokuweko toka mwaka 581 hadi mwaka 960. Kitabu kingine kijulikanacho kwa "kitabu kipya cha dawa za miti-shamba" ni kitabu cha kwanza duniani kinachohusu dawa. Katika kipindi hicho vilitungwa vitabu vingine vya tiba.
Katika elimu ya tiba ya enzi ya Song toka mwaka 960 hadi mwaka 1279, elimu ya akyupancha ilifanyiwa mageuzi makubwa. Uvumbuzi huo una athari kubwa kwa maendeleo ya tiba ya akyupancha katika siku za baadaye.
Tiba ya nchi za magharibi iliingia China katika enzi ya Ming, baadhi ya madaktari wa China walikuwa na msimamo wa "kuunganisha tiba za kichina na za nchi za magharibi".
Nadharia ya Msingi wa Tiba ya Kichina
Nadharia ya msingi wa tiba ya kichina ni ujumlisho wa nadharia kuhusu uhai wa miili ya binadamu pamoja na kanuni ya mabadiliko ya maradhi.
Hasi na Chanya ni za eneo la falsafa ya kale nchini China. Watu waliweka hali ya mgongano katika eneo la hasi na chanya na kueleza mabadiliko ya vitu kwa kutumia mvutano kati ya hasi na chanya. Nadharia hiyo inasema kuwa uwiano mwafaka kati ya hasi na chanya ni msingi wa kudumisha hali nzuri ya miili ya binadamu, pindi uwiano huo ukivurugika binadamu ataugua. Elimu ya "wuxing" ni elimu inayoeleza uwezo na uhusiano kati ya viungo vya mwili wa binadamu kwa maeneo matano ya falsafa ya mti, moto, udongo, dhahabu na maji, inasema kuwa endapo uwiano kati ya viungo vya mwili utavurugika, binadamu ataugua.
Kuthibitisha Ugonjwa kwa Tiba ya Kichina
Daktari anatambua hali ya mgonjwa kwa mbinu ya kuangalia, kusikiliza, kunusa, kupapasa na kuongea na mgonjwa ili kuthibitisha matatizo yake na kuamua namna ya kumtibu mgonjwa.
MBINU YA KUANGALIA
Kuangalia kwa macho ni moja ya mbinu ya kuthibitisha ugonjwa kwa mujibu wa nadharia ya viungo vya mwili na mshipa wa damu na pumzi. Sehemu ya nje ya mwili inahusika moja kwa moja na viungo vya mwili ya binadamu. Endapo mabadiliko yametokea katika hali na uwezo wa viungo vya mwili, ambayo hayana budi kuleta mabadiliko katika hali ya uzima, rangi, maumbo na namna yake. Kwa hiyo daktari anaweza kuona mabadiliko ya viungo vya ndani ya mwili wa binadamu kwa kuangalia mabadiliko yanayoonekana katika sehemu ya nje ya mwili na mabadiliko ya hali na uwezo wa viungo vya usoni yaani macho, pua, mdomo na masikio.
MBINU YA KUNUSA NA KUSIKILIZA
Kunusa harufu ni mbinu nyingine ya daktari ya kuthibitisha matatizo ya mgonjwa kwa kusikiliza sauti inayotoka mwilini mwa mgonjwa na kunusa harufu ya kinyesi chake, ambazo ni pamoja na sauti za maneno yanayosemwa na mgonjwa, kupumua, kukohoa, na kupiga kwikwi na harufu inayotoka katika pua na mdomo wa mgonjwa.
MBINU YA KUULIZA
Daktari anathibitisha ugonjwa kwa mbinu ya kuongea na mgonjwa au na watu wanaofahamu hali ya mgonjwa. Lengo la mbinu hiyo ni kufahamu hali ya ugonjwa isiyoinekana nje au kutoa habari nyingine ili daktari aweze kufanya uchunguzi zaidi, habari anazotaka kujua daktari ni pamoja na kazi, ndoa, kabila, tarehe ya kuanza kuonana na daktari, magonjwa aliyowahi kuugua mgonjwa, hali yake na ya familia yake ya afya, pamoja na hali yake ya haja kubwa na ndogo.
|