16: Hadithi za Mapokeo

Hadithi Kutoka Sehemu za Utalii

Masimulizi kuhusu Mlima Wutai

Mlima Wutai ni moja kati ya milima minne maarufu kwa dini ya Buddha nchini China na pia ni sehemu ya utalii.

Mlima Wutai uko mkoani Shanxi, mlima huo una vilele vitano vilivyozunguka kwa duara, na sehemu ya kila kilele ni tambarare kama jukwaa.

Inasemekana kuwa hapo awali hali ya hewa ilikuwa mbaya sana kwenye sehemu ya Mlima Wutai, katika majira ya baridi ilikukwa baridi mzizimo, katika majira ya Spring upepo wenye mchanga unavuma kwa nguvu, katika majira ya joto jua ni kali sana, wakulima walikuwa hawapati chochote cha mazao. Mungu Wen Zhu alikuwa akieneza dini yake huko, alipoona jinsi watu walivyoteseka na hali mbaya ya hewa, aliamua kuibadilisha.

Wen Zhu alisikia kwamba kwenye bahari ya mashariki kulikuwa na jiwe moja ambalo linaweza kubadilisha hali ya hewa, alijigeuza kama sufii akaenda huko kutaka kuazima jiwe hilo.

Wen Zhu alifika bahari ya mashariki, nje ya kasri la mfalme wa dragoni aliona jiwe hilo, aliingia ndani ya kasri na kumweleza ombi lake la kuazima jiwe. Mfalme wa dragoni alimwambia, "Chochote unachotaka kuazima nakubali, isipokuwa jiwe hilo, kwa sababu jiwe hilo lilikuwa chini ya bahari kwa karne kadhaa na ilipatikana kwa miaka mingi. Watoto wangu baada ya kazi wanajiburudisha na badiri kwa jiwe hilo. Ukiondoka na jiwe hilo watoto wangu watasumbua." Wen Zhu alimshawishi kwa maneno mazuri na kumweleza jinsi watu walivyoteseka kwa hali mbaya ya hewa.

Mfalme aliona vibaya kumkatalia, na huku akifikiri mzee huyo Wen Zhu atashindwa kubeba jiwe hilo zito, basi akamwambia, "Jiwe hilo ni zito sana, sina watu wa kukusaidia, kama ukiweza basi chukua!"

Wen Zhu alimshukuru, alifika mbele ya jiwe na kunong'onona maneno fulani mdomoni, mara jiwe hilo likawa dogo kama gololi, akatia mfukoni na kuondoka nalo. Mfalme wa dragoni alipigwa bumbuazi, akajuta sana.

Alipofika kwenye Mlima Wutai jua lilikuwa kali sana, kutokana na ukame, ardhi ilipasuka. Wen Zhu aliliweka jiwe hilo kwenye bonde, ajabu ilitokea: sehemu zote za kileleni zikawa malisho, hali ya hewa ikawa baridi. Watu walijenga hekalu kubwa. Hadi sasa Mlima Wutai pia unaitwa Mlima wa Baridi.

Mlima Wutai ni hifadhi ya kimaumbile ya kitaifa. Hivi sasa kuna mehekalu 42, kati ya mahekalu hayo, mahekalu ya Nantansi na Foguangsi yamekuwepo kwa miaka 1200.

Mlima Wutai ni sehemu maarufu ya utalii, kuna majabali yenye sura za ajabu, kuna michirizi na miti ya aina kwa aina, kwenye kilele theluji haiyeyuki, hata katika majira ya joto huko hali ya hewa huko ni baridi baridi.

Hadithi kuhusu Ziwa la Xihu

Ziwa la Xihu liko katika mji wa Hangzhou, mashariki mwa China. Katika karne ya 14, mtalii wa Itali Makopolo alipotembelea huko alisifu, "Mtu akiwa huko anajiona kama yuko peponi."

Ziwa la Xihu linazungukwa na mlima kwa pande tatu, mandhari yake inavutia sana. Washairi mashuhuri wa kale karibu wote waliwahi kufika huko na kuandika mashairi kusifu mandhari ya huko.

Ziwa la Xihu likitajwa watu hukumbuka mandhari katika sehemu kumi toka jua linapochomoza mpaka linapozama.

Kuna masimulizi mengi kuhusu Ziwa la Xihu. Moja kati ya masimulizi hayo ni "Daraja Lililokatika", au kwa jina jingine ni "Hadithi ya Joka Jeupe".

Inasemekana kwamba kulikuwa na majoka mawili yenye miaka elfu moja, ambyo yalijigeuza kuwa wasichana wawili na kuja kwenye Ziwa la Xihu kujiburudisha. Walipofika kwenye daraja lililokatika msichana aliyekuwa joka jeupye alimkuta msomi mmoja, akampenda moyoni, wakati huo mvua kubwa ilikuwa inanyesha, msomi alijikinga mvua kwa mwavuli kwenye kando ya mashua.

Msomi huyo alipowaona wasichana hao walikuwa wamelowa mvua, aliwaazima mwavuli na yeye mwenye aliacha mvua imnyeshee. Yeye alimpenda zaidi msichana mwenye asili ya joka jeupe. Kwa msaada wa msichana mwenye asili ya joka jeusi, wao walioana. Baada ya ndoa msichana Joka jeupe alifungua duka la dawa na alipendwa sana na wenyeji.

Sufii aitwaye Fa Hai alifahamu wasichana hao walikuwa majoka, kisirisiri alimwambia msomi huyo. Sufii alimwambia, amshawishi mkewe anywe pombe katika siku fulani, akiwa joka atajirudisha asili yake. Baada ya kunywa pombe, mkewe kweli alijirudisha kuwa joka, msomi alipoona jinsi mke alivyo alikufa kwa hofu. Ili kumwokoa mumewe joka jeupe lilisafiri kwenda mbali kwa shida na kufika kwenye mlima mmoja ambako inasemekana kwamba kuna majani ya dawa ya kuweza kumwokoa mumewe. Baada ya kutumia dawa hiyo, mumewe alifufuka.

Katika siku asipokuwepo joka jeupe, Fa Hai alimdanganya msomi kwenda kwenye hekalu na kumzuia huko asiweze kurudi nyumbani. Wasichana hao wawili walikwenda kwenye hekalu kumrudisha msomi, katika purukushani mke wa msomi alipigwa, kwa sababu alikuwa karibu kuzaa, alikimbia kwa kulindwa na mwenzake joka jeusi.

Walipofika kwenye daraja lililokatika, walimkuta msomi. Hao mume na mke walikumbatiana na kulia sana. Wakati huo Fa Hai alikuja na kumkamata joka jeupe na kumzika chini ya pagoda ya Leifeng.

Baada ya miaka mingi kupita, joka jeusi alijipatia uhodari wa kupigana, alirudi kwenye ziwa la Xihu, alimshinda Fa Hai na kukausha maji ya ziwa la Xihu, aliangusha pagoda ya Leifeng na kumwokoa joka jeupe. Hadithi ya kuachana na kukutana kwa msomi na mkewe inasimuliwa miaka hadi miaka, na kila watu wanapofika kwenye ziwa la Xihu hukumbuka hadithi hiyo.

Hekalu la Yonghegong

Mjini Beijing kuna jengo lenye mitindo ya makabila ya Wahan, Wamen, Wamongolia na Watibet, hilo ni hekalu la Yonghegong.

Yonghegong ni hekalu la dini ya Buddha la madhehebu ya Tibet, eneo lake ni mita za mraba elfu 60, kuna vyumba zaidi ya elfu moja. Hekalu hilo lilijengwa na mfalme wa Enzi ya Qing, Kangxi, mwaka 1694 kwa ajili ya mtoto wake wa nne Yinzhenbeile, lakini mwaka 1723 mtoto huyo alirithi kiti cha ufalme na alihamia kasri la kifalme la Beijing, aliliacha hekalu hilo kwa dini ya Buddha ya madhehebu ya Tibet.

Madhehebu ya Tibet ya Dini ya Buddha yalianzishwa na Zhakba (1375-1419).

Vitu vya kale ndani ya hekalu hilo ni vingi. Kati ya vitu hivyo kuna "maajabu matatu".

Ajabu la kwanza ni mlima wenye sanamu mia tano. Mlima huo una kimo cha mita 4 na urefu wa mita 3. Mlima huo ulichongwa kwa mbao. Kwenye mlima huo umechongwa mapango, vibanda, pagoda, miti, michirizi, ngazi na sanamu. Lakini bahati mbaya sanamu zilizokuwa mia tano hapo awali sasa zimebaki 449 baada ya miaka yenye vurugu za vita katika historia.

Ajabu la pili ni sanamu ya Buddha ndani ya ukumbi mkuu wa hekalu hilo. Kimo cha sanamu hiyo ni mita 26, kati ya mita hizo, mita nane ziko chini ya ardhi.

Sanamu hiyo juu ya ardhi ina urefu wa mita 18, kipenyo chake ni mita 8, uzito ni tani 100, ni sanamu kubwa kabisa duniani iliyochongwa kwa gogo zima. Mwaka 1979 sanamu ilipokarabatiwa, mafundi waligundua kwamba sehemu ya chini bado haijaoza.

Ajabu la tatu ni sanamu ya shaba, nyuma ya sanamu hiyo ni sahani kubwa ya shaba nyekundu yenye michongo ya miale ya jua, chini ya mwangaza, mishale inang'ara nyuma ya kichwa cha sanamu hiyo.

Kwenye nguzo mbili zilizo kando ya sanamu hiyo yalichongwa majoka 99 yaliyoonekana kama ya kweli. Ndani ya ukumbi huo kuna pagoda tano zilizopakwa rangi ya dhahabu na jiwe kubwa lililochongwa kwa maandishi ya makabila manne ya Wahan, Waman, Wamongolia na Watibet. Tokea mwaka 1981 China ilipoanza kufungua mlango kiuchumi, kila mwaka watalii kiasi cha milioni wanatembelea hekalu hilo.

Pagoda ya Mbao Mkoani Shanxi

Nchini China kuna pagoda nyingi za dini ya Buddha. Dini ya Buddha nchini China ilianzia India, lakini pagoda ya dini ya Buddha imechanganya mtindo wa Kichina.

Pagoda ya mbao mkoani Shanxi ilianza kujengwa mwaka 1056 na kumalizika baada ya miaka 140. pagoda hiyo ilijengwa juu ya jukwaa lenye kimo cha mita 4, urefu wa pagoda hiyo ni mita 70 na shina lake lina kipenyo cha mita 30. Pagoda hiyo ilitumia mbao mita za ujazo 3000, uzito wake ni kiasi cha tani 3000.

Umbo la pagoda hiyo ni la pembe nane, lina matabaka 9 na nguzo 28 kwa nje na nguzo 8 kwa ndani.

Kwenye upenu wa kila tabaka kuna kengele, upepo unapovuma kengele hizo zinalia.

Tokea pagoda hiyo ijengwe hadi sasa, katika muda wa miaka zaidi ya 900, iliwahi kukumbwa na matetemeko mengi ya ardhi. Kutokana na rekodi ya historia, miaka 300 baada ya pagoda hiyo kumalizika kujengwa, lilitokea tetemeko kubwa la ardhi, na liliendelea kwa siku 7, lakini pagoda hiyo ilikuwa nzima.

Kabla ya ukombozi wa China, mabwana vita waliendelea kupambana, pagoda hiyo iliwahi kupigwa mabomu ya mzinga zaidi ya 200, lakini pagoda hiyo haikudhurika.

Uimara wa pagoda hiyo unatokana na usanifu wake wa kisayansi, fremu iliposanifiwa ilizingatia matetemeko ya ardhi, na sababu nyingine ni kuwa pagoda hiyo ilijengwa kwa mbao tupu ambazo zina tabia ya kunyumbulika.

Pagoda hiyo haikuwahi kupigwa na radi, kwa sababu ina waya nene iliyochomekwa ndani ya ardhi kwa kina, na pembezoni mwa pagoda hiyo pia kuna miyororo 8 ya chuma iliyofukiwa ndani ya ardhi. Pagoda hiyo imeonesha wazi ufundi mkubwa wa mafundi wa China ya kale, na elimu kubwa ya uwiano na kinga dhidi ya radi.

Hadithi kuhusu Kasri la Potala

Kasri la Potala ni jengo Dini ya Buddha liliko kwenye paa la dunia, Tibet.

Kasri la Potala lilijengwa na mfalme wa Tibet Sonzanganbu katika karne ya saba kwa ajili ya kumkaribisha binti wa mfalme wa Enzi ya Tang Wen Cheng kuwa mke wake. Kasri hilo lilijengwa kwenye mlima wa Tibet.

Katikati ya kasri hilo kuna ukumbi wa kufanyia ibada, ndani ya ukumbi huo kuna sanamu za Sonzangambu, binti wa mfalme wa mfalme wa Enzi ya Tang, Wen Cheng.

Kasri la Potala ni jengo lenye mchanganyiko wa mitindo ya Dini ya Buddha, madhehebu ya Tibet na kabila la Wahan, na ni alama ya ndoa kati ya kabila la Watibet na kabila la Wahan katika miaka 1300 iliyopita

Katika karne ya saba, Sonzanganbu alikuwa mfalme wa Enzi ya Turufan huko Tibet, alikuwa mfalme anayewapenda raia wake na kufanya enzi yake iimarike siku hadi siku. Ili kuweka uhusiano mzuri na Enzi ya Tang na kuingiza utamaduni wa kimaendeleo, Songzanganbu aliamua kumposa binti wa mfalme wa Enzi ya Tang, Wen Cheng. Kwa sababu wakati huo madola mengine pia yalituma wajumbe kuleta posa kwa binti yake, mfalme wa Enzi ya Tang, Tang Taizong aliwatolea maswali matatu, mtu ambaye angejibu vizuri maswali yote matatu, atakubali kumwoza binti yake kwa huyo.

Swali la kwanza: Katika busatani kuna magogo matatu ambayo mviringo wa pande mbili ni sawa, upande gani ni shina? Songzanganbu alijibu, magogo yote yawekwe ndani ya maji, upande uliozama zaidi ndio upande wa shina, kwa sababu upande wa shina ni mzito zaidi.

Swali la pili: Mfalme alitoa jade moja, na ndani ya jade kuna kitundu kilichopinda pinda kutoka upande moja hadi upande mwingine. Mfalme alimtaka apitishe uzi. Songzangambu alipaka asali kwenye upande mmoja, na kufunga uzi kwenye kiuno cha siafu na kumtia upande mwingine, siafu huyo alitambaa kutoka upande mmoja na kutoka kutoka upande mwingine na uzi.

Swali la tatu: Farasi mmoja ana mtoto wake anayenyonya maziwa, anawezaje kutofautisha mama farasi na mtoto wake kati ya kundi la wafasi wengi?

Songzanganbu alitafakari, kisha akasema, farasi wakubwa na wadogo wafungwe ndani ya mazizi mawili, na siku ya pili wafunguliwe, mtoto wa farasi aliyekimbilia farasi mkubwa na kunyonya maziwa yake, hao ndio mama na mtoto.

Baada ya Sonzanganbu kujibu maswali yote hayo sawasawa, mfalme aliongeza swali jingine, alitaka kumtambulisha binti yake Wen Cheng kati ya wasichana wengi. Kabla ya hapo, Songzanganbu alipata habari kwamba Wen Cheng alipenda kutumia manukato inayowavutia nyuki. Katika siku ya kutofautisha binti wa mfalme na wasichana wengine, alitia nyuki nguoni, aliachia nyuki mbele ya wasichana, nyuki walimrukia Wen Cheng. Mfalme Tang Taizong aliona kuwa kweli Songzanganbu ni mwerevu sana, alikubali kumwoza binti yake.

Songzanganbu alifurahi sana, alijenga kasri lenye vyumba 999 kwa ajili ya kumkaribisha binti wa mfalme Wen Cheng, kasri hilo ndio Kasri la Potala.

Hekalu Linalokuwa Hewani Mkoani Shanxi

Kama tujuavyo, mahekalu hujengwa juu ya ardhi, lakini kuna hekalu moja lilijengwa hewani mkoani Shanxi. Hekalu hilo liko karibu na mji wa Tatong mkoani Shanxi, hekalu hilo lilijengwa miaka 1400 iliyopita.

Hekalu hilo lilijengwa kwenye genge la mlima, linaonekana kama liko hewani ambalo liko mita 50 juu ya ardhi, chini ya hekalu hilo kuna nguzo zaidi ya kumi zinazohimili. Hekalu hilo lina vyumba 40, watu wanapokuwa kwenye hekalu hilo wanahofia kuwa huenda hekalu hilo litaanguka, ingawa sakafu ya mbao inalialia inapokanyagwa lakini hekalu hilo ni madhubuti kabisa.

Juu ya hekalu hilo kilele cha mlima kinajitokeza nje kama mwavuli ukikinga mvua, mafuriko yakitokea katika bonde la mlima hayaathiri hekalu. Ingawa hekalu hilo lilijengwa kwa mbao, lakini lilipita milenia moja salama.

Kwa kweli hekalu hilo halisimamishwi na nguzo zaidi ya kumi, bali linasimamishwa na magogo yaliyogongomelewa ndani ya majabali, na magogo hayo yaliwahi kuloweshwa ndani ya mafuta.

Hekalu hilo lilijengwa kwa kufuata mazingira pembeni. Nyuma ya ukumbi lilichimbwa pango ili kuongeza ukubwa wa ukumbi. Kuna njia nyembamba inayopindapinda mlimani na kufikia hekalu hilo.

Watu watauliza, kwa nini hekalu linajengwa gengeni? Hapo awali sehemu ya hekalu hilo ilikuwa ni kipito, ili kurahisisha waumini wafanye ibada hekalu lilijengwa huko. Zaidi ya hayo, chini ya mlima kuna korongo, na mara kwa mara kuna mafuriko, watu wa kale waliamini kuwa kama hekalu likijengwa huko linaweza kutuliza mafuriko. Kwenye jabali karibu na hekalu yamechongwa maneno "Ufundi mkubwa wa Gongshu". Gongshu alikuwa ni fundi mkubwa aliyeishi miaka elfu mbili iliyopita, maneno hayo yanamaanisha kuwa ufundi wa hekalu hilo ni kama ufundi wa Gungshu.

Hadithi kuhusu Kasri la Kifalme Mjini Shenyang

Kasri la Kifalme mjini Shengyang ni kasri la pili kwa ukubwa likilinganishwa na Kasri la Kifalme la Beijing. Tofauti yake na kasri la Beijing ni kuwa mtindo wake wa majengo ni wa kabila la Waman.

Kasri la Kifalme la Mji wa Shenyang liko katikati ya mji huo, lilijengwa katika Enzi ya Qing (1616-1911). Wafalme wawili wa mwanzo wa Enzi ya Qing waliishi katika kasri hilo, na baadaye kabila la Waman lilipindua Enzi ya Ming na kuhamia mji mkuu wa Enzi ya Qing, Beijing, na kujenga Kasri la Kifalme la Beijing.

Kasri hili lina eneo la mita za mraba elfu 60, lina majengo zaidi ya 70 na vyumba zaidi ya 300. Ukumbi mkuu wa kasri hilo ni mahali pa kufanyia sherehe kubwa na kufanya kazi za serikali, kuna vibanda vikubwa 11 ndani ya kasri hilo, ambavyo vinamaanisha mahema ya kabila la Waman wanaoishi kwa ufugaji.

Mbele ya kasri kuna milingoti 7, na juu ya kila mlingoti kuna bakuli la risasi. Kutokana na mila ya kabila la Waman, wanapofanya tambiko walikuwa wanaweka chakula kwenye bakuli hilo ili kuwalisha ndege.

Ingawa kasri hilo lilijengwa kwa mtindo wa kabila la Waman, lakini lilipojengwa utamaduni wa kabila la Wahan ulikuwa umeanza kupokelewa na kabila hilo, kwa hiyo, ukumbi mkuu wa kasri hilo ulijengwa kwa mtindo wa kabila la Wahan ulipokuwa katika Enzi ya Song (960-1279).

Kasri hilo lilianza kujengwa mwaka 1625 na kukamilika baada ya miaka 10, na baadaye wafalme wa Enzi ya Qing walifanya ukarabati na kuongeza majengo katika muda wa miaka 150. kasri hilo lilichanganya sanaa za makabila ya Wahan, Waman, Wamongolia, Wahui na Watibet, ni alama ya muunganisho wa makabila ya China.

Hadithi kuhusu Magenge Matatu ya Mto Changjiang

Mto wa Changjiang ni mto wa kwanza mkubwa nchini China na ni wa tatu kwa ukubwa barani Asia. Katika sehemu ya mwanzo na ya kati kuna magenge matatu ambayo kwa jumla yana urefu wa kilomita karibu mia mbili. Mandhari ya kando mbili za magenge hayo matatu inavutia na ni sehemu maarufu ya utalii duniani.

Katika magenge hayo matatu kuna mji mmoja inaoitwa Baidi. Jina hilo lilitokana na hadithi moja, mhusika mkuu katika hadithi hiyo aliitwa Gong Sunshu.

Mwaka 25 China ilikuwa katika hali ya kubadilisha enzi, Enzi ya Han Magharibi ilipinduliwa na uasi wa wakulima na enzi mpya ilikuwa haijaanzishwa, jemadari wa jeshi lililokalia sehemu ya kusini magharibi ya China alisubiri fursa yake ya kunyakua utawala wa China nzima.

Siku moja Gong Sunshu aliota ndoto, kwenye ndoto alisikia mtu mmoja akimwambia, "Utakuwa mfalme wa miaka 12." Baada ya kuzinduka alipotembea katika bustani yake aliona kuna moshi mweupe unaotoka kisimani, moshi huo ulionekana kama dragoni, Sun Gongshu aliona hii ni dalili ya yeye kupata ufalme, basi alijitawaza kuwa mfalme kwa jina la Baidi, na kuita mji aliokaa kuwa "mji wa Baidi", na kupanga askari wengi kuulinda.

Gong Sunshu alikuwa na rafiki mmoja mkubwa, aliitwa Ma Yuan. Huyo Ma Yuan alikuwa na elimu kubwa, aliposikia Gong Sunshu amejitawaza kuwa mfalme alikuja kutoka mbali kutaka kuonana naye. Lakini hakutegemea kwamba Gong Sunshu alijigamba na kumwamuru abadilishe nguo yake kwa nguo ya kiraia kabisa, kisha alikutana naye huku akiwa anashangiliwa na askari wake wengi. Gong Sunshu alimteua Ma Yuan kuwa jemadari. Wafuasi wa Ma Yuan walitumai wangepewa nyadhifa fulani, lakini Gong Sunshu aliwaambia kwamba, "Hivi sasa jamii inavurugika sana, siwezi kuwapokea." Gong Sunshu hakufahamu kuwa huu ndio wakati wa kupokea watu hodari kushauriana mambo makubwa ya taifa.

Wakati huo Liu Xiu alikuwa ameanzisha mamlaka yake, alimwandikia barua Gong Sunshu kumshawishi ajiunge naye. Lakini Gong Sunshu aliona kuwa yeye ni mfalme, anawezaje kusalimu amri, alikataa, Mwaka 37 Liu Xiu aliongoza jeshi lake kumshambulia, Gong Sunshu aliuawa vitani.

Gong Sunshu alikuwa mfalme kwa miaka 12 na baadaye aliuawa. Toka mwanzo mpaka mwisho Gong Sunshu alitawala sehemu ya kusini magharibi kwa miaka 28. Kutokana na kuwa katika muda huo wa miaka 28 jamii ya sehemu hiyo ilikuwa tulivu, na kilimo kilipata maendeleo. Kwa hiyo baada ya Gong Sunshu kufariki wenyeji walimjengea "hekalu la Baidi" kumkumbuka.

Kwenye magenge matatu kuna sehemu nyingi za utalii na masimulizi ya kale. Kuna vilele 12 vya milima, watu waliviita "vilele vya malaika" na walitunga hadithi nyingi kuhusu vilele hivyo.

Hivi sasa miradi ya hifadhi ya maji inatekelezwa katika sehemu ya magenge matatu, kutokana na miradi hiyo, baadhi ya sehemu za utalii zilitoweka, lakini sehemu nyingine za utalii zilitokea.

Hadithi kuhusu jiwe la kaburi lisilo na maandishi

Mkoani Shanxi, magharibi mwa China, lipo kaburi moja lenye miaka zaidi ya elfu mbili sasa. Katika historia ndefu ya jamii ya kimwinyi ya China kaburi hilo ni la pekee na la ajabu kwa sababu ndani yake wamezikwa wafalme wawili, mfalme wa Enzi ya Tang aliyejulikana kama Li Zhi, na mfalme wa kike wa Enzi ya Zhou aliyejulikana kama Wu Zetian. Wafalme hao wawili licha ya kuwa wawakilishi wa enzi mbili lakini pia walikuwa mume na mke. Wu Zetian alikuwa mfalme pekee wa kike katika historia ya China, ambapo maisha yake yalikuwa na maajabu mengi. Baada ya kifo chake, mbele ya kaburi lake lilisimamishwa jiwe moja lakini halikuandikwa hata neno moja juu yake. Hivi leo maombi yamewasilishwa ya kuingiza kaburi hilo katika orodha ya kumbukumbu za utamaduni duniani. Ifuatayo ni hadithi juu ya jiwe hilo la kaburi.

Wu Zetian alizaliwa mwaka 624. Alipokuwa na umri wa miaka 14 alichaguliwa kuwa mjakazi wa mfalme wa pili wa Enzi ya Tang, yaani Tang Taizong. Wu Zetian alikuwa na tabia ya ukali na kufanya maamuzi bila kusita. Mathalan, mfalme Tang Taizong alikuwa na farasi mmoja mkali, hapana mtu yeyote aliyeweza kumfundisha, lakini Wu Zetian alimwambia mfalme wake, "Niachie mimi, lakini nataka mjeledi wa chuma na jambia. Kwanza nitajaribu kumfundisha kwa mjeledi, nikishindwa nitampiga kichwani, na nikishindwa tena nitamkata koo lake kwa jambia." Ah, kusikia hayo mfalme Tang Taizong alishituka, akashangaa kuwa katika jamii ya kimwinyi yenye miiko mingi kwa wanawake hawapaswi kusema maneno kama hayo. Lakini mwana mfalme Li Zhe alimpenda sana mwanamke huyo aliyemzidi kwa miaka minne.

Baada ya mfalme Tang Taizong kufariki dunia, Wu Zetian akawa mtawa kufuatana na taratibu za kimwinyi, na mtoto wa mfalme Li Zhi akarithi kiti cha ufalme kwa jina la kifalme la Tang Gaozong. Li Zhi hakumsahau Wu Zetian hata siku moja, kwa hiyo muda si mrefu baadaye akamrudisha ndani ya kasri na kumfanya kuwa kijakazi wa kwanza. Lakini Wu Zetian alikuwa haridhiki na hali yake, akitamani sana kuwa mke halisi wa mfalme, basi akatega mtego wa kinyama. Mama Tang Gaozong alikuwa mgumba, lakini aliwapenda sana watoto. Siku moja alikwenda kumwangalia mtoto wa kike wa Wu Zetian aliyezaliwa siku chache zilizopita. Baada ya mke wa mfalme kuondoka tu chumbani mara Wu Zetian akamwua binti yake kwa kumkaba shingoni, kisha akamfunika kwa mfarishi kama kawaida. Baada ya dakika chache, mfalme Tang Gaozong aliingia ndani kumtazama mtoto wake, alipofunua mfarishi akagundua kwamba mtoto amekwishakata roho, alishangaa sana. Wakati huo Wu Zetian alikuwa akilia na kuzirai. Mfalme aliwadadisi vijakazi kutaka kujua mtu aliyewahi kuingia chumbani. Wote walimwambia hakuna yeyote ila mkewe. Mfalme alighadhibika vibaya, aliamini kwamba muuaji ni mkewe, na kuanzia hapo alimchukia sana, mwishowe alimwondoa na kumteua Wu Zetian kuwa mke wake.

Baada ya kupata hadhi ya kuwa mke wa mfalme, Wu Zetian alianza kushiriki katika shughuli za utawala bila kujali utaratibu wa kimwinyi ambao haukuruhusu wanawake kuingilia mambo ya serikali. Hatimaye mfalme alimwachia Wu Zetian madaraka yote, mawaziri wakawaita "watakatifu wawili".

Baada ya mfalme Tang Gaozong kufariki, Wu Zetian alikuwa amejikusanyia madaraka yote, akajitawaza kuwa mfalme alipokuwa na umri wa miaka 67, akabadilisha enzi ya Tang kuwa Enzi ya Zhou. Alikuwa mtu mwenye umri mkubwa kuliko wengine alipochukua wadhifa wa kuwa mfalme na pia ni mfalme pekee wa kike katika historia ya China.

Baada ya Wu Zetian kuchukua madaraka, aliwalea maofisa wake kuwa wakatili kama yeye, kuwaua watu hovyo na kuondoa kabisa wale waliotofautiana naye kimawazo, aliwaua jamaa wote wenye nasaba ya wafalme wa Enzi ya Tang na hata mtoto wake wa kiume. Mawaziri Xu Jingye na Luo Binwang wa Enzi ya Tang walipania kurudisha utawala wa enzi ya zamani ya Tang, walifanya uasi katika mji wa Yang Zhou. Luo Binwang aliandika makala kumshutumu Wu Zetian na kutawanya kote nchini. Baada ya kuisoma Wu Zetian aliinamisha kichwa kwa tabasamu, akawauliza mawaziri, "Ni nani aliyeandika makala hii?" Mawaziri wakamwambia, "Luo Bingwang." Akauliza zaidi, "Mtu hodari kama huyo mbona ameachwa vijijini?", basi papo hapo akatuma askari laki tatu akawaua wote wawili baada ya kupigana vita nao.

Lakini tukimwangalia kutoka upande mwingine, Wu Zetian pia ana sifa nzuri, kwamba alitumia sera mwafaka kuendeleza kilimo, alieneza mfumo wa mtihani wa kifalme wa raia ambao ni mfumo wa kuchagua maofisa kutoka kwa raia, alithamini na kutumia watu hodari na alipandisha hadhi ya wanawake. Wu Zetian alikalia kiti cha mfalme kwa miaka 15, lakini hali ilivyo ni kuwa aliendesha utawala kwa nusu karne. Chini ya utawala wake, China ilikuwa imeimarika kwa nguvu, jamii ilikuwa ya utulivu, idadi ya watu iliongezeka, uchumi ulistawi, na mara kadhaa alisambaratisha mashambulizi ya maadui. Aliweza kuendeleza zaidi ustawi aliourithi kutoka Enzi ya Tang katika Enzi yake ya Zhou.

Wu Zetian aliishi miaka 82, mwili wake ulizikwa pamoja na mumewe mfalme Tang Gaozong, mbele ya kaburi lilisimamishwa jiwe moja lisilokuwa na maandishi yoyote. Hili ni jiwe kamili, lina urefu wa mita nane na upana wa mita mbili, na lina nakshi nzuri. Kutokana na jiwe hilo kutokuwa na maandishi yoyote limetokea kuwa maarufu sana. Kuna mawazo ya aina mbalimbali kuhusu jiwe hilo. Baadhi wanasema, jiwe hili liliachwa tupu kutokana na taabu ya Wu Zetian kujisifu, kwa sababu aliona sifa zake haziwezi kuelezwa kwa maneno; Baadhi wanasema kwamba yeye alipindua utaratibu wa wanaume kutawala, hivyo alijua kosa lake kubwa, kwa hiyo aliona hakuwa na sifa ya kujipatia jiwe lenye maandishi; Lakini baadhi wanasema tofauti kwamba wote waliozikwa ni wafalme, tena ni mume na mke, kwa hiyo upo utata wa cheo, ama ni mke wa mfalme Tang Gaozong wa Enzi ya Tang, au mfalme Wu Zetian wa Enzi ya Zhou. Kutoandika chochote juu yake ni mchepuo wa yote hayo kwa busara. Watu wengi zaidi wanaona kuwa kutoandika lolote ni ujanja wake, kwa kuwa yeye mwenye alijua watu wangekuwa na tathimini tofauti juu yake, na maneno yasingeweza kueleza jinsi maisha yake yalivyokuwa, kwa hiyo aliacha jiwe bila neno na kuwaachia watu wa baadaye wazungumze watakavyo.

Hadithi kuhusu Mlima Lushan

Mlima Lushan ulioko mkoani Jiangxi, kusini mwa China una mandhari ya kuvutia. Tokea enzi na dahari mlima huo unasimuliwa kwa hadithi nyingi.

Katika sehemu ya kaskazini mkoani Jiangxi, mlima huo unajulikana kwa sura zake nyingi za ajabu. Wasomi wengi waliwahi kutembelea mlima huo na waliacha mashairi mengi na picha nyingi. Mshairi mkubwa Li Bai aliyeishi katika karne ya nane Enzi ya Tang aliwahi kuandika shairi lake la kueleza maporomoko ya maji, "Chini ya jua moshi wa udi wapaa hewani kutoka mahekalu, kwa mbali maporomoko ya maji yaonekana kama yaanguka kutoka mbinguni." Mwanafasihi mkubwa wa Enzi ya Song (960-1127) Su Shi alipotembelea mlima huo alieleza kuwa kutoka juu vilele vya mlima vinatofautiana kwa urefu, na huwezi kuona mlima huo Lu Shan ulivyo kwa sababu wewe upo ndani mlima huo."

Inasemekana kwamba karne ya nne Enzi ya Zhou alikuwepo bwana mmoja aliyeitwa Kuang Su, alitawa katika mlima huo na kujaribu kupata uchawi. Mfalme wa Enzi ya Zhou aliposikia habari juu yake, alituma watu mara kadhaa kwenda mlimani kumwalika, lakini Kuang Su alikataa. Baadaye Kuan Su alitoweka, watu walidhani kuwa yeye amekuwa mungu, kwa hiyo watu waliupatia mlima huo kuwa jina jingine, Mlima Kuang.

Mwaka 381 sufii mmoja aitwaye Hui Yuan aliongoza wanafunzi wake kwenda huko na kujenga jumba la watawa linaloitwa Donglinsi, kwa hiyo mlima huo pia ni chanzo cha dini ya Buddha katika sehemu ya kusini ya China. Hui Yuan alikuwa huko kwa miaka 36, kutokana na kuwa aliwasimamia watawa kwa nidhamu kali aliheshimiwa sana.

Kuhusu jumba la Donglinsi na Hui Yuan mwenyewe pia kuna hadithi nyingi. Inasemekana kuwa jumba hilo lilipojengwa vifaa vya ujenzi viliishiwa, Hui Yuan alisumbua sana kila siku. Lakini ghafla siku moja radi ilipigwa mbinguni na mvua kubwa ilinyesha, watawa wote walizuiliwa nyumbani. Siku ya pili jua lilichomoza, na mbele yao lilitokea ziwa moja, na juu ya maji magogo mengi yalielea. Hui Yuan aliamini kuwa magogo hayo yaliletwa na mungu, kwa hiyo alitumia magogo hayo na kujenga ukumbi mmoja mkubwa.

Mbele ya jumba la Donglinsi kuna ziwa moja, na ndani ya ziwa hilo kuna mayungiyungi mengi, mandhari ilikuwa ya kuvutia sana. Inasemekana kuwamba ziwa hilo lilichimbwa na mtu mmoja aitwaye Xie Lingyuan. Huyo Xie Lingyuan alitaka kuwa mtawa lakini alikataliwa na Hui Yuan kwa kuona kuwa yeye sio mtu mtulivu. Hui Yuan alimwambia, afadhali achimbe ziwa moja na awe mtulivu kama maji ya ziwani, kisha atapokelewa kuwa mtawa. Kweli alichimba ziwa hilo na alipokelewa. Baada ya Hui Yuan kufariki, Xie Lingyuan alihuzunika sana, alimwandikia kumbukumbu kwenye jiwe mbele ya kaburi lake.

Licha ya utamaduni, mandhari ya kimaumbile ya Mlima Lushan pia inavutia sana, ni sehemu maarufu ya utalii.

Hadithi kuhusu Mlima Huangshan

Mlima Huangshan uko kusini mwa China, ni urithi wa kimaumbile duniani. Hapo awali mlima huo uliitwa Yishan, maana yake ni mlima mweusi. Lakini kwa nini baadaye umeitwa mlima Huangshan?

Katika masimulizi ya kale, Huangdi ni babu wa wazawa wa taifa la China, alikuwa mtawala kwa miaka zaidi ya mia moja, na alipendwa sana na watu wake. Baadaye kutokana kuzeeka sana, na yeye alikuwa hataki kuondoka duniani, basi baada ya kumwachia kiti chake cha ufalme kijana mmoja aitwaye Shao Hao alikwenda kutafuta njia ya kurefusha maisha yake.

Dini ya Dao ni dini pekee inayopatikana nchini China. Katika historia ya Dini ya Dao waumini walikuwa na mila ya kutengeneza dawa ya kurefusha maisha. Huandi alifuatana na wengine wawili kwenda kutafuta mahali panafaa kutengeneza dawa hiyo.

Walisafiri sana kila mahali nchini China na mwishowe walifika Mlima Yishan. Waliona mlima ulikuwa mrefu sana na hata ulichomeka mbinguni, na mawingu mwepesi ulikuwa kama shashi kila wakati, mabonde yalikuwa ya kina sana, waliona huko panafaa kutengeneza dawa ya kurefusha maisha.

Walikuwa kila siku wakichoma makaa na kutafuta mimea ya dawa mlimani, walichemsha mimea waliyochagua na kuchemsha siku hadi siku, mwaka hadi mwaka mpaka walipata dawa hiyo baada ya miaka 480. Huangdi alimeza donge moja, mara akaona mwili ukawa mwepesi, hata ndevu za mvi zikabadilika kuwa nyeusi, lakini makunyanzi yalikuwa bado yapo.

Wakati huo ghafla maji ya chemchemi ulitiririka kutoka mlimani, maji hayo yalikuwa mekundu na yenye harufu nzuri. Huangdi alioga kwa maji hayo kwa siku saba, ngozi yake ilikuwa laini na makunyanzi yalitoweka, alionekana kama kijana mbichi, Huangdi alikuwa hana wasiwasi wa kufariki. Tokea hapo Mlima Yishan ulipewa jina la Huangshan.

Mandhari inayovutia sana ni "kalamu yenye maua". Ndani ya bonde kuna nguzo ndefu sana, sehemu yake ya chini ni ya mviringo kama kalamu, na sehemu ya juu ni nyembamba kama ncha ya kalamu, kwenye nguzo hiyo kuna miti misonobari ambayo ni kama maua, kwa hiyo watu husema "kalamu yenye maua".

Inasemekana kwamba mshairi mkubwa wa kale Li Bai aliwahi kuota ndoto. Katika ndoto yake aliona mawingu yaliyoelea kama bahari na maua na majani yalistawi sana, ghafla kalamu kubwa ilichomeka kutoka baharini, na kalamu hiyo ilikuwa ndefu kama nguzo, aliwaza: itakuwa ni furaha kama angepata kalamu hiyo na bahari iwe wino.

Alipofikiri hivyo ghafla alisikia muziki na huku aliona miangaza yenye rangi mbalimbali ilitokea na kisha kwenye ncha ya kalamu yalichanua maua, alijaribu kufikia kalamu hiyo, lakini alipoikaribia alizinduka.

Baada ya kuzinduka, alikuwa akikumbuka ndoto yake, alitia nia ya kutafuta kalamu hiyo, mwishowe alifika Mlima Huangshan aliiona, alishituka na kusema, "Ala, kumbe kalamu niliyoota iko hapa." Inasemekana kwamba tokea alipoona kalamu hiyo, mashairi mazuri yalikuwa mengi chini ya kalamu yake.

Hadithi kuhusu Bustani ya Jinci

Bustani za kale katika sehemu ya China zinajulikana sana, lakini katika sehemu ya kaskazini ya China pia kuna bustani maarufu, bustani hiyo ndio Bustani ya Jinci katika mji wa Taiyuan mkoani Shanxi.

Bustani ya Jinci iko kiungani mwa mji wa Taiyuan upande wa kusini magharibi. Katika bustani hiyo kuna kumbi, majumba ya ghorofa, vibanda, madaraja na maziwa, mandhari ni kama picha ya kuchorwa.

Mwaka 1064 mwanzilishi wa Enzi ya Zhou, mfalme Zhou Wuwang alifariki dunia miaka miwili baada ya yeye kuangamiza Enzi ya Shang, mtoto wake wa kiume alirithi kiti chake cha ufalme, aliitwa mfalme Zhou Chengwang. Kwa sababu alikuwa mtoto mdogo, kila siku alibebwa na waziri Zhou Gong kupanda jukwaa kuwapokea salaam za mawaziri katika kasri, na mambo ya serikali yaliendeshwa na waziri Zhou Gong. Waziri huyo alikuwa mwaminifu, alituliza mara kadhaa uasi na alitumia makini sana kumlea mtoto huyo ili awe mfalme hodari.

Siku moja, mtoto huyo Zhou Chengwang alitumia jani moja la mti na kumwambia ndugu yake Shu Yu, "natumia jani hilo kukuteua uwe mtemi." Baada ya siku kadhaa Zhou Gong alisikia habari hiyo, alimwomba Zhou Chengwang achague siku kumteua ndugu yake Shu Yu. Lakini Zhou Chengwanga alisema, "Nilimtania tu." Kwa makini Zhou Gong alisema, "Mfalme haifai kufanya masihara. Maneno ya mfalme yote yataandikwa na yatatekelezwa kwa lazima." Tokea hapo Zhou Chengwang alikuwa mtu wa makini sana, na kweli baadaye alimteua mdogo wake Shu Yu kuwa mtemi wa sehemu ya Tangdi.

Sehemu ya Tangdi iko katika mkoa wa Shanxi. Baada ya Shu Yu kuwa mtu mzima aliendesha mambo vizuri, alistawisha kilimo na kuendeleza umwagiliaji, watu wa huko walikuwa na maisha mazuri. Baada ya Shu Yu kufariki, watu walimjengea bustani ili kumkumbuka. Bustani hiyo ndio bustani ya Jinci.

Mwaka wa kujenga bustani hiyo haubainiki, lakini maandishi ya kale yaliyohusu bustani hiyo yalikuwa ya Enzi ya Wei kaskazini (466-572), kwa hiyo bustani hiyo imekuwa na miaka zaidi ya elfu moja. Katika kipindi hicho cha zaidi ya miaka elfu moja, majengo ndani ya bustani hiyo yaliwahi kukarabatiwa mara kadhaa na kuongezwa. Mwaka 646 mfalme wa pili wa Enzi ya Tang Li Shimin aliiandikia bustani hiyo maelezo, na kuongeza majengo.

Ndani ya bustani hiyo kuna majengo yenye enzi tofauti, na pia kuna mti mmoja uliopandwa katika Enzi ya Sui (karne ya 11 K.K. hadi karne ya 8 K.K,), mti huo umekuwa na miaka karibu elfu mbili, mpaka sasa bado ni mzima majani yanastawi, mti huo pamoja na ziwa la maji ya chemchemi yamefanya mandhari ya bustani ijulikane na kuwavutia watalii wengi.


1 2 3 4 5 6 7