Hadithi za Methali za Kichina
"Mtenda Mabaya Hulipwa Mabaya"
Katika karne ya nane kabla ya kuzaliwa Kristo nchini China yalikuwako madola mengi yaliyokaa pamoja, mojawapo ilikuwa Dola ya Zheng. Malkia wa dola hiyo alijaliwa watoto wawili wa kiume: mkubwa aliitwa Wu Sheng, na mdogo Gong Shuduan. Kutokana na shida aliyoipata wakati wa uzazi wa kifunguamimba, malkia alimchukia Wu Shen na kumpendelea sana mwanawe mdogo, hata siku moja alimwomba mume wake mfalme akubali mwanawe huyo mdogo Gong Shuduan kuwa mrithi wa kiti cha ufalme. Mfalme alimkatalia kabisa. Baadaye mwanawe mkubwa Wu Sheng akatawazwa kuwa mfalme. Huyo ndiye mfalme "Zheng Zhuanggong" katika historia ya China.
Siku moja malkia alimtaka mfalme amgawie ndugu yake sehemu ya Jing, mfalme alikubali, na hivyo ndugu yake akahamia huko.
Kusikia habari hiyo mawaziri wakaenda kumshauri mfalme, "Sehemu ya Jing ni kubwa mno, huenda ikawa balaa kwa taifa. Kutokana na kanuni za mababu zetu, ukubwa wa mji mkubwa hauwezi kuzidi thuluthi moja ya mji mkuu, mji wa kiasi haufai kuzidi moja ya tano ya mji mkuu. Sasa eneo la Jing ni kubwa zaidi, hiyo hailingani na kanuni hata kidogo, baadaye utashindwa kuitawala." Mfalme akajibu, "Njia nyingine sina. Hivyo ndivyo mama malkia anavyotaka, niwezaje kuepukana na janga hili?" Kusikia hayo, mawaziri wakapendekeza, "Ni heri kumpa sehemu nyingine ambayo ni rahisi kumdhibiti asiweze kukuza nguvu zake. Pindi nguvu zake zikiwa kubwa itakuwa ni shida kwetu kupamana nazo. Hebu fikiri kwamba hata magugu kichakani hayawezi kufyekwa yote sembuse ndugu yako anayedekezwa na mama yako!" Mfalme akajibu, "Mtenda mabaya hulipwa mabaya, mtaona wenyewe."
Haukupita muda mrefu baada ya Gong Shuduan kuikalia shemu ya Jing akaanza kupanua zaidi na zaidi eneo lake la pembeni. Wakati huo mawaziri wakamwambia mfalme, "Dola moja haiwezi kumilikiwa na wawili kwa wakati mmoja, una ushauri gani sasa? Ikiwa utamwachia dola yetu, basi turuhusu tumhudumie yeye. La sivyo, tunaomba umwondoe kabisa huyu firauni ili isije ikawa ataungwa mkono na raia wa huko." Mfalme akawaambia kwa utulivu, "Msiwe na wasiwasi, atajipeleka kwenye maangamizi."
Kipindi kingine kikapita, Gong Shu alikuwa ameweka moja kwa moja sehemu ya Jing iliyopanuka chini ya himaya yake, utawala wa eneo lake ukawa maradufu kuliko hapo awali. Wakati huo mawaziri walishindwa kuvumilia, wakamwambia mfalme kinaga ubaga, "Ni wakati wa kumwondoa sasa, ama sivyo tutachelewa kabisa baada ya yeye kuungwa mkono na raia wa huko." Lakini mfalme pia aliwaambia kwa utulivu, "Ilivyokuwa mambo yake yanakwenda kinyume cha uadilifu, atawezaje kuungwa mkono na raia wa huko? Uchoyo wake wa ardhi utamuua."
Wakati huo Gong Shu alianza kushughulikia ujenzi wa kuta za mji, kuandikisha askari, akawa tayari kuushambulia mji mkuu. Alikula njama na mama yake ambayo atamwitikia kwa ndani kwamba atawafungulia askari wa mwanawe mdogo mlango wa mji mkuu. Habari hizo zilimfikia mfalme, akawaita mawaziri akawaambia kwa sauti thabiti, "Sasa wakati wetu umewadia." Akaamrisha askari wake kushambulia sehemu ya Jing. Raia wa huko ambao toka awali walikuwa na nongwa mara walimsaliti Gong Shu walipowaona askari wa mfalme wakija. Gong Shu alikuwa hana mbele wala nyuma akatorokea dola nyingine.
"Unyoya mmoja tu miongoni mwa manyoya ya ng'ombe tisa"
Kichina kinapoeleza kuwa jambo fulani ni dogo, au ni sehemu ndogo kiasi cha kupuuzwa kulingana na kitu kizima huwa kinasemwa "unyoya mmoja tu miongoni mwa manyoya ya ng'ombe tisa", kana kwamba ni tone moja tu la maji katika bahari. Msemo huu unahusu mwanahistoria maarufu wa China ya kale Sima Qian.
SiMa Qian alizaliwa katika ukoo wa mrasimu mdogo mwaka 145 kabla ya Kristo. Baba yake alikuwa ofisa wa mambo ya historia. Kwa kuathiriwa na baba yake, Sima Qian alishikwa na hamu na historia tangu utotoni, alikuwa amesoma vitabu vingi, na kuanzia miaka yake 20 alianza kuzungukazunguka kila mahali kuchunguza watu walioandikwa katika vitabu vya historia, jiografia, na matukio, ambapo alijipatia elimu nyingi, hatimaye akawa mfuasi wa mfalme.
Wakati huo vita kati ya Dola ya Xiong Nu na Dola ya Han ilianza. Mfalme wa Dola ya Han, Liu Che akamchagua jemadari Li Ling kwenda mstari wa mbele kupigana na Xiong Nu. Jemadari huyu akiwa na askari elfu tano alipigana vita kishupavu. Mwanzoni, habari njema za matokeo ya vita zilikuwa zikimjia mfalme kwa mfululizo ambapo mawaziri wengi walimpongeza kwa uchaguzi wake wa hekima. Lakini baadaye hali ilikwenda kombo, jemadari huyo na askari wake walivamiwa pande zote; ingawa walipigana kufa na kupona kwa siku nane mfululizo lakini mwishowe wakauawa karibu wote. Naye jemadari akasalimu amri kwa Xiong Nu.
Kusikia hayo mfalme akakasirika mno, mawaziri waliomsifu uhodari wake wa uchaguzi hapo awali, wote wakaanza kumshutumu jemadari isipokuwa Sima Qian ambaye alikuwa mtulivu. Mfalme akamsaili mawazo yake. Sima Qian akamwambia moja kwa moja, "Li Ling alikuwa na askari elfu tano tu na alivamiwa na maadui zaidi ya elfu 80. Japokuwa hivyo alipigana nao mpaka akaishiwa na chakula, mishale na njia ya kurejea pia ilifungwa. Kwa hiyo Li Ling hakuwa amesalimu amri bali alikuwa akivizia nafasi mwafaka kujitolea kwa taifa. Naona mchango wake ni mkubwa kuliko kosa lake la kushindwa."
Mfalme alipomsikia akimtetea akaghadhibika vibaya, akamtia gerezani papo hapo. Muda si muda baadaye fununu ikaja kwamba jemadari Li Ling amekuwa mwalimu wa askari wa Dola la Xiong Nu. Mfalme alihamaki mara moja, akamshikisha Sima Qian adabu kali ya kudhalilisha ya "kukatwa uume". Kwa kuteswa vibaya hivyo Sima Qian alitamani hata kujiua, lakini baadaye wazo jingine lilimjia, akifikiri kwamba kifo cha mtu mdogo kama yeye hakingeleta huruma yoyote, badala yake pengine kingekuwa kicheko na burudani ya mazungumzo ya watu wanaokunywa chai. Kutokana na wazo hilo akapania kuvumilia aibu yake na kuamua kufunga kibwebwe kuandika kitabu kikubwa cha historia. Tokea hapo alitopea katika kazi hiyo na mwishowe akamaliza kitabu chake kikubwa kijulikanacho kama "Rekodi za Kihistoria".
Sima Qian alidiriki kumwandikia barua rafiki yake mkubwa juu ya mawazo yake. Katika barua yake alifananisha kifo chake "ng'ombe tisa kupoteza unyoya mmoja tu". Kutokana na maneno haya watu wa baadaye wakapata msemo wa "unyoya mmoja tu miongoni mwa manyoya ya ng'ombe tisa".
Hadithi ya "Kutoboa Jani la Mti Kutoka Umbali wa Hatua Mia Moja"
Nchini China katika Enzi ya Madola ya Kivita yaani kutoka mwaka 475 mpaka 221 kabla ya Kristo yalikuwako madola mengi madogo madogo kwa pamoja, na kila dola ilikuwa na watu wake mashuhuri ambao wanasimuliwa miongoni mwa watu hadi leo. Ifuatayo ni hadithi ya "Kutoboa Jani la Mti Kutoka Umbali wa Hatua Mia Moja".
Bai Qi alikuwa hodari wa kupigana vita katika Dola ya Qin, kutokana na uhodari huo watu walimpachikia jina la "Jemadari Asiyeshindwa". Mwaka fulani alitumwa na mfalme aongoze askari wake kuivamia Dola ya Wei. Vita dhidi ya Wei ikishinda, madola mengi yatadhurika mfululizo. Kwa hiyo vita hivyo viliwatia watu wasiwasi.
Alikuwako mshauri mmoja, aliyeitwa Su Li. Aliagizwa kwenda kumshawishi jemadari aache nia yake ya kuivamia Dola ya Wei. Kwa juhudi nyingi, mshauri huyo alifanikiwa kuonana na jemadari, akamsimulia hadithi ifuatayo:
Zamani za kale alikuwako mpiga mshale aliyeitwa Yang Youji. Alipata uhodari wa kupiga shabaha toka utotoni mwake, kiasi kwamba aliweza kutoboa jani la mti kutoka umbali wa hatua mia moja. Wakati huo huo alikuwako mtu mwingine ambaye pia alikuwa hodari wa kupiga mishale aliyeitwa Pan Hu. Siku moja watu hao wawili walikutana kwa bahati, na kila mmoja alikuwa na hamu ya kumshinda mwingine, hatimaye walitaka kupimana uhodari wao. Watu waliposikia habari hii, wengi walikuja kushuhudia mashindano yenyewe.
Dango liliwekwa umbali wa hatua mia moja na shabaha yenyewe ilikuwa mchoro wa moyo kwenye ubao mmoja. Pan Hu alifyatua mishale mitatu mfululizo, na kila mmoja ulilenga katikati ya moyo, ambapo watazamaji walimshangilia kwa mshangao. Baadaye ilikuwa zamu ya Yang Youji, aliangaza macho sehemu zote kisha akasema, "Hatua mia moja si mbali, shabaha ya mchoro wa moyo ni kubwa. Nashauri, tushindane kwa jani la mti kutoka umbali wa zaidi ya hatua mia moja."
Akamwambia mtu mmoja apake jani moja rangi nyekundu, akafyatua mshale wake, jani lenye rangi nyekundu likatobolewa katikati.
Watazamaji wote walipigwa butwaa. Pang Hu alielewa fika kwamba uhodari kama huu hafui dafu, lakini pia hakuamini kuwa kweli Yang Youji angeweza kutoboa jani kila mara kwa umbali zaidi ya hatua mia? Kufikiri hivyo akaenda kwenye mti, akachagua majani matatu na kutia nambari kila moja kwa rangi. Alimwambia Yang Youji atoboe majani hayo matatu kwa mfululizo wa nambari.
Yang Youji alifika chini ya mti, akatambua kila jani kwa nambari yake, akarudi nyuma umbali wa hatua zaidi ya mia moja kutoka kwenye majani, akatia mshale kwenye upinde, akalifyatulia jani la kwanza, la pili na la tatu. Ah! mishale yote ilitoboa katikati ya majani kwa mfululizo wa nambari. Watazamaji wote walimshangilia kwa mayowe. Hapo ndipo Pang Hu aliridhika kabisa na uhodari wake.
Vifijo na vigelegele vilipozagaa uwanjani sauti ya mtu mmoja ilisikika kando ya Yang Youji, "Ehee, mtu hodari kama huyu ndiye anayestahili kufundishwa nami."
Kusikia aliyosema, Yang Youji alikasirika, akamgeukia na kumwuliza, "Utanifundisha namna gani?"
Kwa utulivu mtu huyo alimjibu, "Mimi sitakufundisha namna ya kupiga mishale, bali nakuelewesha namna ya kuhakikisha sifa yako inakuwa ya kudumu. Je, uliwahi kufikiri kwamba endapo ukiishiwa nguvu au ukikosea shabaha walau kidogo, sifa yako itaporomoka? Mpiga shabaha hodari mwenye akili lazima alinde sifa yake."
Mshauri Su Li baada ya kusimulia hadithi yake alimwambia Jemadari Bai Qi, "Wewe una sifa ya 'jemadari asiyeshindwa', lakini haitakuwa rahisi kuishinda Dola ya Wei, ikiwa huwezi kuishinda mara moja, si utajiharibia sifa yako mwenyewe?" Jemadari Bai Qi aliposikia hayo aliyosema, kwa kisingizio cha kuumwa akaacha mashambulizi yake dhidi ya Dola ya Wei.
Hadithi ya "Mbawala Kuitwa Farasi"
Hii ni hadithi ya Dola ya Qin ambayo ni dola ya kwanza kabisa ya jamii ya kimwinyi katika historia ya China.
Qin Shihuang, aliyekuwa mfalme wa kwanza wa Dola ya Qin, alikuwa na watoto wawili wa kiume, wa kwanza aliitwa Fu Su, ambaye alipelekwa kwenye sehemu ya mbali mpakani kusomeshwa baada ya kukomaa. Wa pili aliitwa Hu Hai, ambaye akiwa bado mdogo, mfalme alimpatia mwalimu myeka kumsomesha; mwalimu huyo aliitwa Zhao Gao.
Baada ya Dola ya Qin kufaulu kuunganisha China nzima ilistawi sana. Mfalme wa kwanza Qin Shihuang alikuwa na mazoea ya kutembeatembea kufanya ukaguzi huku na huko nchini akiwa na mawaziri wake huku akijisifu kwa mchango wake kwa kuchonga maneno yake kwenye mawe. Mwaka fulani aliugua akiwa safarini, na ugonjwa ukazidi mbaya, akaona siku zake zinahesabika, akamwagiza mwalimu myeka Zhao Gao kuandika wasia wa kumrithisha mwanawe wa kwanza Fu Su kiti cha ufalme. Siku chache baadaye mfalme wa kwanza Qin Shihuang akafariki dunia.
Lakini Zhao Gao alificha kabisa habari za kifo cha mfalme kwa maslahi yake mwenyewe. Aidha, kwa kugushi hati za mfalme aliandika wasia mwingine wa kumlazimisha Fu Su ajiue. Baadaye alirudi mji mkuu Xianyang na kumtawaza mfalme wa pili, Huhai ambaye alikuwa bado mdogo. Kwa kuwa mwalimu myeka wa mfalme wa pili, Zhao Gao alijiingiza kwenye kundi la kuamua mambo ya taifa bila ya matatizo.
Hata hivyo Zhao Gao hakuridhika, bali alizidi kumdhibiti mfalme mtoto, na alianza kutumia hila kuwaondoa wale wenye mawazo tofauti naye kisiasa. Alimwambia mfalme wa pili, "Utukufu wa mfalme unatokana mawaziri kutoruhusiwa kuonana naye kiholela. Wewe bado ni mdogo, kama maneno yako hayalingani na hadhi yako utachekwa na mawaziri, kwa hiyo ni busara kukaa ndani, na mambo yote niachie mimi, hivyo mawaziri hawataweza kukukanganya kwa makusudi." Mfalme Hu Hai alikubali pendekezo lake, alijifungia ndani na ilikuwa nadra kuonana na mawaziri. Kwa kuwa alimdhibiti vilivyo mfalme wa pili, maofisa wote ndani ya kasri walimwogopa sana.
Lakini Zhao Gao aliendelea kuwa na wasiwasi hata mwishowe akaamua kutumia ujanja wa kupima utiifu wa kila mmoja ili awaondoe wale waliotofautiana naye kimawazo. Siku moja alimwagiza mtiifu wake mmoja alete mbawala na kusema mbele ya mfalme, "Nimekuletea farasi huyu kama zawadi." Mfalme Hu Hai alidhani anamtania, akasema kwa tabasamu, "A,a, umekosea, mbona unamwita mbawala, farasi?" Lakini Zhao Gau alimjibu, "Kweli huyu ni farasi, ukiwa na wasiwasi, waulize mawaziri hawa." Mfalme alipoona jinsi alivyomwambia kwa makini akashikwa na wahka. Akauliza mawaziri kadhaa. Baadhi yao walivungavunga bila ya kusema mbawala wala farasi, na baadhi yao walisema wazi kwamba ni farasi hasa. Alipoona hali hiyo mfalme akazidi kubabaika, akiwaza, jambo dogo na rahisi kama hili laleta mawazo tofauti miongoni mwa mawaziri, hii pengine inaashiria janga la taifa. Kisha mfalme alimwita ofisa wa sadaka, naye akamwambia mfalme kwamba hali hii imesababishwa na mfalme kutomwabudu sana mungu, akamshauri mfalme aondoke kwenye kasri akafunge saumu kwa muda katika sehemu tulivu. Mfalme akahamia bustani moja nje ya kasri, kwa kisingizio cha kufunga akajiburudisha kwa uwindaji huko.
Sasa, turudi kwa Zhao Gao. Baada ya mfalme wa pili kuondoka kwenye kasri Zhao Gao akawa mjeuri wa kufanya mambo atakavyo. Aliwafunga gerezani au kuwaua kisirisiri wale waliosema ukweli katika jaribio la "mbawala kuitwa farasi".
Tokea hapo kasri ikawa kimya, hapakuwa na mpinzani wake hata moja. Hata hivyo hakuacha uchoyo wake, kwa sababu lengo lake ni kuwa mfalme halisi.
Muda si muda msukosuko ukatokea kote nchini, kwa kutumia fursa hii Zhao Gao alituma watu waliojifanya mahaini wavamie makazi ya mfalme na kumlazimisha ajiue. Baada ya yote hayo Zhao Gao alivumisha habari kwamba mfalme aliuwawa na mahaini, na dola haiwezi kukaa bila mfalme, kwa kuwa mfalme wa pili hana mtoto, yeye atakuwa mfalme. Mawaziri walikasirika mno, hakuna hata mmoja aliyemkubalia.
Baba mdogo wa mfalme wa pili alikuwa na nongwa toka zamani. Baada ya kupata habari kwamba kweli mpwa wake, mfalme wa pili, amekufa, alimwua Zhao Gao kwa njama, na yeye mwenyewe akawa mfalme wa tatu wa Dola ya Qin. Lakini jambo la kusikitisha ni kwamba baada ya siku 45 tu Dola ya Qin ikaangamizwa katika maasi ya wakulima. Ingawa Dola ya Qin iliangamizwa lakini hadithi ya msemo "Mbawala Kuitwa Farasi" ikawa simulizi, ikilenga wale watu wanaopindua ukweli na uwongo na kuwa na nia ya kufanya mambo mabaya.
Chang E Arukia Mwezini
Tarehe 15 mwezi Agosti kwa kalenda ya Kichina ni sikukuu ya mwezi. Sikukuu hiyo ni mila ya Wachina yenye historia ndefu. Katika siku hiyo jamaa wa familia moja hujikusanya pamoja kula keki za mwezi na kuburudika na mwezi mpevu. Sikukuu hiyo ilitokana na hadithi ya "Chang E Arukia Mwezini".
Chang E alikuwa mungu wa mwezi, mume wake Houyi alikuwa hodari wa kupiga mishale. Mwaka mmoja duniani ulitokea msiba mkubwa duniani, wanyama wakali walitoka majini na misituni kuwashambulia binadamu. Mungu mkuu alipofahamu hali hiyo alimtuma Houyi ashuke duniani akiwa na mkewe Chang E. Aliwaua wanyama wakali lakini wakati huo mbinguni kulitokea majua kumi, joto kali lilikausha mimea yote, mito ilikauka, misitu iliwaka moto na watu wengi walikufa.
Houyi alishawishi majua kumi yatokee moja moja kwa zamu, lakini yalikuwa hayasikii. Kwa kukasirika, Houyi alitungua majua tisa na kubakiza moja mbinguni.
Kutokana na wivu Houyi alisingiziwa na miungu mingine mbele ya mungu mkuu, basi mungu mkuu alimwadhibu Houyi abaki duniani pamoja na mkewe. Lakini mke wa Houyi alishindwa kuishi maisha magumu duniani.
Houyi alisikia kwamba kuna dawa ya ajabu kwenye mlima wa Kunlun, mtu akila dawa hiyo ataweza kuruka mbinguni. Houyi alisafiri mbali kwa shida, na mwishowe aliipata dawa hiyo. Lakini dawa hiyo inaweza kutumiwa na mtu mmoja tu, kutokana na kutotaka kuachana na mke wake Chang E, Houyi alificha dawa hiyo.
Katika tarehe 15 Agosti Chang E alitumia fursa ya mume wake kutokuwepo nyumbani alikula dawa hiyo na mara akapaa mbinguni hadi mwezini.
Houyi aliishi duniani kwa kuwinda, aliwapokea wanafunzi kadhaa kuwafundisha upigaji mishale. Kati ya wanafunzi hao alikuwako mmoja aliyeitwa Peng Meng, alipata maendeleo makubwa katika upigaji mishale. Mwanafunzi alifikiri kuwa kama Houyi akiwa hai basi yeye daima atakuwa wa pili katika upigaji mishale, basi alitumia fursa ya Houyi kulewa alimwua Houyi.
Chang E aliishi peke yake mwezini ila tu sungura mmoja mweupe na mti mmoja mkubwa, alimkumbuka mumewe hasa katika siku ya tarehe 15 mwezi Agosti.
"Utendaji wa Busara"
Kuanzia karne ya tano mpaka karne ya tatu kabla ya kuzaliwa Kristo ilikuwa enzi ya "Madola ya Kivita" katika historia ya China. Nyakati hizo yalikuwako madola mengi na yalikuwa mara kwa mara yakipigana vita kwa ajili ya kunyang'anyana ardhi. Vita vya muda mrefu viliwatokeza majemadari hodari na mahiri wengi wa mambo ya kijeshi, Sun Bin ni mmojawapo aliyejitokeza zaidi katika historia ya China. Haya, katika kipindi hiki nitawaelezeeni jinsi Sun Bin alivyotumia mbinu zake kuwashinda maadui.
Kabla ya kupata umaarufu, Sun Bin alikuwa na Pang Juan kusomea pamoja mbinu za kivita. Kisha baadaye Pang Juan akawa jemadari wa Dola ya Wei, lakini alitambua fika akilini kwamba umahiri wake haungefua dafu mbele ya Sun Bin. Kwa hiyo, aliwaza kwamba iwapo Sun Bin angekuja kwenye Dola ya Wei nafasi yake ya ujemadari hakika ingekuwa hatarini. Hivyo alimghilibu Sun Bin aje kwake. Baada ya Sun Bin kufika kwake, kwa hila alimkata miguu yake na akamtupa ndani ya zizi la nguruwe.
Kutokana na Sun Bin kujifanya mwendawazimu aliachiwa na mlinzi ambapo aliweza kuonana na mwakilishi wa Dola ya Qi kwa siri. Mwakilishi wa Qi alifurahia sana umahiri wake, akamsaidia kutorokea Dola ya Qi.
Mara baada ya Sun Bin kufika katika Dola ya Qi akapata heshima ya mfalme na kupewa cheo kikubwa.
Siku moja mfalme wa Dola ya Wei alimtuma Pang Juan na askari wake kushambulia Dola ya Han. Dola ya Han ikaiomba Dola ya Qi msaada. Mfalme wa Qi akawateua Tian Ji awe jemadari na Sun Bin awe mshauri wa kijeshi wakiambatana na askari kuisaidia Dola ya Han. Kwa ushauri wa Sun Bin askari wa Qi hawakuenda kwenye Dola ya Han iliyoomba msaada, badala yake walikwenda moja kwa moja katika Dola ya Wei kuushambulia mji mkuu wake Da Liang. Ili kuiokoa dola yake, Pang Juan aliacha mashambulizi yake dhidi ya Dola ya Han na kurejea haraka.
Sun Bin alipotambua kwamba Pang Juan amekwisharubuniwa, akamwambia jemadari wake, "Askari wa Dola ya Wei ni hodari zaidi, wanadharau askari wetu wakidhani wote wanaogopa vita, kwa hiyo watu hodari wa kupambana vita wanapaswa kutenda mambo kwa busara. Sasa basi, tujifanye kuogopa vita, turudi nyuma na kupunguza vishimo vya kuinjika sufuria kila siku, tuwaache maadui wakosee kuelewa ukweli ulivyo." Kufuatana na mawazo yake, jemadari Tian Ji aliwaamrisha askari wake wachimbe vishimo laki moja vya kupikia kwa siku ya kwanza, elfu 50 kwa siku ya pili na elfu 30 kwa siku ya tatu.
Baada ya kugundua kwamba askari wa Qi wamerudi nyuma, Pang Juan akaamrisha mara moja askari wake wawafukuze moja kwa moja akitaka kuwaangamiza kwa pigo moja. Kila alipofika mahali askari wa Qi walipopiga mahema siku iliyotangulia Pang Juan huwaamrisha askari wake kuhesabu vishimo, na kugundua vishimo vikipungua siku hadi siku; hivyo alifurahi mno akidhani askari wa Qi wametoroka kwa kuhofia ukali wa askari wake, na sasa waliobaki ni wachache tu. Ili kumuua Sun Bin, Pang Juan alipiga mbio na askari wake wa farasi kwa kufuata alama alizoacha Sun Bin.
Wakati huo Sun Bin na askari wake walikuwa wamefika sehemu nzuri ya vita iitwayo Ma Ling, Sun Bin alionyesha kidole kuonyesha mti mmoja mkubwa na kuwaambia askari wake waondoe magome yote, na kuchonga maneno juu yake, "Pang Juan atakufa chini ya mti huu!", kisha akawaamrisha tena askari hodari wa kupiga mishale wajifiche vichakani, na kuwaambia kwamba wapige mishale pale watakapoona moto.
Pang Juan alipofika Ma Ling usiku ulikuwa umeingia. Askari wake walikuwa hoi baada ya mwendo wa mchana kutwa, baada ya kushuka kwenye farasi mara wakajitafutia miti ya kuiegemea kwa ajili ya usingizi. Wakati huo mtu mmoja alipapasa ule mti wenye maneno, akapiga kelele. Pang Juan aliwaita askari walete mienge kumulika maneno, alipoyatambua tu yale maneno papo hapo mishale kemkem ikafyatuliwa huko. Askari wa Wei wakasambaratika na kutoroka ovyo. Hapo ndipo Pang Juan alipofahamu ameingia mtegoni. Lakini kwa kuzingirwa barabara na askari wa Qi, Pang Juan akawa hana njia, akajiua pale pale kwenye mti.
Hiki ndicho kisa maarufu "Mapambano ya Kiakili ya Sun Bin" katika historia ya China, msemo wa "Utendaji wa Busara" inatokana na kisa hicho.
Pu Songling na kitabu chake cha "Hadithi za Mashetani"
Mwanzoni mwa karne ya 18, kitabu maarufu cha hadithi fupi fupi yaani "Hadithi za Mashetani" kiliibuka nchini China, Pu Songling kwa ustadi wake aliandika hadithi nyingi za mashetani na bweha.
Pu Songling alizaliwa mwaka 1640 na kufa mwaka 1715, alikuwa mwanafasihi katika Enzi ya Kifalme ya Qing. Alizaliwa katika ukoo wa wafanya biashara, lakini alifanya kazi ya ualimu. Katika maisha yake aliandika makala mengi na kitabu chake cha mkusanyiko wa hadithi fupi yaani "Hadithi za Mashetani" ndicho kilichompatia umaarufu.
Kitabu cha "Hadithi za Mashetani" kimekusanya hadithi 430, ambapo miongoni mwa hadithi hizo iliyo fupi kabisa ina maneno mia mbili au tatu hivi, na ile ndefu sana ina maelfu kadhaa ya maneno. Kitabu kizima kinaeleza hadithi za mashetani na bweha kikilaani pingu za maadili ya kimwinyi, ubovu wa mitihani ya kifalme ya kuchagua maofisa na kudai uhuru wa maisha ya binadamu. Katika kitabu hiki hadithi za kupendeza sana ni zile za mapenzi kati ya mashetani na bweha ambazo zilionyesha matumaini ya binadamu kuvunja pingu za maadili ya kimwinyi kati ya wanaume na wanawake.
Katika kitabu cha "Hadithi za Mashetani" bweha hujitokeza kama kisura. Miongoni mwa hadithi hizo, maarufu zaidi ni "Hadithi ya Xiao Cui". Kwa kifupi hadithi hiyo inaeleza kama ifuatayo:
Alikuwako afisa mmoja aliyejulikana kama Wang Taichang, ambapo mtoto wake wa kiume Yuan Feng alikuwa punguani, na hapana hata msichana mmoja aliyekubali kuolewa naye, hali ambayo iliwasikitisha sana wazazi wake. Siku moja kwa ghafla walikuja nyumbani kwao mama mzee mmoja na binti yake. Mama mzee alisema kwamba kwa sababu ya umaskini anakubali kumwoza binti yake Xiao Cui kwa Yuan Feng. Kisha mama mzee huyo kwa kisingizio akaondoka nyumbani kwao na hakuonekana tena. Xiao Cui alikuwa msichana mwerevu, kila siku alicheza cheza na Yuan Feng bila kumchukia kutokana na utaahira wake. Wazazi wa Yuan Feng walimpenda sana mkamwana wao.
Alikuwako afisa mwingine, aliyejulikana kama Wang Jijian, ambapo alitaka kumtia hatiani Wang Taichang kwa kumsingizia, lakini Xiao Cui aligundua hila hiyo mapema. Alijipamba kama afisa mkubwa na kwa vishindo alimtembelea Wang Taichang, hivyo Wang Jijian aliona kwamba kumbe Wang Taichang ana tegemeo la afisa mkubwa, na ndipo akaacha hila yake ya kumsingizia. Familia ya Wang Taichang ikaepuka janga hilo.
Siku moja Xiao Cui alioga, kwa makusudi alimtosa mumewe Yuan Feng ndani ya maji ya moto. Wakwe zake walikasirika sana, lakini Xiao Cui hakutilia maanani akisema, Yuan Feng alikuwa punguani, afadhali afe kuliko kuishi. Maneno hayo yaliwakasirisha zaidi wakwe zake kiasi cha kutaka kumfukuza nyumbani, lakini wakati huo mtoto wao Yuan Feng alipona na kuwa mtu wa kawaida kabisa.
Baada ya miaka miwili kupita, mzee Wang Taichang alitaka kumhonga mtu fulani kwa jagi moja la thamani lakini kwa bahati mbaya Xiao Cui alilivunja, wazazi wakamshutumu na kumtukana Xiao Cui bila kujali wema aliowatendea. Kutokana na hilo Xiao Cui alijiua kwa kujitumbukiza kisimani.
Hadithi hiyo iliandikwa kwa vituko vingi vya kuwavutia wasomaji, ambapo mwandishi alimsawiri kwa ustadi msichana mmoja mwenye akili, roho nzuri na wa kupendeza. Mwishoni mwa hadithi hiyo mwandishi alibainisha kwamba Xiao Cui alikuwa bweha mdogo, kwa sababu mama yake aliwahi kukimbia janga nyumbani kwa wale wazee, akajigeuza kuwa binadamu ili kuwalipa wema wao.
Katika kitabu cha "Hadithi za Mashetani", pia wako bweha wenye sura mbaya lakini roho nzuri. Hadithi ya "Bweha Mwenye Sura Mbaya" ilieleza jinsi bweha mmoja mwenye sura ya kuchukiza alivyomkuta msomi mmoja, ambaye alikuwa maskini hahehohe hata chakula kilikuwa ni shida kwake achilia mbali nguo. Bweha huyo alimsaidia maisha yake. Lakini baada ya msomi huyo kupata nguo safi, nyumba za fahari na kila kitu kwa maisha ya starehe alimwomba mchawi amfukuze bweha. Bweha alihamaki sana kutokana na msomi huyo kukosa shukrani, ndipo licha ya kurudisha yote aliyompa msomi, alimtuma shetani kumwadhibu vibaya. Kwa masimulizi ya hadithi hii mwandishi anawaonya watu wenye roho mbaya.
Katika kitabu cha "Hadithi ya Mashetani" mwandishi Pu Songling pia alitunga hadithi ya bweha kisura lakini mwenye roho katili. Hadithi ya "Kuchora Ngozi ya Mrembo" ilieleza kuwa bweha mmoja alijifunika kwa ngozi yenye sura nzuri akiishi kwa kufyonza damu za binadamu, bweha huyo mwishowe aliuawa na binadamu. Hadithi nyingine ya "Bweha Aingiaye ndani ya Jagi" ilieleza jinsi bweha mmoja mara kwa mara alivyofanya uhalifu nyumbani kwa watu, na baada ya kugunduliwa akajigeuza kuwa moshi na kujipenyeza ndani ya jagi la maua, mwenye nyumba mwerevu mara akaziba mdomo wa jagi akamwua bweha ndani.
Kwa kifupi, Pu Songling aliwaelezea wasichana wengi kwa sura ya bweha, na wasichana hao walikuwa na maadili mengi mazuri ambayo binadamu hawakuwa nayo.
"Hadithi ya Mashetani" ni maandishi makubwa katika historia ya fasihi ya Kichina, maandishi hayo pamoja na maandishi mengine yaliyoandikwa katika enzi moja yaani "Ndoto kwenye Jumba Jekundu" yaliipeleka kileleni historia ya riwaya za Kichina. Katika muda wa miaka mia mbili iliyopita kitabu hicho kimetafsiriwa kwa lugha za kigeni zaidi ya kumi na kusambazwa kote duniani. Aidha, hadithi nyingi kwenye kitabu hicho zimetengenezwa kuwa michezo ya sinema na televisheni inayowafurahisha sana watazamaji.
Hanxin Aibishwa kwa Kupita Kati ya Miguu
Karne ya pili K.K. ilikuwa ni Enzi ya Qin, katika enzi hiyo Ukuta Mkuu ulikuwa umeanza kujengwa. Lakini kutokana na utawala wa kikatili, enzi hiyo ilidumu kwa miaka 15 tu. mwishoni mwa enzi hiyo wakulima walifanya uasi huko na huku, wakati huo walitokea mashujaa wengi, Hanxin alikuwa mmoja kati ya mashujaa hao.
Hanxin alikuwa jemadari mkubwa, alizaliwa katika ukoo maskini, na alifiwa na wazazi wake tokea alipokuwa mtoto. Kabla ya kuwa jemadari, Hanxi alikuwa hafahamu kufanya biashara na kulima, aliishi katika hali ya umaskini kabisa na mara kwa mara alikosa chakula.
Ili aweze kuishi, ilimpasa kuvua samaki kwa mshipi kwenye mto Huaishui uliokuwa karibu na nyumbani kwake. Kulikuwa na dobi mmoja mzee, kwa kumhurumia, mara kwa mara alimpa chakula. Hanxin alisisimka sana na kumwambia mzee dobi, "Nitalipa wema wako." Mzee dobi aliposikia hayo alikasirika na kusema, "Wewe ni mwanamume hata unashindwa kujipatia riziki. Nakupa chakula kwa kukuhurumia tu sitaki ulipe wema wangu." Hanxin alijionea masikitiko, huku aliamua kuwa ni lazima afanye kitu.
Wenyeji walimdharau Hanxin. Siku moja kijana mmoja alitaka kumdhalilisha, alimwambia Hanxin, "Ukiwa jasiri niue kwa upanga wako, ama sivyo pita kati ya miguu yangu." Watu wengi walikuja kutaka kuona Hanxin atakuwaje. Hanxin baada ya kufikiri alipita kati ya miguu ya huyo kijana. Watu walioshuhudia walicheka, wakiona kuwa Hanxin ni mhofu. Hii ndio "hadithi ya kumwaibisha Hanxin kwa kupita kati ya miguu".
Hanxin alikuwa mtu mwenye mtazamo wa mbali. Alipoona kuwa jamii inapokuwa katika kipindi cha kubadilisha enzi, alijitahidi kujifunza uhodari wa kupigana vita, aliamini kuwa ataibuka katika jamii. Mwaka 209 wakulima walifanya uasi kila mahali dhidi ya utawala wa Enzi ya Qin. Hanxin alijiunga na jeshi moja, lakini hakuthaminiwa kama alivyotaka. Hatimaye alimfahamu mshauri Xiao He wa Liu Bang, wao mara kwa mara walijadiliana mambo ya kijeshi, Xiao He aliona kuwa Hanxin ni mtu hodari, kwa hiyo alijitahidi kumpendekeza Hanxin kwa Liu Bang. Lakini Liu Bang hakumthamini sana.
Siku moja Han Xin aliondoka kutoka jeshini na kukimbilia kwenyue jeshi jingine. Baada ya kusikia habari hiyo Xiao He alimkimbilia kwa farasi. Liu Bang alidhani hao wawili walitoroka. Lakini baada ya siku mbili walirudi kwa Liu Bang. Xiao He alimwambia, "Nilimkimbilia Han Xin." Liu Bang alibabaika na kusema, "Zamani majemadari wangapi walitoroka, mbona Han Xin tu ulimkimbilia na kumrudisha?" Xiao He alisema, "Waliotoroka wote walikuwa wa kawaida, lakini Han Xin sivyo, ni mtu asiyepatikana kwa urahisi, ukitaka kupata nchi Han Xin ni mtu wa lazima." Liu Bang alisema, "Kama ni hivyo, basi mbakize na awe jemadari mkuu." Tokea hapo Han Xin alipomsaidia Liu Bang kuipata nchi nzima alipata ushindi mkubwa katika vita.
Bwana Dong Guo na Mbwa-mwitu wa Zhong Shan
Hadithi ya "Mvuvi na Shetani" kutoka "Elfu lela u lela" inajulikana kote duniani. Lakini pia iko hadithi nyingine ambayo inafanana na hadithi hii inasimuliwa sana duniani. Hii ni hadithi iitwayo "Bwana Dong Guo na Mbwa-mwitu wa Zhong Shan".
Hadithi hiyo inatokana na kitabu kilichotungwa na Ma Zhongxi katika Enzi ya Ming, karne ya 13. Hadithi yenyewe ni kama ifuatayo:
Hapo kale alikuwako msomi mmoja Dong Guo, huyu bwana macho yake yalikuwa hayabanduki kwenye vitabu vyake kila siku na kila wakati. Hivyo akawa mbukuzi na elimu yake ilikuwa ya kitabuni tu. Siku moja akiwa na mfuko wake wa vitabu mgongoni alitoka na punda wake akienda mahali paitwapo Zhong Shan kutafuta nafasi ya udiwani.
Ghafla mbwa-mwitu mmoja aliyejeruhiwa alitokea mbele yake na kumsihi, "Ewe bwana, nafukuzwa na mwindaji, nilipigwa mshale, karibu nife. Naomba unifiche ndani ya mfuko wako. Nakuahidi nitakulipa kwa wema wako."
Bwana Dong Guo alijua mbwa-mwitu ni madhara kwa binadamu, lakini kuona alivyokuwa maskini, alimhurumia, alisita kidogo, lakini akamwambia, "Nikifanya kama usemavyo nitamkosea mwindaji, lakini basi nitakuokoa." Kisha akamwambia mbwa-mwitu ajikunyate, akamfunga miguu yake na kumwingiza kwenye mfuko.
Punde si punde mwindaji alikuja akaona mbwa-mwitu katoweka. Alimwuliza Bwana Dong Guo: "Je umemwona mbwa-mwitu kupita hapa? Amekimbilia wapi?"
Bwana Dong Guo alimjibu, "Hataa, sikumwona. Hapa njia panda ni nyingi, pengine amechukua njia nyingine." Mwindaji akamwamini, akafuata njia nyingine kuendelea kusaka.
Kusikia vishindo vya mwindaji na farasi wake vimekwenda mbali, mbwa-mwitu alimsihi Bwana Dongo Guo mfukoni "Naomba uniachie huru nikimbize roho haraka!"
Mwenye rehema Dong Guo alidanganywa na maneno ya mbwa mwitu, akamtoa mfukoni. Lakini ghafla, huyo mbwa-mwitu akamgeukia na kusema kwa kelele, "Sasa nabanwa na njaa, ilivyokuwa umenifanyia wema, basi unifanyie zaidi, nikumalize." Papo hapo akamrukia. Bwana Dong Guo alikukurushana naye, huku akiguta, "Usiye na fadhila we!"
Wakati huo, mkulima mmoja alipita hapo alikuwa na jembe mkononi. Bwana Dong Guo alimsimamisha na kumweleza kisa chenyewe, lakini mbwa-mwitu alikana kwamba aliokolewa naye. Baada ya kutafakari, mkulima akasema: "Hata mimi siamini wewe bwana ungeweza kumficha ndani ya mfuko wako mdogo kama huu, au umfiche tena nione." Mbwa-mwitu kakubali, akalala chini akajikunyata mviringo akimwachia Dong Guo amfunge miguu yake kwa kamba na kumwingiza mfukoni. Kwa haraka mkulima akafunga kabisa mfuko huku akimwambia Bwana Dong Guo, "Unadhani mnyama kama huyu angeweza kubadili tabia yake asimdhuru binadamu? Asilan! Ni ujinga kuwa na huruma kwa mbwa-mwitu!" Kisha akainua jembe lake akamwua kabisa mbwa-mwitu. Bwana Dong Guo akaerevuka na kumshukuru sana kwa kumwokoa.
"Bwana Dong Guo na Mbwa-mwitu wa Zhong Shan" imekuwa hadithi ya mafunzo: "Bwana Dong Guo" anawakilisha watu wababaishaji wa jema na baya na kutumia ovyo huruma; "mbwa-mwitu wa Zhong Shan" anawakilisha watu wasio na shukrani.
Hadithi ya "Kugawa Uji na Achali"
Fan Zhongyan alikuwa mwanasiasa na mwanafasihi mkubwa katika historia ya China, michango yake mikubwa haikuwa katika fasihi tu bali pia katika mambo ya kijeshi. Makala yake inayojulikana kama "Kumbukumbu katika matembezi ya banda la Yue Yang Lou" ni maarufu sana katika fasihi ya kale ya Kichina. Vifungu ndani ya makala hiyo "Kiongozi anapaswa awe na wasiwasi kabla ya wananchi, na afurahie matunda nyuma ya wananchi" vinasifiwa na watu kizazi hadi kizazi. Katika kipindi hiki nitawasimulieni jinsi alivyojitahidi kusoma utotoni mwake.
"Fan Zhongyan alikuwa mtu wa Enzi ya Song ya karne ya kumi. Kabla hata hajatimiza umri wa miaka mitatu alifiwa na baba yake, maisha yalikuwa ya kusikitisha sana. Alipofikisha umri wa miaka 10 aliondoka nyumbani kwenda kutafuta elimu na mwishowe alipata mwalimu katika Chuo cha Ying Tian Fu. Alipokuwa chuoni maisha yake yalikuwa ya ufukara kama maji, kwa kuwa hakuwa na fedha za kununulia chakula na kwa muda mrefu alilazimika kunywa uji tu. Kila siku asubuhi alichemsha uji na baada ya uji kupoa na kuwa mgando akaugawa pamoja na achali sehemu tatu ili asitumie zaidi sehemu moja kwa wakati mmoja.
Siku moja Fan Zhongyan alipokuwa akila, rafiki yake alikuja kumtembelea, akagundua chakula chake kilikuwa hafifu na cha kusikitisha, kwa huruma akampa fedha za kumsaidia apate chakula bora, lakini Fan Zhongyan alikataa kwa kumshukuru sana. Rafiki yake alishindwa kumshawishi, basi siku ya pili akamletea chakula kizuri cha kufisha ubuge. Fan Zhongyan alilazimika kukipokea.
Siku kadhaa zilipita, rafiki yake huyo alikuja tena kumtembelea, akagundua kwamba chakula alichomnunulia hakikuguswa hata kidigo, akakasirika na kusema, "Wewe unajiheshimu kupita kiasi, hata unakataa chochote cha wengine."
Fan Zhongyan alitabasamu na kusema, "Ndugu, umenielewa vibaya. Sio mimi nakataa chakula kitamu, bali sithubutu kukitumia. Kwani nikila chakula kinono kama hiki cha nyama na samaki, nitashindwa kumeza uji na achali baadaye. Wema wako naupokea, halahala usinihamakie." Kusikia hayo rafiki yake akamheshimu zaidi.
Fan Zhongyan aliwahi kuulizwa na wengine malengo yake katika maisha yake. Alijibu, "Malengo yangu ni kuwa daktari hodari au waziri mkuu mwema, kwani daktari anawaokoa wagonjwa, na waziri mkuu anaiendesha dola." Na kweli baadaye alikuwa waziri mkuu akawa mwanasiasa mashuhuri katika historia ya China.
Fan Zhongyan, kwa upande mmoja alistawisha elimu na kwa upande mwingine alifanya mageuzi ya idara za serikali iliyokuwa ya umangi meza. Alijenga shule nyingi kote nchini na kuongeza walimu ili kuwalea watu hodari wanaohitajika sana katika ujenzi wa taifa. Na yeye mwenyewe aliwathamini kwa vitendo watu wenye umahiri wa fani mbalimbali, mwanasiasa Ou Yangxiu, mwanafasihi Zhou Dunyi na mwanafasafa Zhang Zai n.k, wote walipata kusaidiwa naye.
Fan Zhongyan mbali ya kushughulika na mambo yake ya taifa naye pia alijinyima wakati kuandika maandishi mengi mazuri. Ni stahili yake kusifiwa kwamba yeye alipinga tungo za kuchezea maneno tu bila maudhui. Alitetea fasihi ifungamane na hali ilivyo ya jamii ili kupeleka mbele jamii na maendeleo ya binadamu. Utetezi huu ulikuwa umeathiri sana maendeleo ya fasihi ya baadaye.
Kuacha kalamu na kushika silaha
Katika karne ya kwanza, China ilipokuwa katika Enzi ya Han alikuweko msomi mmoja mashuhuri, anaitwa Ban Chao. Kwa ajili ya kulinda mipaka ya nchi aliacha kalamu na kushika silaha, na akawa bingwa wa kivita na mwanadiplomasia.
Mwaka 32 Ban Chao alizaliwa katika ukoo wa maofisa wa kuandikia historia, baba yake mdogo na ndugu yake mdogo wa kike wote walikuwa watu mashuhuri wa kuandikia historia katika historia ya China. Baba yake Ban Biao aliendelea kuandika mfululizo wa kitabu cha "Rikodi za Historia", kaka yake Ban Gu alihariri na kuandika kitabu cha Historia ya Han na ndugu yake mdogo wa kike aliendelea kuandika kitabu hicho baada ya kaka yake kufariki. Ban Chao alisoma vitabu vingi toka utotoni mwake. Alikuwa mtu mwenye akili nyepesi, ujasiri mkubwa na uhodari wa kuongea kiada.
kwa sababu ya umasikini wa ukoo wake, ilimpasa Ban Chao kunukulu nyaraka serikalini ili kupata kijungu jiko. Lakini Ban Chao alikuwa mtu mwenye matumaini makubwa, haridhiki na kazi yake hiyo iliyokuwa ikirudia rudia kila siku.Wakati huo dola yake Han ilikuwa imepata tu utulivu baada machafuko ya muda mrefu wa vita, nguvu za taifa zilikuwa bado dhaifu, mpaka wa kaskazini mara kwa mara ulishambuliwa na dola ya Xiong Nu. Siku moja mkono wake ulimkaza kwa ajili ya kuandika sana, akifikiri kuwa kazi kama hii ina maana gani kwa taifa linalosumbuliwa mpakani! Akaitupilia mbali kalamu yake huku akipiga kite na kusema, "Mimi dume halisi laizima nitoe michango mpakani, bali sio kuishi na kalamu kila siku!" Basi akaacha kazi yake ya ukatibu akajiandikisha kujiunga na jeshi.
Baada ya kujiunga na jeshi, Ban Chao alipigana na vita kwa ushupavu na ujanja, akapata sifa nyingi nzuri. Werevu na ushupavu wake vilimvutia mfalme, hivyo akatumwa kwenye sehemu ya magharibi ya China, yaani mkoa wa Xin Jiang wa leo ili kuweka uhusiano mzuri na madola mengine ya huko.
Ban Chao aliondoka na wafuasi wake 36. Kwanza alifika Dola ya Shan Shan. Mwanzoni mfalme alimhehimu na kumkaribisha kwa ukarimu. Lakini baada ya siku kadha kupita mfalme akawa baridi. Kuona jinsi mfalme alivyo akawaambia wafuasi wake, "Mabadiliko ya msimamo wa mfalme panengine yatokana na kuja kwa wajumbe wa Xiong Nu ambao wanajaribu kuharibu uhusiano wetu na mfalme, nendeni mkafanye uchunguzi." Baada ya kufanya upelelezi akaambiwa kwamba hali ilivyo ndivyo alivyokadiria. Basi Ban Chao aliwakusanya wafuasi wake pamoja akasema: "Tuko mbali na nchi yetu, na tumekuwa hatarini sasa, maana ikiwa mfalme wa Shan Shan akifuata ushawishi wa Xiong Nu sote tutauawa. Niambieni basi tufanyeje sasa?" Mara wafuasi wakamjibu, "Tutakusikiliza tu kufa au kupona." Ban Chao akawaambia kwa uthabiti, "Hatuna njia nyingine ila tu kuwafyeka kabisa maadui wetu pangoni!"
Usiku huo huo aliwaongoza wafuasi wake kujificha nje ya mahema ya wajumbe wa Xion Nu. Kwa kusaidiwa na upepo waliwasha moto, na moto ukawaka ripuripu. Maadui walibumburuka na kukhangaika ovyo, kwa kutumia fursa hii wakatoma mahemani wakawaua wajumbe wote wa Xio Nu. Siku ya pili, Ban Chao alipomwona mfalme alifichua njama za Xion Nu na kumfariji vema mfalme. Mfalme akakata shauri kuweka uhusiano na Dola ya Han.
Kisha baadaye akiwa na wafuasi wake 36, Ban Chao alifika Dola ya Shu Le. Mfalme wa Dola ya Shu Le alikuwa ni mfalme wa kupandikizwa tu kutoka nje, kwa hivyo wananchi walikuwa wakimchukia, Ban Chao aliwasaidia kumwondoa na akamsimamisha mfalme wao wenyewe. Jambo hili liliungwa mkono na wananchi. Ban Chao licha ya kuweza kutumia ujanja wake kuwafyeka maadui, bali pia alikuwa hodari wa kuwashawishi wafalme waungane pamoja kupigana na maadui. Sha Che ilikuwa dola yenye nguvu, wakati huo mara kwa mara ilishambulia mataifa mengine ya magharibi. Ban Chao aliunganisha madola hayo kuishinda dola hiyo. Tokea hapo jina la Ban Chao lilikuwa likivuma sana katika sehemu ya magharibi ya China.
Katika muda wote wa miaka 31 alipokuwa katika sehemu ya magharibi, Ban Chao alifanya michango mingi mikubwa katika vita na diplomasia, akarudisha tene uhusiano wa Han na nchi nyingine uliokatika zaidi ya miaka 60, na alisaidia madola ya magharibi kutuliza ghasia na kuwashinda maadui wa nje. Kwa hivyo Ban Chao alipendwa sana na watu wa nchi za magharibi, aliporudi nyumbani Han kwa kuagizwa na mfalme wake, hata watu walilia machozi wakishika miguu ya farasi kumzuia asiwaache.
Ban Chao aliyekuwa msomi hapo awali na kushika silaha baadaye akawa mfano bora wa wasomi wa kujitolea kwa taifa.
Mao Sui Ajipendekeza kwa Kazi
Kuna usemi wa Kichina unaosema "kama kweli ni dhahabu, basi itang'ara tu". Hadithi ya Kichina ya "Mao Sui ajipendekeza kwa kazi" ndio inaeleza usemi huo.
Katika Kipindi cha Madola ya Kivita, mji mkuu wa Dola la Zhao Handan ulivamiwa na askari wa Dola la Qin lenye nguvu, mji ulikuwa katika hali ya kutekwa.
Ili kuuokoa mji wa Handan mfalme wa Dola la Zhao alitaka kushirikiana na Dola la Chu lenye nguvu vile vile kupambana na Dola la Qin. Alimtuma mtoto wake Ping Yuanjun kwenda kumshawishi mfalme wa Dola la Chu.
Kabla ya safari, Ping Yuanjun alitaka kuchagua washauri hodari 20 kati ya mawaziri, lakini mwishowe alichagua mahodari 19 tu. Wakati huo alikuja mtu mmoja bila kualikwa, alijipendekeza kujaza pengo la mtu mmoja. Huyo alikuwa Mao Sui.
Ping Yuanjun alimwangalia na kumwuliza, "Wewe ni nani? Una shida gani nami?"
Mao Sui alimwambaia, "Jina langu ni Mao Sui. Nimesikia utakwenda Dola la Chu kwa ajili kuuokoa mji wa Handan, napenda kufuatana nawe."
Ping Yuanjun alimwuliza, "Umefanya kazi kangu kwa muda gani?"
Mao Sui alijibu, "miaka mitatu."
Ping Yuanjun alisema, "Muda wa miaka mitatu si mfupi. Mtu akiwa hodari ni kama sindano ya viatu iliyotiwa mfukoni ambayo itatoboa mfuko mara moja. Lakini wewe umekuwa na miaka mitatu hapa, na sijasikia uhodari wako. Safari yangu ya kwenda Dola la Chu inahusika na msaada wa jeshi na hatima ya taifa, mtu asiye hodari haifai kwenda huko, basi wewe baki basi."
Ping Yuanjun alisema moja kwa moja. Lakini Mao Sui alimjibu kwa uhakika, "Umekosea, sio mimi sina uhodari, bali wewe hukunitia mfukoni. Ungenitia mfukoni, uhodari wangu ungeonekana kama sindano ya viatu."
Kutokana na mazungumzo, Ping Yuanjun alimwamini na kukubali. Baada ya kupata washauri 20 alifunga safari nao kwenda kuzungumza na mfalme wa Dola la Chu. Baada ya kuwasili Dola la Chu Ping Yuanjun alimweleza vilivyo haja yake ya kupata ushirikiano wa Dola la Chu ili kupambana na Dola la Qin, lakini mfalme wa Dola la Chu alikuwa kimya. Mazungumzo yao yaliendelea mpaka mchana bila matokeo yoyote. Wafuasi 20 walisubiri nje wakiwa na wasiwasi.
Mao Sui alifuatana na Ping Yuanjun kwa kujipendeza, kwa hiyo wengine 19 walimdharau, wakifikiri kuwa alijitukuza tu. wakati huo walitaka kumwadhiri,
"Ndugu Mao, mazungumzo yamekuwa marefu, unaonane uingie na kuona hali ilivyo?"
Mao Sui alikubali. Alichomeka kitara kiunoni na kufika mbele ya mfalme wa Dola la Chu, alisema,
"Mheshimiwa mfalme, ushirikiano wa Chu na Zhao ni wa lazima. Hilo ni jambo la maneno mawili matatu tu kwa kufanya uamuzi. Lakini toka asubuhi mpaka sasa hujaamua, kwa nini?"
Kujitokeza kwa Mao Sui kulimkasirisha mfalme wa Chu, badala ya kuongea naye, alimwuliza Ping Yuanjun kwa hasira,
"Ni nani huyu?"
Ping Yuanjun alijibu, "Ni mfuasi wangu."
Kwa hamaki, mfalme Chu alimkaripia Mao Sui,
"Mimi nazungumza bwana wenu, wewe ni kama nani kujiingiza katika mazungumzo yetu!"
maneno ya mfalme Chu yalimhamakisha Mao Sui, alitoa kitara chake kutoka ala, akapiga hatua mbele ya mfalme na kusema kwa ukali,
"Mheshimiwa, sababu yako ya kuthubutu kunipokea si unaona dola lako kubwa? Na kutegemea pembeni mwako wako walinzi? Lakini sasa nakuambia, yote hayo hayasaidii kitu ninapokuwa mbele yako kwa kitara, uhai wako uko mkononi mwangu!"
Mfalme Chu alilowa jasho kwa hofu, alikuwa kimya.
Mao Sui alisema, "Dola la Chu lina nguvu, linastahili kuwa mwamba kati ya madola yote, lakini rohoni mwako unaogopa Dola la Qin. Dola la Qin lilishambulia dola lake mara nyingi na kunyakua ardhi yako, ni aibu namna gani hiyo! Hata sisi watu wa Dola la Chu tunakuonea fedheha. Sasa tumekuja kuomba ushirikiano wako kwa ajili ya kuuokoa mji wa Handan, lakini huku tunakusaidia kulipiza kisasi. Lakini wewe ni mhofu kama hivi, huoni aibu!"
Kutokana na maneno ya Mao Sui, mfalme Chu alisikitika sana.
Mao Sui aliongeza, "Mheshimiwa mfalme, vipi sasa? Utakubali kushirikiana nasi kupambana na Dola la Qin?"
"Nakubali, nakubali!" mfalme akajibu haraka.
Baada ya Dola la Chu na Zhao kutia saini mkataba wa kushirikiana kupambana na Dola la Qin, akina Ping Yuanjun wakarudi mjini Handan na kumwambia mfalme wa Dola la Chu,
"Bahati njema Mao Sui alifuatana nami, kwa ulimi wake ametupigia jeki kuliko nguvu za askari milioni moja." Kabla ya siku tatu kupita, jina la Mao Sui lilienea miongoni mwa watu wa mji wa Handan. Baadaye methali hiyo hutumika kueleza kuwa mtu mwenye uwezo anajipendekeza kwa kazi.
"Ushindani wa Fikra za Aina Mia "
Msemo wa Kichina "Ushindani wa Fikra za Aina Mia" ulianzia siku za kale katika Enzi ya Madola ya Kivita. Katika enzi hiyo, falsafa za aina nyingi zilikuweko kwa pamoja, wanasalsafa walikuwa wakitoa maoni na mitizamo yao huria, wakijadiliana, wakichapisha vitabu na kufundisha wanafunzi wao, hali hii ya ustawi wa falsafa tofauti katika uwanja wa taaluma ulipamba moto. Yafuatayo ni maelezo kuhusu msemo huo.
Enzi ya Madola ya Kivita iliyokuwa kabla ya karne ya tano mpaka karne ya tatu kabla ya kuzaliwa Kristo ilikuwa ni kipindi cha mwanzo wa ustaarabu wa China. Madola mengi yalikuwa pamoja na fikra za aina nyingi tofauti pia zilistawi katika jamii. Ili kuwavutia wasomi wa madola mbalimbali wajadiliane huria na kuwafundisha wanafunzi wao, mfalme wa Dola ya Chi alijenga kasri moja kubwa nchini mwake. Mwanaye Chi Xuanwang pia aliwapenda sana mabingwa wa fasihi na washauri wa kuzuru, kwa hiyo alijenga hosteli nyingi ili kuwahudumia bure. Wasomi waliokuja mji mkuu wa Dola ya Chi walifikia hata elfu, Dola ya Chi ikawa kama kituo cha ufafanuzi wa fasihi, falsafa na sayansi. Kila aina ya falsafa na taaluma ilijitahidi kujitangaza na kupinga aina nyingine, na ilitaka wafalme wa madola yote wapokee fikra zao katika utawala wao. Huu ndio msemo wa "ushindani wa fikra za aina mia".
Sasa nawasimulieni kisa kimoja cha mfano: siku moja Chi Xuanwang alisema mbele ya Mencius: "Nimesikia kwamba mfalme Zhou Wenwang alijitengea sehemu ya uwindaji yenye eneo la kilomita za mraba 35, lakini wananchi wanaona kuwa sehemu hiyo ni ndogo, hali ambapo mimi nimejitengea sehemu ya uwindaji yenye eneo la kilomita za mraba ishirini tu, hata hivyo wananchi wanalalamika wakisema kuwa sehemu hiyo ni kubwa. Hivi leo wananchi hawajali mantiki". Mencius akamwambia, "Ingawa sehemu ya uwindaji aliyojitengea mfalme Zhou Wenwang ni kubwa kiasi cha kilomita za mraba 35, lakini wananchi wanaruhusiwa kuingia ndani kukata kuni na kuwinda, kwa hiyo mfalme anatumia sehemu hiyo na wananchi kwa pamoja, ndio maana wananchi wanataka sehemu iwe kubwa zaidi. Mimi nilipokuja kwenye dola ya Chi nilisikia kwamba sehemu yako ya uwindaji hairuhusu wananchi kuingia mule ndani, na pindi mtu akiingia huadhibiwa. Kwa hiyo ingawa sehemu yako ni ndogo kiasi cha kilomita za mraba 20 tu lakini wananchi hawaambulii chochote, hii ndio sababu ya wao kuona sehemu yako kuwa kubwa, kwani hii sio kawaida?" Mfalme wa Dola ya Chi aliona aliyosema ni hoja kabisa, basi akawaruhusu wananchi kuitumia sehemu yake. Fikra hizi za Mencius ndio zilitetewa na Confucius, yaani "Ukarimu".
Fikra zilizotetewa na tapo la Mo Ti ziligongana moja kwa moja na fikra za Confucius, kwamba zinakataza adabu nyingi na harija kubwa za mazishi, bali zilitetea "kubana matumizi", na pia zilipinga vikali vita kati ya madola, zilitetea amani. Kufuatana na fikra za Mo Ti, iwapo watu wanaishi bila ubadhirifu na kwa kupendana, basi dunia itakuwa na amani daima.
Lilikuwepo tapo lingine la fikra ambalo liliwakilishwa na fikra za Han Fei, huyu ni mwanafalsafa wa uyakinifu. Alitetea mageuzi, aliona kwamba jambo lolote huwa na sheria yake ya mwanzo na mwisho. Yeye alikuwa ndio wa kwanza kutoa hoja ya "hitilafu". Alieleza ngano moja: Mtu mmoja aliuza mkuki na ngao. Alimwambia mtu aliyetaka kununua mkuki akisema, mkuki wake unaweza kutoboa ngao yoyote duniani, kisha alimgeukia mtu mwingine aliyetaka kununua ngao, akisifu ngao yake inaweza kukinga mkuki wowote duniani. Basi mtu wa tatu aliuliza pembeni: Nikitumia mkuki wako kutoboa ngao yako je? Muuzaji alishindwa kujibu. Kutokana na ngano hiyo Han Fei alitoa hoja ya kuwa kila jambo huwa na pande mbili.
Katika siku za fikra za aina tofauti mashindano ya wasomi licha ya kufundisha wanafunzi pia waliandika vitabu, wakajitokeza wawakilishi kadhaa wa matapo ya fikra tofauti kama Mencius, Zhuanzi, Hanfei, na Mo Ti, ambapo walichapisha maandishi mengi ya taaluma. Fikra zao zilisogeza sana mbele fikra na maendeleo ya utamaduni wa China ya kale. Hivi leo watu wanaendelea kutumia msemo huu wanapofananisha na ushindani huru wa fikra tofauti.
"Safari ya Kwenda Magharibi", Wu Chengen.
Katika historia ya fasihi ya kale ya China yako maandishi makubwa manne, ambayo ni riwaya ndefu za "Madola Matatu ya Kifalme", "Mashujaa katika Vijamasi", "Safari ya Kwenda Magharibi" na "Ndoto kwenye Chumba Chekundu". Leo katika kipindi hiki nimewaletea maelezo kuhusu mwandishi wa riwaya ya "Safari ya Kwenda Magharibi", Wu Chengen, mwandishi mashuhuri katika Enzi ya Ming iliyoanzia mwaka 1368 hadi 1644.
Wu Chengen ni mwenyeji wa wilaya ya Huai An mkoani Jiangsu, ambapo tangu utotoni alikuwa mwerevu na mshabiki wa mambo mengi. Alikuwa hodari wa kuchora picha, usanii wa maandiko ya Kichina kwa brashi ya wino, pia alipenda kukusanya na kuhifadhi picha na maandiko ya watu mashuhuri. Alipokuwa kijana jina lake lilikuwa maarufu sana katika sehemu ya makazi yake kwa sababu ya kipaji chake cha fasihi. Lakini mara nyingi alishindwa katika mitihani ya kifalme ya kuchagua maafisa, na maisha yake yakawa ya shida. Kutokana na hayo akagundua ubovu ulioenea miongoni mwa maafisa na jinsi jamii ilivyotatanika, akawa na kinyongo moyoni mwake. Katika shairi lake moja alisema kwamba ubovu wa jamii unatokana na mfalme kuwatumia maafisa wabovu. Alitaka kubadilisha hali hiyo lakini hakuweza kufanya lolote ila kuipigia kite. Hivyo aliweka matumaini na kinyongo chake kwenye riwaya yake ya "Safari ya Kwenda Magharibi".
"Safari ya Kwenda Magharibi" ni riwaya nzuri katika historia ya fasihi ya kale ya China. Riwaya hii ilitungwa kwa mujibu wa vituko vilivyomkuta sufii mkubwa wa dini ya Kibuda, Tang Zeng, alipokuwa katika safari yake ya kwenda India kuchukua msahafu katika karne ya 7 K.K. Katika riwaya hiyo Wu Chengen alibuni wafuasi watatu kufuatana na sufii huyo. Mmoja wa wafuasi wake alikuwa mfalme kima Sun Wukong. Sun Wukong alikuwa na nguvu za kudura ya mungu, anaweza kujigeuza sura 72 na fimbo yake ya kupambana na mashetani yaweza kurefushwa kuwa ndefu hadi mbinguni na kufupishwa kuwa ndogo hadi kama sindano ya kutia sikioni. Mfalme kima Sun Wukong ndiye aliyethibitisha matumaini ya mwandishi kwamba mambo yote maovu yatatokomeza kabisa katika jamii.
"Safari ya Kwenda Magharibi" iliandikwa na Wu Chengen katika miaka yake ya uzeeni, lakini matayarisho ya riwaya hiyo yalimgharimu maisha yake yote. Alipokuwa mtoto mara kwa mara alifuatana na baba yake kwenda kwenye misitu minene na mahekalu, na baba yake humweleza hadithi za ajabu zilizotokea huko. Hamu yake ya kusikiliza hadithi utotoni mwake haikupungua hata baada ya yeye kuwa mtu mzima. Baada ya kutimiza miaka 30 alikuwa amekusanya hadithi nyingi za ajabu akanuia kuandika riwaya. Alipofikia umri wa miaka 50 hivi alikuwa amemaliza sura 10 za mwanzo za riwaya yake ya "Safari ya Kwenda Magharibi", lakini baadaye kwa sababu fulani aliacha kwa miaka mingi hadi baada ya kujiuzulu kazi na kuwa nyumbani.
"Safari ya Kwenda Magharibi" iliandikwa hadithi moja moja, lakini kila hadithi pia ni sehemu ya riwaya nzima. Ndani ya riwaya hiyo walitokea mashetani na miungu mingi ambao wanawakilisha haki na uovu. Kasri ya mbinguni ilionekana adhama sana lakini kwa kweli mungu aliyekuweko ndani ya kasri hiyo alikuwa mbabaishaji wa watu wema na wabaya, akilenga mfalme duniani; na kasri ya dunia ya pili ingawa ilionekana ukakamavu, lakini maofisa wanasaidiana katika hatia, walikuwa hawajali sheria na wadhulumiwa hawakuweza kupata haki. Hayo alilenga katika hali ya utawala wa kifalme. Mashetani walikula na kuwaua watu huku wakiwa wachoyo wa mali na kupenda warembo na kufanya uovu watakavyo. Katika hayo mwandishi alifananisha madhalimu na maofisa wa kifalme. Kwa upande mwingine Wu Chengen alifanikiwa shujaa kima Sun Wukong, ambaye alikuwa mtetezi wa haki, alikuwa na nguvu za kudura ya mungu na mwenye msimamo bayana kati ya watu wema na wabaya, fimbo yake ina nguvu za ajabu. Hii inaonyesha tarajio la Wu Chengen la kukomesha maovu yote katika jamii aliyoishi.
Riwaya ya "Safari ya Kwenda Magharibi" inajulikana sana kutoka kizazi hadi kizazi na katika miaka mia kadhaa iliyopita riwaya hii ni kama chimbuko la kutunga hadithi kwa watoto na michezo ya filamu na televisheni.
Kutunga Shairi kwa Hatua Saba
China ina historia ndefu ya miaka elfu tano kwa mujibu wa rekodi. Katika historia ndefu kama hiyo utamaduni wake wa aina mbalimbali ulikuwa ukitajirika zaidi na zaidi kutoka enzi hadi enzi. Utamaduni huu ni kama uhondo tunaoufaidi bila mwisho. Mila na desturi, riwaya, hadithi, matukio na watu wenye vipaji, n.k. mengi yalitokea na yanaendelea kuathiri kwa kina Wachina wa sasa. Leo, katika kipindi hiki nitawasimulieni hadithi kuhusu mtu mmoja mashuhuri, aliyeitwa lake Cao Zhi.
Baba yake Cao Cao alikuwa mwanzilishi wa Dola ya Wei katika karne ya pili, Enzi ya Madola Matatu ya Kifalme. Maisha yake yote yalikuwa ya kupigana vita, lakini pia alikuwa mshairi hodari na mashairi yake mengi yanasomwa mpaka hivi leo. Cao Cao alikuwa na watoto wawili, wote wa kiume. Mkubwa aliitwa Cao Pi, na wapili Cao Zhi. Baada ya Cao Cao kufariki, mwanawe wa kwanza Cao Pi alirithi kiti chake cha ufalme. Cao Pi alikuwa mhakiki wa fasihi, na kitabu chake "Tasnifu" ni utunzi wa kuanza kipindi kipya katika historia ya uhakiki wa fasihi. Mtu anayeelezwa katika kipindi hiki ni ndugu yake Cao Zhi, mtoto wa pili wa Cao Cao. Cao Zhi alikuwa mtu mwenye kipaji kikubwa katika fasihi, alikuwa mshairi hodari wa mwisho katika enzi yake.
Kaka yake Cao Pi baada ya kurithi kiti cha ufalme alimwonea gere kwa kipaji chake cha fasihi. Hata siku moja kwa makusudi alitaka kumtesa, ila atunge shairi moja kamili kabla ya kupiga hatua saba, na shairi lenyewe lilitakiwa liwe na vina. Cao Zhi alielewa kwamba kaka yake alimkanganya kwa makusudi, lakini hakuweza kumkatalia kwa kuwa yeye alikuwa mfalme. Huku akifikiria kuwa anayemtesa ni kaka yake wa tumbo moja, Cao Zhi alijawa na huzuni na hasira, na papo hapo alitunga shairi lake lenye beti nne:
Kunde zachemshwa na vikonyo vyake sufuriani,
Kunde zalia machozi kwa huzuni,
Kunde na vikonyo vyatokana na mzizi mmoja awali,
Ya nini kutesana hivi kikatili.
Shairi hili lilimgusa kaka yake, aliona haya, akaacha nia yake ya kumtesa.
Ufanisi mkubwa wa Cao Zhi maishani mwake ulikuwa tungo zake za mashairi. Katika Enzi ya Madola Matatu ya Kifalme, vita vilikuwa vikiendelea kwa mfululizo, vita vilisababisha jamii kunyauka. Ingawa alikuwa na nasaba ya kifalme lakini aliwahurumia sana wananchi maskini na waliopoteza maskani yao. Dunia ilivyokuwa ya fujo na hali ilivyokuwa ya masikitiko ilimwamsha uzalendo wake, hata katika shairi lake aliandika hivi, "Jitolee mhanga kuokoa taifa, kufa ni kama kuzaliwa". Ubeti huu ni maarufu katika enzi zote.
Ingawa Cao Zhi alikuwa na ujuzi mkubwa wa kutunga mashairi, lakini hakuridhika nao, bali alikuwa siku zote akitaka kufanikisha mambo ya kisiasa. Kutokana na hayo alishukiwa na kunyanyaswa na kaka yake mfalme, maisha yake yalikuwa hayamwii shwari. Mengi ya mashairi yake yalieleza jakamoyo yake ya kutoweza kukamilisha ndoto yake, lakini alikuwa hawezi kujieleza kinaganaga. Kutokana na sababu hiyo, hali ya ajabu ilitokea katika mashairi yake, kwamba alisawiri wasichana wengi warembo, kama vile katika vitabu vyake vya "Juzuu ya Mashairi ya Vipusa", "Warembo wa Nchi ya Kusini" n.k. Warembo katika mashairi yake walikuwa sio tu waliumbika kikamilifu bali pia ni wasichana wenye ujuzi mkubwa, maadili mazuri na wenye matumaini mema, aliandika hivi ili kujiliwaza. Miongoni mwa mashairi kama hayo, uliojitokeza ziadi ni Utenzi wa "Malaika Luo Shui". Luo Shui ni jina la mto karibu na Mji wa Luo Yang. Katika hadithi ya mapokeo msichana mmoja alijitosa mtoni na baadaye akawa malaika. Kwa kutumia hadithi hii Cao Zhi alisawiri msichana mmoja mwenye haiba nyingi, na alieleza uchungu wake asiweze kumwoa malaika huyo kutokana na kuwa binadamu. Ingawa mhusika mkuu huyo ni wa kubuniwa tu lakini kwa ustadi wake mkubwa alimsawiri jinsi alivyovutia kama alivyo hai. Alieleza, "Dansi aliyocheza kama bata-maji arukavyo angani, nyonga aliyokatika kama joka majini". Utenzi huu unasifiwa na wanafasihi wote.
Cao Zhi mwenye kipaji cha mashairi alikuwa na miaka 41 tu duniani, lakini athari zake ni kubwa katika fasihi nyuma yake. "Kutunga shairi kwa hatua saba" umekuwa msemo wa kueleza fulani mwenye kipaji kikubwa cha fasihi.
" Mwanzo Dharau, Mwisho Heshima "
" Mwanzo Dharau, Mwisho Heshima " ni msemo mmojawapo wa Kichina. Sasa nakusimulieni kisa chenyewe.
Karne ya tano kabla kuzaliwa Kristo ilikuwa Enzi ya Madola ya Kivita nchini China. Katika kipindi hiki yalikuwako madola mengi,lakini saba kati yao yaliyojitokeza zaidi, nayo ni Qin, Chu, Qi, Yan, Han, Zhao, Wei. Dola la Qin ambalo lilikuwa kaskazini-magharibi mwa China, yaani Jimbo la Shanxi kwa leo, lilikuwa na nguvu zaidi kwa sababu ya kufanya mageuzi ya kisiasa na kiuchumi. Dola hili lilikuwa mara nyingi likichokoza madola mengine sita. katika kukabiliwa na hali hiyo, ndani ya tawala za madola sita, yalitokea makundi mawili tofauti kuhusu namna ya kushughulikia Qin. Kundi moja lilitetea kwamba madola yote sita yafanye "yaungane na Qin", yawe marafiki na Qin na kujitahidi kutoudhi dola hilo isije ikawa kisingizio cha kuleta uchokozi. Kundi lingine lilitetea kwamba madola yote sita "yaungane dhidi ya Qin".
Walikuwako washauri wengi waliokuwa wakieneza utetezi wao katika madola yote saba. Iwapo utetezi fulani ungekubaliwa, mshauri mwenyewe angejulikana, thamani yake ingekuwa kubwa mno. Mshauri Su Qin alikuwa mmojawapo.
Mshauri huyo kwanza alifika katika Dola la Qin akijaribu kueneza utetezi wake wa "kuungana na Qin", kuhamasisha Dola la Qin kutuliza madola sita, na baadaye kuyateka. Qin ilikana utetezi wake kwa kusema kwamba haikuwa na hamu na utetezi huo, lakini ukweli ni kwamba wakati huo Dola la Qin lilikuwa bado halijatayarishwa vya kutosha kuyameza madola sita. Su Qin hakuwa na ujanja; ilikuwa karibu aishiwe na nauli na nguo zake zilikuwa zimechakaa, basi akarudi makwao kwa masikitiko.
Familia yake ilipomwona jinsi alivyokuwa katika simanzi, wazazi walikosa hamu ya kuzungumza naye; mkewe aliyekuwa akiendelea kufuma nguo hata hakumwinulia macho. Aliomba mke wa kaka yake ampatie chakula, lakini badala ya kuandaliwa chakula alilaumiwa. Su Qin aliona uchungu rohoni mwake, akaazimia kusoma ili kujiimarisha. Alikuwa akisoma usiku na mchana, kufafanua mbinu za kivita, usingizi ulipomwelemea aliweza hata kujichoma sindano kwenye paja lake. Na ndipo usemi wa "Kuchoma sindano ili kusoma" ukaanzia hapo.
Su Qin alifanya utafiti juu ya hali ya kila dola, mwishowe aliona kuwa "muungano dhidi ya Qin" ungeweza kukubalika, hivyo alianza kushawishi madola sita. Kweli muungano huo uliongozwa na Dola la Chu ukapatikana, Su Qin akawa kamanda mkuu. Kwa sababu ya muungano huo, Dola la Qin likatulia tuli lisithubutu kuvamia dola lingine. Utulivu huo uliendelea kwa miaka 15 mpaka mfalme Qin Shihuang alipounganisha China nzima.
Ilivyokuwa Su Qin alikuwa ni amirijeshi mkuu, amejipatia heshima kubwa katika madola sita. Siku moja alisafiri kikazi alipita nyumbani kwake Luo Yang. Kusikia habari hiyo maofisa wa sehemu waliamrisha kusafisha barabara, na walikuwa tayari mapema kumkaribisha foleni. Wazazi wake walisepetukasepetuka wakafika mwanzo wa njia wakimsubiri. Baada ya Su Qin alipofika nyumbani, mkewe alinyamaza pembeni asithubutu kutazamana naye uso kwa uso. Mke wa kaka yake ndiye aliyekuwa akinyenyekea kumsalimu. Su Qin alisema, "Shemeji, mbona unavyonifanyia leo ni tofauti kabisa na hali ya zamani. Kabla ya hapo ulinibeza, na sasa unanitukuza." Shemeji alijibu huku mwili ukimtetemeka, "Nawezaje kuthubutu kukutendea kama zamani, hali umekuwa mwenye cheo kikubwa na umetajirika sana." Su Qin alishusha pumzi na kusema, "Mtu akiwa maskini hudharauliwa na wazazi wake, akiwa tajiri hata jamaa zake humwogopa, hii ndio sababu ya watu kuyamezea mate madaraka!"
Hiki ndicho kisa cha msemo wa "Mwanzo dharau, mwisho heshima", ikieleza wale wanaopima watu kwa sura, au cheo na mali.
Kuchuma Maua katika Bustani ya Qujiang
Katika karne ya nane wakati Enzi ya Sui nchini China, mfalme alianzisha utaratibu wa kufanya mtihani wa kuchagua maofisa wakubwa wa serikali, hadi Endi ya Tang utaratibu huo uliendelea na kuwa wasomi wa kawaida waliweza kushiriki katika mtihani huo, kwa hiyo utaratibu huo ulikuwa njia ya kujipatia nyadhifa kwa wasomi wote.
Mtihani uligawanyika katika ngazi tatu, ngazi ya mwisho ni mtihani wa kuchagua maofisa wakubwa ambao wanaweza kufanya kazi karibu na mfalme, lakini mtihani huo ulikuwa mgumu kiasi kwamba hata kati ya watu mia moja waliofanya mtihani, waliochaguliwa hawakufika ishirini. Watu wengi walishindwa mara kadhaa, na baadhi walifaulu mtihani hadi walipokuwa na umri wa zaidi ya miaka hamsini.
Mfalme alikuwa anafanya sherehe kubwa kuwapongeza waliofanulu mtihani katika bustani ya Qujiang mjini Xi'an, mji mkuu wa Enzi ya Tang.
Bustani ya Qujiang ilikuwa kubwa, ndani yake kuna ziwa kubwa, maua, pagoda ya Dayan na mahekalu.
Kwenye sherehe, waliofulu mtihani waliweka mabakuli yenye pombe juu ya maji, mabakuli yalielea na yanapotulia karibu na fulani basi yeye anachukua bakuli hilo kunywa pombe na kutunga mashairi, na kuwaalika vijana wawili kwenda kuchuma maua na kumpa kila mmoja wa waliofaulu mtihani kutia kifuani.
Mwaka mmoja, mfalme alifanya sherehe katika bustani hiyo, na baada ya kumaliza sherehe, wasomi waliofaulu mtihani walitembea katika bustani hiyo. Mmoja kati ya wasomi hao alipofika kwenye pagoda ya Dayan alichonga jina lake kwenye jiwe la pagoda hiyo, tokea hapo kuchonga majina ya wasomi waliofaulu mtihani ikawa ni desturi, kwamba baada ya sherehe ya mfalme kila mmoja alikuwa anachonga jina lake kwa wino, na kama baadaye fulani alikuwa jemadari au waziri basi jina lake lilikuwa linapakwa rangi nyekundu.
Utaratibu wa kuchagua maofisa kwa kuwafanyia mtihani uliwawezesha wasomi wa kawaida kabisa kupata nafasi ya kuwa maofisa wakubwa wa kusimamia mambo ya taifa. Lakini utaratibu huo ulibadilika kuwa mbaya, hasa katika enzi za Ming na Qing, mtihani ulibadilika kuwa wa vitabu vya Confucius tu, na makala ilikuwa ni lazima iwe na idadi maalumu ya maneno na mtindo maalumu. Mtihani huo ulikuwa wa kuchezea maneno bila maana. Vitabu vya "Hadithi za Mashetani" na "Mashujaa kwenye Vinamasi" vilifichua ubovu wa mtihani huo.
"Uongo ukirudia mara tatu ukawa kweli"
Uzushi na kashfa zikivuma kwa marudio, huaminika kuwa kweli. Kifuatacho ndicho kisa chenyewe:
Katika karne ya tano kabla ya Kristo kuzaliwa, nchini China yalikuwako madola madogo madogo mengi, na madola hayo yalikuwa hayaishi kupigana vita kunyakuana ardhi, kwa hiyo wanahistoria wa baadaye wanaziita enzi hizi kuwa "Enzi za Madola ya Kivita".
Lakini hata hivyo yalikuwako madola mawili yaliyopakana, Dola la Wei na Dola la Zhao, yaliahidiana kuweka urafiki kwa mkataba. Ili kuhakikisha mkataba huo ufuatwe, madola haya yalikubaliana kupeana makole kama ni wadhamini. Mfalme wa Wei aling'amua kumpeleka mwanawe kwenye mji mkuu wa Dola la Zhao, Handan, pamoja na mwanawe kwenda huko pia alikuwako waziri wake, Pang Cong, ili kuhakikisha mwanawe katika hali ya usalama.
Peng Cong alikuwa na wapinzani kadha ndani ya kasri kwa kumwonea gele umahiri wake. Kwa hiyo, alikuwa na wasiwasi kwamba angesingiziwa asipokuwepo. Kufikiri hivyo, kabla ya yeye kuondoka alionana na mfalme wake, alisema:
"Mheshimiwa mfalme, ikiwa fulani atakuambia chui amekuja mjini kwenye barabara, utaamini?"
Mfalme alijibu haraka, "Hataa, chui anawezaje kuja hata barabarani?"
Pang Cong aliuliza zaidi, "Ikiwa watu wawili wakikuambia hivi, utaamini?"
Mfalme alijibu, "Kama nikiambiwa hivi na watu wawili, nitakuwa na tuhuma kidogo."
Pang Cong aliendelea, "Ikiwa watu watatu je?"
Mfalme alisita kidogo kisha alimwambia, "Nikiambiwa na wote watatu, basi inanipasa niwaamini."
Kusikia majibu hayo, Peng Cong aliingiwa na wahka zaidi, alishusha pumzi na kusema, "Mheshimiwa, jua kwamba chui hawezi kuja barabarani, huu ni ujuzi wa kawaida kwa kila mtu. Almradi watatu wamesema hivi, basi usemi wa chui wa barabarani ukawa wa kweli. Umbali kati ya mji mkuu wa Dola la Zhao, Handan, na mji mkuu wetu Daliang ni mkubwa sana kuliko umbali kati ya kasri na barabara, na watakaonisengenya pengine watazidi watatu."
Mfalme alielewa maana aliyokusudia, akasema, "Nishakuelewa, nenda tu usiwe na wasiwasi!"
Basi Pang Cong na mwana wa mfalme walifunga safari kwenda mji wa Hanadan.
Kweli haikuwa muda mrefu kupita baada ya Pang Cong kuondoka, maneno mabaya juu yake yakaanza kuvuma. Mwanzoni mfalme alikuwa humzungumzia, akisema Pang Cong ni mahiri tena ni mtiifu. Lakini wapinzani walikuwa wanarudiarudia kashfa zao, mwishowe mfalme akawaamini kabisa. Baada ya Pango Cong kurudi nchini kutoka Dola la Zhao mfalme hata hakumruhusu aonane naye.
Pia kiko kisa kingine kinachofanana na hiki: Zeng Can alikuwa msomi katika Enzi ya Madola ya Kivita. Yeye alikuwa mwadilifu kamili. Siku moja alisafiri mbali. Kwa sadfa alikuwako mhalifu mmoja mwenye jina sawa na lake, alikamatwa. Jirani kwa haraka alimhabarisha mama yake, "Toba! mwanao amekamatwa kwa uhalifu wa uuaji". Mama wa Zeng Can alimwamini kabisa mwanawe kwamba uhalifu kama huu kamwe mwanawe hauwezi, aliendelea kufuma nguo yake. Punde si punde mwingine alikuja akimwambia mama huyo, "Ala, mwanao ameua mtu!" Hapo, mama huyo akaanza kushikwa na wasiwasi, lakini pia hakuamini. Muda si muda mtu wa tatu akaja na maneno yale yale. Wakati huo mama huyo akawaamini kabisa, alitupa kazi yake akatoroka haraka.
Visa hivi vyote vinatuambia "ULIMI UNAUA".
Kuwa katika Hali ya Kuzingirwa na Wapinzani Pande Zote
Tuseme Fulani akikumbwa na matatizo mengi na hali ya mazingira yenyewe inaelekea kuwa hakika huyo atashindwa, usemi wa Kichina hueleza mtu kama huyo amekuwa katika hali ya kuzingirwa na wapinzani pande zote. Sasa nawaelezeni changzo cha usemi huo jinsi ulivyotokea:
Katika mwaka 202 kabla ya kuzaliwa Kristo historia ya China iliingia katika Enzi ya Kifalme ya Qin. Sanamu za askari na farasi zilizofukuliwa katika Jimbo la Shaansi pamoja na Ukuta Mkuu yote ni masalio ya utamaduni wa enzi hiyo.
Wafalme wa enzi hiyo walikuwa wakijitahidi kutukuza ufahari wao, na kati ya wafalme hao aliyejitokeza zaidi alikuwa Qin Shihuang. Huyo mfalme alijengesha kasri kubwa ya fahari na kaburi la starehe kwa pesa nyingi alizozinyonya kutoka kwa wananchi wake. Hivyo basi wananchi walikuwa wakiinuka mara kwa mara, matokeo yakawa Enzi ya Qin ilipinduliwa baada ya miaka 15 tu tangu ilipoanza. Baada ya Enzi ya Qin kupinduliwa, vilikuwako vikundi viwili vilivyokuwa vikijitahidi kunyakua utawala wa China. Kimoja kiliongozwa na Xiang Yu, kingine kiliongozwa na Liu Bang.
Xiang Yu alikuwa jamadari katika sehemu ya Chu mwenye hulka ya unyoofu, ujeuri na ni mjasiri wa kupigana vita. Liu Bang alikuwa ofisa mdogo kabla ya Enzi ya Qin kupinduliwa mwenye hulka ya ujanja na ni hodari wa kuchagua wasaidi wake. Katika siku za kupindua Enzi ya Qin hao wawili walikuwa ndugu wa kuchanjiana wakisaidiana katika hali na mali. Lakini baada ya tu kufanikiwa kupindua Enzi ya Qin wakageukiana.
Mwanzoni nguvu za Xiang Yu zilimzidi kabisa Liu Bang, alijitawaza kuwa "Mbabe Chu" ambaye ni kama mfalme, Liu Bang akatawazwa kuwa "Mwinyi Han" ambaye ni kama mtawala wa sehemu tu. Ili kuhifadhi nguvu Liu Bang alijidai kukubali utawala wa Xiang Yu, lakini kichini chini aliwakusanya mahodari na kuzidisha nguvu zake za kijeshi. Hivyo basi zaidi na zaidi nguvu zake zikawa zinalingana na nguvu za Xiang Yu.
Vita baina ya Xiang Yu na Liu Bang viliendelea kwa miaka kadha. Kipindi hiki kinaitwa "Vita vya Chu na Han" katika historia. Katika vita Xiang Yu alimshindilia mbali Liu Bang na aliwateka nyara baba na mkewe. Xiang Yu alimtia kizuizini baba wa Liu Bang kama kole, akimdai Liu Bang asalimu amri, sivyo atamchinja na kumchemsha kuwa supu. Lakini bila kutazamiwa, Liu Bang akamwambia Xiang Yu, "Tulipopambana na Qin tulikuwa ndugu, basi baba yangu ni yako pia, ikiwa ukitengeneza supu kwa baba yangu basi usisahau kunigawie." Kusikia hayo Xiang Yu alikuwa hana budi ila kumrudishia Liu Bang baba yake na mkewe.
Vita vya kuamua mshindi vilipigana katika sehemu ya Gaixia [Jimboni Anhui kwa leo]. Vita vilikuwa vikali na mwishowe askari wa Liu Bang walimzingira Xiang Yu na askari wake. Ingawa Xiang Yu alikuwa katika hali mbaya lakini bado alibaki na askari kiasi cha laki moja na Liu Bang hakuweza kuwafyeka kwa mkupuo.
Siku moja usiku, ghafla Xiang Yu na askari wake waliozingirwa walisikia nyimbo walizozoea kutoka pande zote, wakateka zaidi masikio, kumbe zilikuwa ni nyimbo za watani wao Chu. Xiang Yu na askari wake walistaajabu sana wakidhani Liu Bang keshauteka watani wake na kuwaleta mateka wenyeji wa huko kuimba. Nyimbo zilisababisha askari kukumbuka sana watani wao, nia ya kupigana ikaporomoka, nao wakatoroka katika usiku wenye giza tititii, askari kiasi cha laki moja mwishowe wakabaki mia kadha tu.
Kumbe, hii ilikuwa ni ujanja wa Liu Bang. Aliwashirikisha askari wake kuimba nyimbo za huzuni za sehemu ya Chu ili kuporomosha nia ya askari wa Xiang Yu.
Liu Bang alishinda kabisa katika vita hivyo, akaanzisha Enzi ya Han, na Xiang Yu akalazimika kujiua. Enzi ya Han ilijitokeza sana katika usitawi wa uchumi na utamaduni katika historia ya China.
Hadithi ya "Msichana Jirani Amchungulia Song Yu"
Katika historia ya China alikuwepo mwandishi mmoja mkubwa wa Dola la Chu, aliitwa Song Yu. Inasemekana kuwa huyo Song Yu alikuwa mwanamume mzuri kwa sura. Mwandishi huyo aliwahi kuandika makala moja ya kuvutia kwa jina la Msichana Jirani Amchugulia Song Yu.
Hadithi inasema hivi: Song Yu na Deng Tuzi wote walikuwa maofisa waliokuwa na uhusiano wa karibu na mfalme Chu. Deng Tuzi alimwonea wivu Song Yu kutokana na uhodari wake na mara kwa mara alimsema vibaya mbele ya mfalme. Alimwambia mfalme, "Song Yu ana sura ya kuvutia, ana elimu kubwa, lakini ni mwasherati. Kwa hiyo wewe mfalme kabisa usimruhusu aende kwenye ua wa nyuma mahali wanapoishi mahawara wako, ama sivyo atafanya matata."
Mfalme alimwita Song Yu mbele yake, na kumwuliza ili athibitishe kama ni kweli. Song Yu alisema, "Sura yangu nzuri nilizaliwa nayo, elimu yangu nimepata kutokana na kusoma sana, ama kuhusu uasherati sina kabisa."
Mfalme Chu alimwuliza, "Una ushahidi?"
Song Yu alijibu, "Warembo wanapatikana zaidi katika dola lako la Chu, na warembo hao wengi zaidi wanapatikana katika maskani yangu Chenli, na huko Chenli, mrembu maafuru ndio jirani yangu. Mrembo huyo akiwa urefu kidogo anapita kiasi, akiwa na ufupi kidogo atakuwa mfupi. Akijipodoa anaonekana mweupe kupita kiasi akipaka kidogo rangi nyekundu ataonekana mwekundu kupita kiasi. Meno yake, nywele zake na vitendo vyake, vyote vinavutia sana. Akitabasamu anawalewesha wanaume wote. Lakini mrembo huyo mara nyingi alinichungulia kwa miaka mitatu, na mimi nilikuwa baridi tu. Nawezaje kuwa mwanasherati? Ukweli ni kwamba mwasherati ndio Deng Tuzi."
Mfalme Chu alitaka kufahamishwa zaidi. Song Yu alisema, "Mke wa Deng Tuzi hana sura nzuri, lakini alimpenda mara moja alipomwona, na walizaa watoto watano." Baada ya kusikia hayo, mfalme Chu hakujua la kusema.
Song Yu aliandika maandishi mengi, lakini sasa vimebaki vitabu zaidi ya kumi tu. Kitabu chake maarufu ni "Utenzi wa Malaika".
|