Wanasayansi wa China ya Kale
Mwana-hisabati Zu Chongzhi
Uwiano kati ya mzingo wa duara na kipenyo ulikuwa tatizo kubwa na gumu katika hisabati. Katika China ya kale wanahisabati wengi walijitahidi kutafuta jawabu la uwiano huo, lakini hawakufanikiwa hadi karne ya tano ambapo Zu Chongzhi alipiga hatua kubwa katika utatuzi wa tatizo hilo.
Zu Chongzhi alikuwa ni mwana-hisabati mkubwa na mnajimu katika China ya kale. Alizaliwa mwaka 429 katika mji ambao sasa unaitwa Nanjing, watu wa familia yake walikuwa na elimu ya unajimu kizazi kwa kizazi. Kutokana na mazingira ya familia yake, tangu utotoni mwake Zu Chongzhi alipewa elimu ya hisabati na unajimu. Mwaka 464 alipokuwa na umri wa miaka 35 alianza kutafuta jawabu la uwiano kati ya mzingo wa duara na kipenyo.
Katika China ya kale, kutokana na mazoezi ya kazi watu walikuwa wanafahamu kwamba "mzingo wa duara ni mara tatu na zaidi kidogo kuliko kipenyo". Lakini "zaidi" kwa kiasi gani? Majibu yalikuwa tofauti. Zu Chongzhi alitopea katika hesabu zake na baadaye akifanya hesabu tena na tena na mwishowe akapata jawabu lake lenye namba saba mbele ya nukta yaani kati ya 3.1415926 na 3.1415927. Jawabu hilo ni sawa na jawabu walilolipata wana-hisabati wa nchi za nje baada ya miaka zaidi ya 1000. Ili kukumbuka mchango wake katika uwiano huo wana-hisabati wa nchi za nje wanaita alama ya uwiano kati ya mzingo wa duara na kipenyo kuwa "Uwiano wa Zu".
Licha ya mafanikio aliyopata kuhusu uwiano kati ya mzingo wa duara na kipenyo, naye pia alishirikiana na mwanawe kufanikiwa kupata kanuni ya kuhesabu ujazo wa tufe. Kanuni waliyotumia ilipewa na jina la "Cavalieri" katika nchi za Magharibi wakati Mtaliana Cavalieri alipogundua kanuni hiyo miaka elfu moja baadaye. Ili kuwakumbuka baba na mwana kanuni hiyo pia inaitwa "kanuni ya Zu" katika elimu ya hisabati.
Mafanikio ya Zu Chongzhi katika uwanja wa hisabati yameonesha kwa kiasi tu maendeleo ya hisabati katika China ya kale. Ukweli ni kwamba kabla ya karne ya 14 China ilikuwa imetangulia mbele katika hisabati. Kwa mfano, uhakiki wa pembetatu mraba katika hesabu za maumbo ulikuwa umeandikwa katika kitabu karne ya pili K.K. wazo la namba hasi na kanuni za kutoa na kuzidisha hesabu za namba hasi na chanya zilikuwa zimekwisha tolewa katika karne ya kwanza.
Mtaalamu wa dawa Li Shizhen
Tiba ya jadi ya Kichina ina historia ndefu, na walitokea wataalamu wengi wa dawa. Katika karne ya 16, Enzi ya Ming nchini China, alikuweko mtu mmoja mashuhuri wa dawa za mitishamba aliyeitwa Li Shizhen. Kitabu maarufu cha "Tiba na Dawa za Mitishamba" ndicho kilichoandikwa naye.
Li Shizhen (1518—1593) alizaliwa katika mkoa wa Hubei. Baba wa Li Shizhen alikuwa mganga, na Li Shizhen alipokuwa mtoto mara kwa mara alifuatana na baba yake kwenda milimani kutafuta dawa za mitishamba na kutengeneza dawa nyumbani. Lakini kutokana na kuwa hadhi ya waganga ilikuwa duni katika jamii, Li Shizhen aliamua kusoma ili apate nafasi ya ofisa.
Mwaka 1531, Li Shizhen alipokuwa na umri wa miaka 14 alifanikiwa katika mtihani wa wilaya, baadaye aliwahi kushiriki mitihani ya taifa kwa mara tatu lakini mara zote alishindwa. Tokea hapo alianza kujifunza udaktari kutoka kwa baba yake. Ili kujipatia elimu nyingi alikuwa mara kwa mara anazungumza na wavuvi, wawindaji, watema kuni na wakulima ili kukusanya tiba za kienyeji, na kwa kufanya majaribio alielewa kazi ya tiba ya kila aina ya mitishamba. Mwaka 1522, Li Shizhen alipokuwa na umri wa miaka 35 aliandika kitabu chake "Tiba na Dawa za Mitishamba".
Kitabu cha "Tiba na Dawa za Mitishamba" kimekusanya dawa za mitishamba aina 1892 na aina za matibabu zaidi ya elfu 11, na pia kuna picha za mimea ili watu watambue vilivyo mimea yenyewe.
Li Shizhen alitumia maisha yake yote katika ukusanyaji uzoefu wa matumizi ya dawa za mitishamba miongoni mwa watu wa China na aliandika kitabu cha "Tiba na Dawa za Mitishamba". Kitabu hicho kilichapwa mara kadhaa nchini Japan na pia kilitafsiriwa kwa lugha za Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani na Kilatini, kilienea duniani kote tokea karne ya 17.
Mnajimu Zhang Heng
Zhang Heng alizaliwa mkoani Henan, alipokuwa mtoto alipenda sana kujifunza na kuandika insha na alipokuwa na miaka 17 alifika mji wa Changan ambao uliwahi kuwa mji mkuu wa enzi nyingi katika historia ya China, alipokuwa huko alifanya uchunguzi wa kumbukumbu za kale, mila na desturi za wenyeji na hali ya uchumi ya jamii, kisha baadaye alichaguliwa kuwa ofisa katika mji wa Luoyang, ambao ulikuwa mji mkuu katika miaka yake. Lakini kutokana na hamu yake na unajimu kwa mara mbili aliacha kazi yake ya ofisa na alitumia miaka mitatu kufanya utafiti kuhusu falsafa, hisabati, unajimu na alipata elimu nyingi.
Katika miaka elfu mbili iliyopita, elimu kuhusu ulimwengu zilikuwa nyingi. Zhang He aliona kuwa ulimwengu ni kama yai, dunia ni kama kiini cha yai, mbingu ni kubwa na dunia ni ndogo, na aliona kuwa kabla kutengana kwa mbingu na ardhi, dunia ilikuwa ya mchanganyiko wa vitu vyote, na baada ya kutengana, vitu vyepesi vilipaa juu na vitu vizito vilibaki chini na kuwa dunia. Aliweza kueleza mwendo tofauti wa sayari kutokana na umbali tofauti na jua, sayansi ya zama hizi imethibitisha kuwa mwendo wa sayari unahusika na umbali na jua, kwa hiyo mtazamo wa Zhang He ulikuwa sawa.
Zhang He alibuni kifaa cha kupima tetemeko la ardhi, kifaa hicho ni cha mwanzo kabisa duniani. Mwaka 138 kifaa hicho kilitoa habari ya tetemeko la ardhi lililotokea katika mkoa wa Shanxi.
Zhang Heng licha ya kuwa mnajimu, naye pia alikuwa mwanafasihi na mchoraji. Kutokana na maandishi ya kale, Zhang Heng alituachia maandishi yake 32 kuhusu sayansi, falsafa na fasihi. Na kati ya makala hayo yako makala ya kueleza msimamo wake wa siasa, kuna makala inayoeleza matumaini ya binadamu kusafiri katika sayari nyingine na kuna makala inayoeleza mandhari ya miji.
|