Wengine
Daktari wa Ajabu Huatuo
Watu wanapougua wanakwenda kuonana na daktari wakitumai kupona, lakini kama ugonjwa ukiwa sugu,watu hao husema "laiti daktari ajabu Huatuo angekuwa hai". Huyu Huatuo alikuwa mganga wa miaka zaidi ya elfu mbili iliyopita, kutokana na uhodari wake watu walimmsifu kuwa ni "daktari wa ajabu".
Huatuo alikuwa ni mwenyeji wa mkoa wa Anhui, tarehe yake ya kuzaliwa haiwezi kuthibitishwa, lakini aliuawa kabla ya mwaka 208. Inasemekana kwamba Huatuo alikuwa na afya nzuri na alipokuwa na umri wa miaka mia moja afya yake bado ilikuwa njema. Kutokana na maandishi ya historia, alikuwa mganga wa kienyeji na alikuwa na nafasi nyingi za kuwa ofisa, lakini alikataa. Jemadari mkubwa Cao Cao (155-220) alikuwa na ugonjwa wa kuumwa na kichwa kwa muda mrefu, alimwomba Huatuo amtibu, muda si mrefu Cao Cao alipona kabisa. Tokea hapo Cao Cao alimlazimisha Huatuo aishi naye na kutunza afya yake. Lakini siku chache baadaye Huatuo alirudi nyumbani kwa kisingizio kuwa mkewe alikuwa anaumwa. Ingawa Cao Cao alimhimiza mara kadhaa arudi kwake, lakini Huatuo hakurudi. Cao Cao aliamua kumtia gerezani na baada ya muda alimwua.
Huatuo alikuwa na elimu nyingi za tiba ambazo zinahusika na magonjwa ya maambukizi, minyoo, wanawake na watoto, mfumo wa kupumua na ngozi, na hasa elimu ya kufa ganzi kwa mwili mzima na upasuaji.
Huatuo alikuwa mtu anayependwa sana na watu, kwa kiasi fulani uhodari wake katika matibabu umeonesha maendeleo ya tiba katika miaka elfu mbili iliyopita nchini China. Huatuo alikuwa mmoja wa watu waliotangulia kutumia dawa za ganzi duniani.
Huatuo alikuwa hodari wa kufanya upasuaji. Aliwahi kumfanyia upasuaji msichana mmoja mwenye umri wa miaka 20 ambaye alikuwa na kidonda kwenye goti kwa miaka minane. Huatuo alifunika dawa ya unga kwenye kidonda baada ya kutoa kipande kimoja cha mfupa, msichana huyo alipona baada ya siku saba. Watu wa leo wanaona kuwa kipande cha mfupa alichotoa kilikuwa ni kipande kilichokufa. Kulikuwa na mgonjwa mwingine mzee ambaye alikwenda kumwona, baada ya kuchunguza ugonjwa wake Huatuo alimwambia kuwa ugonjwa wake umekuwa mkubwa na anaweza tu kufayiwa upasuaji wa tumbo, lakini hata hivyo, anaweza kuishi kwa miaka 10 hivi, na bila ya upasuaji pia ataishi muda huo huo, kwa hiyo ni afadhali aache upasuaji. Lakini kutokana na usumbufu wa ugonjwa wenyewe alimwomba Huatuo amfanyie upasuaji, maumivu yalipungua lakini mzee huyo hakuishi zaidi ya miaka 10.
Huatuo pia alikuwa hodari wa kugundua ugonjwa kwa kuangalia sura ya mtu. Siku moja alipokuwa katika baa, aliwaona watu kadhaa wakinywa pombe, aligundua mmoja kati yao alikuwa na ugonjwa mkubwa, alimwambia asinywe zaidi na kurudi nyumbani haraka. Mtu huyo alipokuwa njiani alianguka kutoka kwenye gari na baada ya kufika nyumbani siku chache alikufa.
Watu wa leo wanatilia maanani sana mazoezi ya kuimarisha afya. Miaka elfu mbili iliyopita Huatuo alivuni mazoezi mepesi ili kuimarisha afya, "mchezo wa wanyama wa aina tano" ambayo yalikuwa ni mazoezi mepesi kwa vitendo vya aina tano za wanyama: chui, swala, dubu, nyani na ndege. Watu wanaofanya mchezo huo wananyoosha mishipa, kuongeza mzunguko wa damu, kuongeza uwezo wa kujikinga na maradhi. Wanafunzi wa Huatuo walikuwa wengi, na kati yao watatu walikuwa maarufu ambao walitoa mchango mkubwa katika tiba ya Kichina. Baada ya Huatuo kufariki, watu walimjengea mahekalu mengi kumkumbuka katika mahali alipowahi kutoa matibabu.
Chen Sheng na Wu Guang Wafanya Uasi
Chen Sheng na Wu Guang walikuwa ni viongozi mashuhuri wa uasi wa wakulima, uasi ulioongozwa nao ulikuwa mkubwa na wa kwanza katika historia ya China ambao ulizuka katika karne ya tatu mwishoni mwa Enzi ya Qin.
Mwaka 210 mfalme wa kwanza wa Enzi ya Qin alifariki, mtoto wake Hu Hai alirithi kiti cha ufalme.
Mfalme Hu Hai alikuwa mpumbavu, chini ya utawala wake raia waliishi vibaya na kutozwa kodi nyingi.
Mwaka 209 mfalme Hu Hai aliamuru wakulima 900 kwenda kulinda mji wa Yu Yang (wilaya ya Miyun karibu na Beijing).
Chen Sheng aliteuliwa kuwa kiongozi wa wakulima hao. Lakini walipokuwa njiani walizuiliwa na mvua kubwa, walikuwa hawawezi kufika mji wa Yu Yang kwa wakati uliopangwa. Kutokana sheria, wangechelewa wote wangeuawa. Chen Sheng na Wu Guang aliwaambia wakulima kuwa ni afadhali kufanya uasi kuliko kuuawa. Wakulima hao waliwachagua Cheng Sheng kuwa jemadari na Wu Guang kuwa msaidizi wake na kuunda jeshi la kwanza la wakulima katika historia ya China.
Katika muda mfupi jeshi hilo liliteka miji sita mikuu ya wilaya na popote jeshi hilo lilipopita raia waliliunga mkono na kujiunga nalo. Jeshi hilo lilikuwa na askari wengi siku hadi siku na kuwa jeshi kubwa lenye askari laki kadhaa.
Jeshi hilo liligawanyika katika sehemu tatu, wakati jeshi hilo lilipokuwa na askari laki kadhaa walianza kushambulia mji mkuu wa Enzi ya Qin.
Mfalme Hu Hai alishikwa na hofu wakati jeshi la Cheng Sheng na Wu Guang lilipokaribia mji mkuu, alihamisha askari laki kadhaa kuja mji mkuu na kushirikiana na jeshi la kifalme kupambana na jeshi la uasi kutoka mbele na nyuma, na Wu Guang aliuawa. Mwezi Desemba mwaka 209 Cheng Sheng pia aliuawa katika pambano kali na jeshi la Enzi ya Qin.
Ingawa viongozi wa uasi huo Chen Sheng na Wu Guang wate waliuawa, lakini askari wao walijiunga na jeshi jingine lililoongozwa na Xiang Yu na Liu Bang na kuendelea kupambana na jeshi la Enzi ya Qin. Mwaka 206 Enzi ya Qin iliangushwa na jeshi la uasi la wakulima.
Wang Zhaojun
Katika historia ya kale ya China migogoro kati ya kabila la Wahan na makabila mengine ikitokea, ilikuwa inatatuliwa kwa vita, lakini pia iliwahi kutokea njia nyingine ya kutatua migogoro kati ya makabila, nayo ni kumwoza binti wa mfalme kwenye kabila jingine na kupata urafiki na kabila hilo.
Karne ya kwanza ilikuwa ni kipindi cha Enzi ya Han. Kabila la Waxiongnu lililokuwa katika sehemu ya kusini magharibi ya China lilikumbwa na migogoro kutokana na watemi kugombea madaraka. Wakati huo mtemi mmoja aliyejulikana kwa jina la Han Xie alikuja kwa mfalme wa Enzi ya Han kuomba msaada. Mfalme wa Enzi ya Han alimkaribisha kwa ukarimu na alimsaidia kwa nafaka nyingi, na baada ya kurudi alifanikiwa kupata utawala wa kabila la Waxiongnu.
Ili kupata urafiki wa daima mwaka 33 K.K. Han Xie kwa mara nyingine alikuja mji mkuu kuonana na mfalme na kuomba amwoe binti yake. Mfalme wa Enzi ya Han mara alikubali ombi lake. Mfalme aliwaambia vijakazi wake "kati yenu atakayekubali kuwa mke wa mfalme wa kabila la Xiongnu atakuwa binti yangu."
Kulikuwa na msichana mmoja mwenye sura nzuri na werevu, aliitwa Wang Zhaojun. Msichana huyo alikuwa mwerevu na kupenda kusoma, aliweza kutunga mashairi na kupiga kinanda, alikubali kuolewa na mfalme wa kabila la Waxiongnu kwa ajili ya urafiki wa makabila mawili.
Kwa kusindikizwa na maofisa wa Enzi ya Han Wang Zhaojun alisafiri mbali na kufika sehemu ya kabila la Waxiongnu. Mwanzoni maisha ya kabila hilo yalikuwa magumu kwake lakini baada ya muda alizoea na kuishi vema na Waxiongnu.
Yanzi
Katika kitabu maarufu cha "Rekodi ya Historia" kilichoandikwa na Simaqian, walielezwa wanadiplomasia kadhaa mashuhuri, mmoja wao alikuwa Yan Zi aliyeishi katika karne ya sita.
Kipindi kati ya mwaka 770 K.K. hadi 481 K.K. katika historia ya China kinaitwa kipindi cha Spring na Autumn. Wakati huo utawala wa Enzi ya Zhou ulikuwa umeanza kudhoofika, madola yaliyo chini ya himaya kake aylikuwa yanapigana kugombea ardhi na mwishowe yalitokea madola kadhaa yenye nguvu kubwa, na pia walitokea wanasiasa mashuhuri. Yan Zi alikukwa mmojawapo.
Kwa mujibu wa maandishi ya historia, kimo cha Yan Zi kilikuwa mita moja na sentimita arobaini tu, lakini elimu yake ilikuwa pana na alikukwa mtu mwerevu na mcheshi.
Yan Zi aliwahi kwenda kwenye madola mengine mara nyingi akiwa mjumbe wa Dola la Qi, kati ya safari zake, hadithi katika safari mbili alipokuwa katika Dola la Chu zilikuwa maarufu. Mfalme wa Dola la Chu alijua yeye ni mbilikimo, alitaka kumdhihaki. Katika safari ya kwanza alipokuwa kwenye Dola la Chu mfalme aliamuru watu wake wamwingize mjini kutoka kwenye kilango kidogo pembeni mwa lango kubwa. Yan Zi alielewa mfalme Chu akitaka kumdhalilisha, alikataa kabisa na kusema, "Nikifika kwenye dola la mbwa nitaingia kwenye kilango cha mbwa, sasa nimekuja kwenye dola la Chu nikiwa mjumbe wa dola, niwezaje kuingia mjini kupitia kilango cha mbwa!" Walinzi walikuwa hawana budi ila kumpitisha kutoka kwneye mlango mkubwa. Mfalme wa Chu alipokutana na Yan Zi alimwuliza kwa makusudi: "Kwani dola la Qi linashindwa kumchagua mtu mwingine aje kwenye dola la Chu badala yako?" Yan Zi alimjibu kwa utaratibu, "Dola la Qi lina mazoea ya kutuma wajumbe wenye maadili mema kwenye madola yenye maadili mema, na kutuma wajumbe wapumbavu kwenye madola ya wapumbavu. Mimi ni mpumbavu kabisa kati ya wajumbe wote, ndio maana nimetumwa hapa."
Safari ya pili alipokwenda kwenye dola la Chu, mfalme wa Chu alitaka kumwaibisha Yan Zi hadharani. Wakati mfalme wa Chu alipomkaribisha kwenye chakula, ghafla askari wawili walileta mtu mmoja aliyefungwa kamba mbele ya mfalme, wakisema mtu huyo ni mtu wa dola la Qi, aliiba mali yao. Mfalme alimtupia macho Yan Zi akisema, "Kwani watu wa dola la Qi walizaliwa na wezi?" Mwerevu Yan Zi mara alikumbuka mto Huaihe uliokuwa mpaka wa madola mawili, alitumia michungwa kumjibu mfalme: "Machungwa yaliyopatikana kwenye ukingo wa kusini wa mto ni matamu, lakini yaliyoko kwenye ukingo wa kaskazini ni machungu, sababu udongo wenyewe ni tofauti. Watu wanaoishi katika dola la Qi hawaibi, lakini wanaoishi katika dola la Chu wana tabia ya kuiba, kwani ardhi ya Chu inalea wizi?"
Mambo kama hayo yalikuwa mengi ambayo Yan Zi aliwashinda wapinzani wake waliojaribu kumdhihaki na kuharibu heshima ya dola lake. Alikuwa mwanadiplomasia mashuhuri katika hitoria ya China.
Su Wu
Kuna hadithi moja kuhusu Su Wu nchini China, nayo ni hadithi ya "Mchugaji Kondoo Su Wu".
Su Wu alikuwa mtu wa Enzi ya Han katika karne ya kwanza. Ili kuweka urafiki na kabila la Waxiongnu lililoko katika sehemu ya kaskazini magharibi ya China Su Wu alitumwa na mfalme kwenda kwa Waxiongnu akiwa na zawadi nyingi, na baada ya kumaliza kazi aliyopewa na mfalme tayari kurudi nyumbani, alibakizwa huko kwa kusingiziwa kuwa alishiriki katika mgogoro uliotokea ndani ya kabila la hilo, na alilazimishwa kuhaini Enzi ya Han.
Mwanzoni Su Wu alishawishiwa kuwa ofisa kwa mshahara mkubwa, lakini Su Wu alikataa, baadaye aliadhibiwa na Xiongnu kwa kutompa chakula na maji. Siku zilikwenda, Su Wu alifungiwa ndani ya shimo, akiwa na kiu alikula theluji, akiwa na njaa alikula koti lake ya ngozi. Mwishowe aliachiwa huru kutokana na nia yake thabiti ya kutohaini Enzi yake ya Han. Lakini hakuruhusiwa kurudi nyumbani bali alifukuziwa mbali kwenye sehemu ya baridi Siberia kuchunga kondoo, aliambiwa kuwa ataruhusiwa kurudi nyumbani pindi kondoo dume akizaa.
Su Wu alifukuziwa kando ya ziwa la Baikal na kuchunga kondoo kwa miaka nenda miaka rudi, nywele zikawa na mvi na ndevu zikawa nyeupe.
Aliishi kwenye ziwa la Baikal miaka 19. katika muda wa miaka zaidi ya kumi mfalme aliyemfukuzia alikufa, na mfalme wake wa Enzi ya Han pia alifariki, aliyeathiri kiti cha ufalme alikuwa mtoto wake. Wakati huo mfalme mpya alitekeleza sera mpya na mfalme huyo mpya alimtuma mtu kumrudisha Su Wu nyumbani.
Su Wu alikaribishwa kwa shangwe na wananchi katika mji mkuu wa Enzi ya Han, maofisa wa serikali walimheshimu kutokana na uzalendo wake.
Guan Zhong na Bao Shuya
Guan Zhong na Bao Shuya walikuwa wanasiasa katika karne ya saba na walikuwa marafiki. Guan Zhong alikuwa maskini na Bao Shuya alikuwa tajiri, na hao wawili walifahamiana na kuamiana na hata walishirikiana kufanya biashara, kutokana na umaskini Guan Zhong alitoa raslimali chache, lakini walipogawana faida alipewa pesa nyingi zaidi kuliko Bao Shuya ili aweze kuwatunza jamaa zake.
Baadaye watu hao wawili wote walishiriki katika mambo ya siasa, ambayo wote wawili waliwafundisha watoto wawili wa mfalme wa Dola la Qi katika madola mengine tofauti. Baadaye uasi ulitokea katika Dola la Qi, mfalme aliuawa. Baada ya kusikia habari kuhusu kifo cha baba yao, watoto wote wawili walikimbilia nyumbani dola la Qi ili kurithi kiti cha ufalme. Njiani mtoto Qi Huan Gong na ndugu yake walikutana. Guan Zhong alimfyatulia mshale Qi Huan Gong ili ndugu wa Qi Huan Gong apate nafasi ya ufalme. Mshale huo ulimkwaruza tu Qi Huan Gong kiunoni, lakini alijidai kuwa amepigwa na kuanguka kama amekufa. Ndugu yake alidhani amekwisha kufa, na kiti cha utawala hakika kitakuwa chake, akapunguza mwendo wa safari. Lakini Qi Huan Gong hakuumia, aliharakisha safari yake usiku na mchana na alifika nchini mapema kwa siku sita kuliko ndugu yake, mawaziri walimwunga mkono awe mtawala wa dola la Qi.
Baada ya kuwa mfalme wa dola la Qi, Qi Huan Gong aliwapokea watu wengi wenye busara hata hakuwa na kinyongo na yule Guan Zhong aliyemfyatulia mshale na kumteua kuwa waziri wa dola lake.
Guan Zhong alikuwa waziri kwa miaka mingi na alitoa mchango mkubwa kwa ajili ya kuimarisha dola lake.
Bao Shuya alipofariki, Guan Zhong alilia sana mbele ya kaburi lake, alisema, "nilizaliwa na mama yangu lakini aliyenielewa ni Bao Shuya!"
Mfalme Chu Zhuangwang
China ni nchi yenye uvumilivu mkubwa, watu wanaona kuwa uvumilivu unaweza kuyeyusha fitina. Hadithi ya "kuondoa kishungi kwenye kofia" inawafundisha watu wenye uvumilivu watalipwa mema.
Katika kipindi cha Spring na Autumn, karne ya saba, kulikuwa na madola mengi kwa wakati mmoja. Mfalme wa Dola la Chu, Chu Zhuangwang alikuwa mwerevu, na chini ya utawala wake dola hilo liliimarika sana.
Siku moja, mfalme Chu Zhuangwang aliwakaribisha maofisa kwenye chakula na kuburudika kwa nyimbo na ngoma. Giza lilikuwa linaingia, mfalme aliwaambia kuwasha mishumaa. Watu walikula na kunywa kwa furaha.
Ghafla upepo ulivuma, mishumaa ilizimika, wakati huo mke wa mfalme alisikia kuna mkono mmoja ulimshika shika, mke wa mfalme alighadhabika akang'oa kishungi cha kofia ya yule aliyemtomasa, akaenda kwa mfalme na kumnong'oneza, "washa mishumaa na kuona kama nani alikosa kishungi kwenye kufia na kumwadhibu." Lakini mfalme alipaaza sauti na kusema, "Msiwashe mishumaa, ni furaha pekee kunywa pombe gizani." Baadaye mfalme aliwauliza maofisa, "Mnafurahia chakula?" wote walijibu "Ndio!" Mfalme aliendelea, "kama kweli mnafurahia chakula, basi ng'oeni vishungi kwenye kofia zenu!" wote waling'oa. Kisha mfalme aliwaambia wawashe mishumaa. Maofisa walipoona kofia zote zilibadilika sura wote walicheka, waliendelea kula na kunywa mpaka kupambazuka.
Baada ya kurudi kwenye kasri la kifalme, mke wa mfalme alihasirika sana alisema, "Wewe mfalme unawadekeza sana maofisa, hivyo utashindwa kuwatawala." Mfalme alicheka na kusema, "Nawakaribisha maofisa kwenye chakula kwa lengo la kuwafurahisha. Ni jambo la kawaida kwa mtu akizidiwa na pombe na kufanya kitendo kisicho cha kawaida. Nikimwadhibu ofisa huyo kwa jambo hilo dogo nitaharibu furaha na kuwafedhehesha maofisa. Hilo silo lengo la kuwaandalia chakula."
Baadaye dola la Chu lilishambulia dola la Zheng. Kulikuwa na jemadari mmoja aliyekuwa shupavu mkubwa katika mapambano dhidi ya askari wa dola la Chu, na alifanya mashambulizi mpaka karibu na mji mkuu wa dola la Chu. Jemadari huyo ndiye aliyemshikashika mke wa mfalme wa dola la Chu.
Hadithi ya "kuondoa kishungi kofiani" inawaambia watu wawe wavumilivu.
Yu Boya na Zhong Ziqi
Katika kipindi cha Spring na Autumn, katika dola la Chu kulikuwa mwanamuziki mmoja ajulikanaye kwa jina la Yu Boya. Huyu Yu Boya alikuwa mwerevu toka alipokuwa mtoto, na alipenda sana muziki. Baadaye alijifunza kupiga kinanda kwa mwalimu wake Lian Cheng.
Baada ya kujifunza kwa miaka mitatu, alikuwa mwanamuziki mashuhuri, lakini Yu Boya hakuridhika, aliona kiwango chake kilikuwa bado si kikubwa kileleni. Mwalimu wake Lian Cheng alifahamu Yu Boya aliyofikiri moyoni, alimwambia kwamba atamwongoza kwa mwalimu wake ambaye ufahamu wake wa muziki ni wa juu sana. Yu Boya alikubali.
Baada ya kutayarisha chakula cha kutosha hao wawili walipanda mashua na kufika kwenye mlima wa Penglai. Mwalimu wake Lian Cheng alimwambaia, "Nisubiri hapa, nakwenda kumtafuta mwalimu wangu." kisha akaondoka. Siku nyingi zilipita, lakini mwalimu wake Lian Cheng hakurudi. Boya aliangalia bahari isiyo na mwisho na misitu mlimani alihuzunika sana, kwa kusukumwa na moyo alipiga kinanda chake. Muziki ulijaa huzuni, lakini tokea hapo alikuwa mwanamuziki mkubwa. Kwa kweli mwalimu wake Lian Cheng alifanya hivyo kwa makusudi ili Yu Boya apate hisia za kweli moyoni.
Kuishi katika kisiwa kilichojitenga, usiku na mchana kitu alichoona ni bahari, ndege na misitu, siku nenda siku rudi hisia zake zilibadilika na kuelewa zaidi muziki, alitunga muziki maarufu uliowagusa mioyo wasikilizaji. Yu Boya alikuwa mwanamuziki mkubwa, lakini watu waliofahamu muziki wake walikuwa wachache.
Siku moja Yu Boya alisafiri kwa mashua, alipofika karibu na mlima, mvua kubwa ilinyesha, aliegesha mashua yake kukimbia mvua. sauti ya mvua na mandhari nzuri ya ukungu uliokuwa kwenye uso wa mto ilimsisimua, alipata msukumo wa kupiga kinanda. Muziki alioupiga ulikuwa ni sauti kutoka moyoni mwake. Kulikuwa na mtu mmoja kwenye ukingo wa mto akisikiliza muziki wake, mtu huyo aliitwa Zhong Ziqi.
Baada ya kusalimiana Yu Boya alimkaribisha Zhong Ziqi ndani ya mashua yake na kumpigia muziki. Zhong Ziqi alisikiliza kwa msisimko. Yu Boya alisema, "Katika dunia hii ni wewe tu unayefahamu sauti ya moyoni mwangu, wewe ndiye mwelewa sauti yangu!" Hao wawili walikuwa ndugu wa kuchanjiana.
Yu Boya aliahidiana na Zhong Ziqi kuwa watakutana baadaye. Siku moja Yu Boya alikwenda kwa Zhong Ziqi kama walivyoahidiana, lakini wakati huo Zhong Ziqi alikuwa amefariki. Baada ya kusikia habari hiyo Yu Boya alikimbilia kwenye kaburi la Zhong Ziqi na kumpigia muziki kwa huzuni kubwa, kisha alisimama na kuvunja kabisa kinanda chake. Tokea hapo Yu Boya aliacha kabisa kupiga kinanda.
Sun Wu
Sun Wu aliyeishi katika karne ya sita K.K. ni mtu maarufu sana nchini na duniani, kitabu chake cha "Mbinu za Kivita za Sun Zi" kilikuwa ni maandishi makubwa ya kivita katika China ya kale.
Sun Wu alizaliwa mwaka 551 K.K. kilikuwa ni kipindi cha Spring na Autumn katika historia ya China. Alikuwa mtu wa dola la Qi, alipokuwa na umri wa miaka 19 alikwenda dola la Wu, na katika kiunga cha mji mkuu wa dola la Wu (mji wa Suzhou wa leo) aliandika kitabu chake cha mbinu za kivita na kumpa mfalme wa dola la Wu. Mfalme alifurahi sana, lakini hakujua kama mbinu zenyewe zinaweza kutumika, alimtaka Sun Wu afanye mazoezi kwa masuria waliokuwa ndani ya kasri la kifalme.
Sun Wu aliwagawa masuria 180 kwa vikundi viwili na kuwateua wawili waliopendwa sana na mfalme kuwa viongozi wa vikundi viwili, kimoja kulia na kingine kushoto, na kufanya mazoezi.
Sun Wu alisimama kwenye jukwaa na kuwafahamisha mpango wa mazoezi yake. Sun Wu alipiga ngoma ya kuanzisha mazoezi. Lakini masuria walikuwa kama hawajasikia mdundo wa ngoma, bali walichekacheka na kuchezacheza, safu zao zilivurugika, ingawa Sun Wu aliwaasa mara kadhaa, lakini haikusaidia kitu. Kutokana na hali hiyo, Sun Wu aliamuru kuwaua viongozi wawili.
Mfalme alipoona kweli Sun Wu alitaka kuwaua wapendwa wake wawili alimsihi awaache. Lakini Sun Wu hakubali ombi la mfalme, aliwaua. Kisha akaanza tena mazoezi, safari hii masuria walifanya mazoezi kwa makini, walipiga hatua mbele na nyuma, waliviringika na kutambaa kifudi fudi, kila mmoja alifanya vizuri. Kuona hali hiyo mfalme alifurahi, akamteua Sun Wu kuwa jemadari.
Chini ya uongozi wa Sun Wu jeshi la dola la Wu lilikuwa hodari sana na lilipata ushindi kila mara katika vita vya kupigana na madola mengine.
Mwaka 482 K.K. mfalme wa dola la Wu alikuwa mbabe kati ya madola yote kutokana na mbinu zilizoandaliwa na Sun Wu.
Kutokana na ushindi, mfalme alikuwa anavimba kichwa. Kwa kuona jinsi mfalme alivyokuwa, Sun Wu aliondoka na kuishi mbali na mfalme milimani.
Kitabu cha "Mbinu za Kivita za Sun Zi" ingawa kilikuwa na maneno elfu 6 katika makala 13, lakini kilionesha kikamilifu mbinu zake za kivita. Kitabu hicho kilisifiwa na watu wa baadaye kuwa ni "kitabu cha kwanza duniani kuhusu mbinu za kivita", na kilitumika sana katika mambo ya kijeshi, kisiasa na uchumi.
Qi Jiguang
Katika mlima wa Yu Shan mkoani Fujian kuna hekalu moja lililowekwa sanamu ya Qi Jiguang, watalii wanapofika huko hawakosi kwenda kutoa heshima kwake kutokana na uzalendo wake na mchango wake katika mapambano dhidi ya wavamizi.
Qi Jiguang alikuwa jemadari katika Enzi ya Ming, alizaliwa katika ukoo wa jemadari. Kwa kuathiriwa na baba yake, Qi Jiguang toka alipokuwa mtoto alipenda sana mambo ya kijeshi na kuwa na nia ya kuwa mwanajeshi hodari. Wakati huo wavamizi wa Japan walikuwa mara kwa mara wanashambulia China. Alipokuwa na umri wa miaka 17 alirithi wadhifa wa baba yake na kuanza maisha yake ya kijeshi. Alipokuwa tu jemadari tatizo lililomkabili lilikuwa ni mashambulizi ya Japan.
Tokea mwishoni mwa Enzi ya Yuan na mwanzoni mwa Enzi ya Ming maharamia wa Japan mara kwa mara walikuwa wakipora mali na kuua watu kwenye mwambao. Katika nusu ya pili ya karne ya 15 maharamia wa Japan walikuwa wanashirikiana na wafanyabiashara wabaya wa China kufanya uovu.
Mwaka 1555 Qi Jiguang alitumwa kwenye mwambao, aliunda jeshi la wakulima na wachimba migodi. Walitumia mishale na mikuki kuwaua baada ya kuwatega mitegoni.
Jeshi lake lilikuwa na askari elfu 4, na baada ya kuwafundisha na kuwafahamisha askari mbinu za kivita, jeshi hilo lilikuwa hodari sana, na kutokana na kuwa na nidhamu kali liliungwa mkono na wananchi.
Mwaka 1561 maharamia wa Japan elfu kadhaa na mashua zaidi ya mia walifanya mashambulizi katika sehemu ya Taizhou mkoani Zhejiang. Qi Jiguang kwa haraka aliwaongoza askari wake kupambana nao na kuwaangamiza maharamia wote.
Kutokana na juhudi za Qi Jiguang na majemadari wengine, maharamia wa Japan walitoweka, mikoa ya Zhejiang na Fujian ilikuwa tulivu, na uchumi ulistawi. Qi Jiguang alitoa mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya maharamia wa Japan na alisifiwa sana na watu wa China.
|