Mila
Siku ya Mwisho ya Majira ya Baridi
"Siku ya Mwisho ya Majira ya Baridi" ni moja katika vipindi 24 vya majira katika kalenda ya Kichina. Mapema miaka elfu mbili na saba iliyopita watu wa China ya kale walikuwa na siku hiyo.
"Siku ya mwisho ya majira ya baridi" haimaanishi kwamba katika siku hiyo jotoridi ni chini kabisa, bali inamaanisha dunia imefika mahali fulani katika njia yake ya kulizunguka jua. Katika siku hiyo, mchana ni mfupi kabisa katika mwaka mzima, na baada ya siku hiyo muda wa mchana unakuwa mrefu siku hadi siku. Katika China ya kale wafalme walikuwa wanafanya sherehe kwa siku tano na kufanya tambiko katika hekalu la Tiantan mjini Beijing.
"Siku ya Mwisho ya Majira ya Baridi" watu pia wanaita "mwanzo wa siku tisa tisa". Watu wanaanza kuhesabu siku tisa tisa kuanzia siku hiyo, jumla kuna "siku tisa tisa" tisa, yaani siku 81, na majira ya Spring huanza kabla ya "siku tisa tisa" ya sita. Miongoni mwa wenyeji baadhi ya watu wana desturi ya kupaka rangi kwenye maua, jumla maua 81, kila baada ya siku moja kupita wanatia rangi kwenye ua moja mpaka maua yote 81 yapakwe rangi ambapo majira ya Spring yanakuwa yamefika na jitoridi linakuwa la uvuguvugu.
Siku Safi na Angavu
Siku Safi ya Angavu iko katika mwanzoni mwa majira ya Spring.
Siku Safi na Angavu ni moja katika vipindi vya majira 24 katika kalenda ya Kichina, siku hiyo iko mwanzoni mwa mwezi Aprili. Katika siku hiyo watu huenda kutembelea viungani au kwenda kusafisha makaburi kuwakumbuka marehemu.
Katika siku kabla na baada ya Siku Safi na Angavu, watu huwa wanakwenda kwenye makaburi kutoa heshima kwa wazee waliokufa. Kwenye makaburi wanaondoa majani, wanachoma karatasi zilizokatwa kama noti na kupiga magoti au kusimama kimya kuwakumbuka marehemu kwa dakika chache.
Kuwakumbuka marehemu katika siku hiyo kulianzia Enzi ya Han (206 K.K.--220 K,K.), na katika enzi za Ming na Qing (1368—1911) shughuli za kusafisha makaburi zilipamba moto, na baadhi ya watu licha ya kusafisha makaburi, wnapika vyakula kuweka mbele ya makaburi.
Kusafisha makaburi kumekuwa mila ya Wachina katika siku hiyo na kuendelea mpaka leo, ila tu licha ya kuwakumbuka marehemu pia wanakwenda kwenye makaburi ya mashujaa na kuweka mashada ya maua kuonesha heshima zao.
Kwa sababu kipindi cha Siku Safi na Angavu ni mwanzo wa majira ya Spring, watu hufanya utalii katika viunga vya miji kuburudika mazingira ya kuchipua kwa majani na kupunga upepo mzuri.
Katika China ya kale wanawake walikuwa na desturi ya kuchuma mboga msituni na kutengeneza Jiaozi na kuchomeka maua kichwani.
Katika kipindi cha Siku Safi na Angavu watu pia wana desturi ya kurusha tiara, kucheza mchezo wa kuvutana kwa kamba na kubembea.
Lakini kwa nini siku hiyo inaitwa Siku Safi na Angavu? Kwa sababu katika kipindi hicho majira ya Spring imeanza, mbingu ni safi na jua si kali, majani yameanza kuchipuka, na watu wameanza kupanda mbegu na miti. Katika China ya kale watu walikuwa na desturi ya kupanda miti katika sehemu za makazi yao.
Masimulizi kuhusu Mungu wa Jiko
Katika miaka zaidi ya elfu mbili, Wachina wamekuwa na mila ya kufanya tambiko kwa mungu wa jiko katika tarehe 23 mwezi Februari kwa kalenda ya Kichina.
Mungu wa Jiko alitokea katika hadithi za mapokeo, yeye ni ofisa aliyetumwa na mungu kwenye kila familia, na kila mwaka anakwenda kwa mungu kutoa ripoti. Kwa hiyo watu humwabudu sana na kwa ajili ya kumfurahisha, kila mwaka katika siku hiyo watu hufanya tambiko.
Zamani za kale kulikuwa na tajiri mmoja aliyeitwa Zhang Sheng, mke wake Ding Xiang alikuwa kisura na mwenye akili. Mwanzoni waliishi kwa furaha sana.
Siku moja tajiri huyo alimkuta msichana mmoja mrembo aliyeitwa Hai Tang, mara walianza kupendana. Muda si mrefu baadaye tajiri alimwoa na kumleta nyumbani. Msichana Hai Tang alipoona mke wa tajiri alikuwa mrembo na ni mke halali alikuwa na wivu, alimtaka tajiri kumfukuza.
Tokea hapo Zhang Sheng na mkewe waliishi maisha ya anasa, na kabla ya kutimia miaka miwili, walifuja mali zote na wote walikuwa maskini. Kwa kuona kuwa Zhang Sheng amekuwa maskini, Hai Tang alimwacha na kuolewa na mwengine. Zhang Sheng alibaki peke yake, kwa kulazimika na umaskini alibadilika kuwa ombaomba. Siku moja theluji ilikuwa kubwa, Zhang Sheng alisikia baridi na njaa, alianguka mbele ya mlango wa nyumba ya tajiri mmoja. Mtumishi alipotoka nyumbani alimwona na kumsaidia kumpeleka jikoni. Dakika chache baadaye mwenye nyumba alikuja kumwangalia, Zhang Sheng alishtuka alipofahamu kuwa huyo mwenye nyumba ndiye aliyekuwa mkewe Ding Xiang. Kwa kuona aibu alijipenyeza ndani ya tundu la kijiko cha kuwashia kuni. Ding Xiang alipoingia jikoni hakumwona yeyote, aliona ajabu, kisha baadaye aligundua kitu fulani kilichoziba tundu la kijiko, alikivuta kitu hicho akatambua ni mtu aliyekuwa mumewe ambaye amekwisha kufa kutokana na kuungua na moto. Siku chache baadaye Ding Xiang alikufa kutokana na huzuni. Mungu alipopata habari hiyo aliona kuwa Zhang Sheng ni mtu mwema, alijuta makosa yake, alimteua kuwa mungu wa jiko. Watu walimwabudu mungu huyo wa jiko na mkewe pia, na kuweka sanamu zao ndani ya jiko.
Ili mungu awasemee wema mbele ya mungu, watu hupika sukari ya kimea iliyonatanata kwa nafaka, ili mungu wa jiko anapokula sukari hiyo ulimi utakuwa ladha tamu na kusema maneno mazuri juu ya familia aliyokaa. ?
Mila ya Ndoa
China ina historia ndefu na ni nchi kubwa. Kuhusu mila ya ndoa ingawa inabadilika tokea zama za kale hadi leo, lakini sherehe ya ndoa ambayo hufanywa kwa shangwe na furaha, haikubadilika.
Katika China ya kale, ndoa huwa na hatua kadhaa mfululizo zikiwa ni pamoja na kutoa zawadi ya kuomba ndoa, kutoa mahari ya ndoa na kumpokea Bi. harusi. Kijana akimpenda msichana fulani humwomba mshenga kwenda nyumbani kwa msichana, wakati huo upande wa kijana utampa zawadi mshenga na kutoa zawadi kwa wazazi wa msichana. Kama pande mbili kimsingi zimekubaliana, basi wazazi wa upande wa kijana huchagua siku kwenda kwa familia ya msichana ili kuelewa hali ya upande wa msichana kama uchumi, maadili, tabia ya msichana na sura. Kadhalika, wazazi wa upande wa msichana pia wanakuja nyumbani kwa familia ya kijana kumfahamu kijana atakayekuwa mkwe. Lakini katika zama za kale, msichana hakuruhusiwa kwenda kuonana na kijana atakayekuwa mume wake. Hali ilivyo sasa ni kinyume na ya zamani, kwamba wasichana wengi huongozana na wazazi wao kwenda nyumbani kwa nyumbani kwa wachumba wao kufahamu hali ya familia na watu wenyewe, na kama wakikubali kubakizwa kula nyumbani kwao, inamaanisha kuwa wamekubali ndoa yao.
Kutoa mahari ni hatua muhimu katika hatua mfululizo za ndoa, ilikuwa kama ni hatua ya kuhalalisha ndoa. Mahali hutolewa na watu wa uapande wa mvulana.
Katika siku ya kumpokea Bi. arusi, msichana huvaa nguo nyekundu ikiashiria baraka, na hivi leo baadhi huvaa skati ndefu. Wakati Bi. arusi anapoondoka nyumbani kwa wazazi hulia kwa machozi ikionesha kuwa hataki kuoachana na wazazi wake. Baada ya kufika nyumbani kwa mume sherehe ya ndoa huanza. Katika baadhi ya sehemu nchini China watu wana mila ya Bi. harusi kuvuka karai la makaa ikimaanisha kuchoma mambo yote yaliyopita na kuanza kuishi na mumewe maisha motomoto. Baada ya kuingia chumbani, kwanza wanapiga magoti kwa mungu, kwa wazazi na wao wenyewe, kisha wanakunywa pombe kwa kuzungushiana mikono, na ndani ya chumba chao mume na mke hukata nywele chache na kuweka pamoja kama ni kitu cha ahadi ya uaminifu wao na kuhifadhi nywele hizo daima.
Chakula cha ndoa pia kinaitwa "karamu ya furaha". Watu wanaoshiriki katika ndoa hiyo huenda "kunywa pombe ya furaha". Bi. arusi inampasa awamiminie pombe wageni na kuwapatia vitoweo kwa kuonesha kuwashukuru kushiriki katika ndoa yao.
|