20: Makumbusho kwenye Mtandao

Ugunduzi Mkubwa wa Vitu vya Kale

"Njia ya Hariri"

"Njia ya Hariri" iliyofunguliwa miaka elfu mbili iliyopita inajulikana sana duniani. Hii ni njia kama daraja kati ya China na nchi za Ulaya, Asia na Afrika, na ilitoa mchango mkubwa katika biashara ya mabadilishano ya vitu kati ya Mashariki na Magharibi.

"Njia ya Hariri" ilisafirisha hariri za China hadi Magharibi. Kutokana na uchunguzi njia hiyo ilianza katika Enzi ya Han, wakati huo njia hiyo ya upande wa kusini ilielekea magharibi hadi Afghnistan, Iran na Misri, njia nyingine ilipitia Pakistan, Kabul nchini Afghanistan, na kufikia Karach nchini Pakistan na kutoka Persia kufikia Rome.

Tokea karne ya pili K.K. hadi karne ya pili, njia hiyo iliunganisha nchi nne kubwa, nchi hizo zilikuwa ni Rome, Parthia (Iran ya kale), Kushan (Asia ya kati) na Enzi ya Han ya China. Tokea hapo maendeleo ya utamaduni wa nchi yoyote hayakuwa ya nchi moja tu.

Tokea karne ya 7 hadi karne ya 9 katika Enzi ya Tang, biashara iliyofanywa kwa kutumia njia hiyo ilikuwa ya kufana kabisa, bidhaa nyingi za China zilisafirishwa nchi za nje na bidhaa za nchi za Magharibi ziliingizwa nchini China. Pamoja na bidhaa, vyombo vya vioo, wanyama, vito na lulu, ubani, muziki na dansi pia ziliingizwa nchini China, na pamoja na hariri, ufundi wa kutengeneza karatasi, uchapaji, baruti, dira na vyombo vya vanishi pia vilijulikana katika nchi za Magahribi.

Kadhalika, dini ya Buddha ilijulishwa nchini China katika Enzi ya Han Magharibi (206-220), picha zilizochorwa kwenye kuta za mapango yaliyochongwa katika karne ya 3 mkoani Xinjiang zimeonesha wazi jinsi dini ya Buddha ilivyoingia nchini China kutoka India.

Hadi kufikia karne ya 9, kutokana na mabadiliko ya uchumi na siasa katika nchi za Ulaya, na hasa kutokana na maendeleo ya uchukuzi wa baharini, njia hiyo ilianza kuzorota. Hadi kufikia karne ya 10 yaani Enzi ya Song, njia hiyo haikutumika sana kwa ajili ya biashara.

"Njia ya Hariri" ni ndefu na ilikuwa na miaka mingi, iliwahi kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya ustaarabu duniani. Katika miaka ya karibuni UNESCO imetoa wito wa kuanzisha "uchunguzi mpya wa njia mpya ya hariri", na kuipatia "njia ya hariri" kuwa "njia ya mazungumzo" ili kustawisha mazungumzo na maingiliano kati ya Mashariki na Magharibi.

Mapango ya Maijishan na Mapango ya Longmen

Mapango ya Maijishan yako katika sehemu ya kaskazini magharibi ya China, mkoani Gansu. Kutokana na maandishi ya historia, mapango hayo yalianza kuchongwa katika karne ya 3 K.K. yaani Enzi ya Qin, na tokea hapo sanamu za Buddha mbalimbali zilianza kuchongwa mlimani kuanzia mita 30 juu ya ardhi hadi mita 70.

Sanamu za Buddha zilichongwa ndani ya mapango 194 yenye sanamu 7000, na jumla ya picha kwenye kuta za mapango zina mita za mraba 1300. Sanamu hizo na picha zinasaidia sana uchunguzi wa historia ya dini ya Buddha, historia, mila na desturi za raia.

Mapango ya Longmen yako katika mkoa wa Henan, karibu na mji mkuu wa mkoa huo kwa kilomita 13. mapango kwa jumla yako 2300 na sanamu za Buddha zaidi la lakini moja, na kuna mawe yenye maandishi 3600, minara ya dini ya Buddha 40. ndani ya mapango kwenye kuta pia kuna picha za kuchorwa.

Sanamu na picha hizo ni vitu halisi kwa ajili ya utafiti wa enzi za kale za China Kati ya mapango hayo, pango moja linaloitwa Pango la Binyang lilianza kuchongwa mwaka 500 na kumalizika mwaka 523. Sanamu ya Buddha ndani ya pango hilo pamoja na wafuasi wake zote zilichongwa kama watu wa kweli, hata mikunjo ya nguo inaonekana wazi.

Kaburi la Yi na Kengele Mfululizo

Kwa mujibu wa maandishi ya kale, watawala wa enzi za kale nchini China walitilia maanani sana muziki. Kila wanapofanya sherehe walikuwa wakiburudika na muziki, na waliona muziki ni dalili ya ustawi wa taifa. Mwaka 1978, kengele mfululizo za muziki zilifukuliwa kutoka kaburi la mtu wa kale Yi katika mji wa Suizhou, mkoani Hubei.

Februari mwaka 1978 sehemu moja ilipojengwa, wajenzi waligundua sehemu ya "udongo wenye rangi nyeusi" tofauti na sehemu nyingine. Baada ya kuchimba waligundua kaburi lenye urefu wa mita 21 na upana wa mita 16. Baada ya kufumua kaburi hilo waligundua vitu zaidi ya 15,000 vya vyombo vya shaba nyeusi, ala za muziki, silaha, vyombo vya dhahabu na vya mianzi, lakini kilichovutia zaidi ni kengele mfululizo 65 za shaba nyeusi.

Kengele kubwa ina kimo cha sentimita 153.4 na ndogo ina urefu wa sentimita 20.4, jumla ya uzito ni kilo 2500, kuna maneno 2800 yaliyochongwa kwenye kengele hizo. Kila kengele ina sauti mbili za muziki, na zinaweza kupigwa muziki wa aina yote.

Kwa kufanya utafiti wataalamu wamethibitisha kuwa kwenye kaburi hilo alizikwa mtu aliyeitwa Yi ambaye alikuwa mtemi wa Dola la Zeng, na mtu huyo alizikwa kiasi cha miaka 400 K.K.

Kutokana na kuwa kaburi hilo lilikuwa ndani ya maji chini ya ardhi, vitu ndani ya kaburi havikuharibika na kwa sababu ya maji, vitu kwenye kaburi hilo havikuibiwa.

Baada ya kufukua kengele mfululizo, serikali ya mkoa ilijenga jumba la maonesho, na kaburi lilirudishwa kama awali, na vilevile imeundwa bendi ya kupiga muziki kwa kengele hizo.

Magofu ya Yin na Maneno kwenye Gamba la Kobe

Kwa sababu historia ya China ina karne kadhaa, vitu vya utamaduni vilivyoko chini ya ardhi ni vingi. Tokea karne ya 20 teknolojia ya kisasa ya nchi za Magharibi ilipoanza kutumika nchini China, vitu vingi vya kale viligunduliwa.

Mjini Anyang mkoani Henan, kuna magofu yenye kilomita za mraba 24. Hayo ni magofu maarufu ya Yin. Kutokana na maandishi ya historia, katika karne 14 K.K. mfalme wa Enzi ya Shang alihamisha mji mkuu kutoka mji wa Qubu hadi Anyang, tokea hapo katika miaka 300, mji huo ulikuwa ni mji mkuu wa Enzi ya Shang. Mwaka 1046 K.K. mfalme wa Enzi ya Zhou alimshinda mfalme wa Enzi ya Shang, mji huo ukawa magofu. Kwa sababu Enzi ya Shang pia inaitwa Enzi ya Yin, kwa hiyo magofu hayo yamepewa jina la "Magofu ya Yin".

Magofu ya Yin ni ugunduzi mkubwa wa vitu vya kale katika karne ya 20 nchini China. Mwaka 1928 katika ugunduzi mwa mwanzo yaligunduliwa maneno kwenye gamba la kobe, vyombo vya shaba nyeusi.

Maneno kwenye gamba la kobe yalitumika kwa ajili ya kupiga ramli, kwenye gamba hilo yalichongwa majina ya wapiga ramli, tarehe na maswali yaliyoulizwa, kisha kukaushwa kwa moto na gamba likapasuka. Wapiga ramli watapata majibu kutokana na mipasuko.

Hivi sasa kuna magamba kama hayo laki moja na elfu 60, na kati ya magamba hayo baadhi ni vipande tu ambavyo havina maandishi, kutokana na hesabu, maneno kwenye magamba ni zaidi ya elfu nne, na kati ya maneno hayo elfu nne yaliyotambulika kwa maana yake yako zaidi ya elfu moja. Kutokana na maneno hayo elfu moja, watu wa leo wanaweza kufahamu kwa kiasi fulani hali ya siasa, uchumi na utamaduni katika Enzi ya Shang.

Mtaalamu mashuhuri Bw. Guo Muore aliandika matokeo yake ya utafiti wa maneno kwenye gamba la kobe mwaka 1929. hivi sasa wataalamu wa maneno hayo ni profesa Qiu Sigui wa Chuo Kikuu cha Beijing na profesa Li Xueqin wa Taasisi ya Historia ya China.

Magamba ya kobe yenye maneno licha ya kugunduliwa katika magofu ya Enzi ya Shang, mengine ambayo yalikuwa mapema zaidi ya Enzi ya Zhou Magharibi pia yaligunduliwa, lakini magamba hayo hayana maneno mengi. Katika muda wa miaka 70 iliyopita, wataalamu wa mambo ya kale wamegundua mahekalu zaidi 50, makaburi 12 na makaburi mengi ya makabwera na matajiri na vyombo vya udongo, vyombo vya shaba nyeusi katika magofu ya Enzi ya Shang. Vitu hivyo vimewafahamisha watu kimsingi hali ya jamii ya kale nchini China.

Makaburi ya Wafalme wa Dola la Xixia

Ugunduzi wa kaburi la mfalme wa Dola la Xixia ni ugunduzi mkubwa wa mambo ya kale katika karne ya 20 nchini China, kaburi hilo liko katika sehemu ya kaskazini magharibi ya China.

Miaka 770 iliyopita, nchini China kulikuwa na enzi tatu za kifalme kwa pamoja, nazo ni Song, Liao na Xixia.

Dola la kifalme Xixia lilikuwa na lugha na maandishi yake, lakini kwa bahati mbaya, mwaka 1227 liliposhambuliwa na jeshi la kabila la Wamongolia maandishi yote yalichomwa moto, kwa hiyo habari kuhusu maandishi ya dola hilo imekuwa kitendawili.

Mwanzoni mwa miaka ya 70 ya karne iliyopita makaburi ya wafalme wa Dola la Xixia yaligunduliwa, na katika muda wa miaka 30 wataalamu wa mambo ya kale walifanya uchunguzi mara nyingi na kupiga ramani katika sehemu ya makaburi na kimsingi wamethibitisha makaburi ya wafalme yalipo na hali ya ndani ya makaburi hayo.

Makaburi ya wafalme yako katika sehemu ya jangwa yenye kilomita za mraba 50, kwa jumla kuna makaburi tisa ya wafalme na makaburi ya matajiri 250. Sehemu hiyo ya makaburi ni kubwa ambayo inaweza kulingana na sehemu ya makaburi ya wafalme wa Enzi ya Ming mjini Beijing. Kila moja kati ya makaburi ya wafalme tisa lilijengwa kwa umbo la mstatili kutoka kaskazini hadi kusini.

Kaburi la Nam. tatu kati ya makaburi tisa lina eneo kubwa zaidi, wataalamu wanaona kuwa kaburi hilo ni la mfalme wa kwanza wa Dola la Xixia, Li Yuanhao.

Pagoda ndani ya sehemu ya makaburi hayo inasifiwa kama ni "piramidi ya Mashariki". Mnara una pembe nane, na kipenyo kirefu kina urefu wa mita 34, na kinapungua jinsi mnara unavyokwenda juu, lakini hivi sasa ni vigumu kuthibitisha kama mnara huo ulikuwa na matabaka matano au saba.

Katika ugunduzi uliofanyika tarehe 30 Aprili mwaka 2000 katika kaburi la namba tatu, wataalamu waligundua sanamu yenye mwili wa ndege na kichwa cha binadamu. Wataalamu walisema, sanamu hiyo ni pambo katika hekalu la dini ya Buddha.

Hivi sasa vitu zaidi ya laki moja vimegunduliwa katika sehemu hiyo, ambavyo ni thamani kubwa kwa ajili ya utafiti wa utamaduni wa Dola la Xixia.

Hekalu la Famensi

Hekalu la Famensi liko katika mkoa wa Shanxi, magharibi mwa China, hili ni hekalu maarufu sana kwa sababu ndani ya hekalu hili chini ya pagoda kilizikwa kipande cha mifupa ya mwanzilishi wa dini ya Buddha, Sakyamuni. Aprili, mwaka 1987, watalamu wa mambo ya kale walipojenga upya pagoda ya Buddha lililoporomoka, bila makusudi waligundua ukumbi mmoja ulio chini ya msingi wa pagoda ya zamani, vitu ndani ya ukumbi huo vilistaajabisha duniani. Ugunduzi wake unathaminiwa kama ugunduzi wa sanamu za askari na farasi za Enzi ya Qin.

Hekalu la Famensi liko mbali na mji wa Xi An kwa kilomita 120 upande wa magharibi, lilijengwa katika Enzi ya Wei Kaskazini nchini China, yaani mwaka 499 hivi. Hekalu hili liliwahi kuwa na ustawi mkubwa katika Enzi ya Tang iliyokuwa katika karne ya 7 nchini China. Serikali ya Enzi ya Tanga ilitumia pesa nyingi na watu wengi kuongeza majengo katika hekalu hilo mpaka likawa na nyua 24 za nyumba, na watawa elfu 5. Wakati huo hekalu hili lilikuwa kubwa kabisa katika eneo la mji mkuu wa Enzi ya Tang.

Kutokana na vidokezo vya dini ya Buddha, ili kuenzi dini ya Buddha mfalme mmoja wa India ya kale ambaye aliifanya dini hiyo iwe ya kitaifa aliigawa mifupa ya mwanzilishi wa dini ya Buddha, Sakyamuni, kwa vipande vipande na kuvizika chini ya pagoda 84,000 duniani. Pagoda kama hizo 19 zilijengwa nchini China, na pagoda ndani ya hekalu la Famensi ni moja kati ya hizo.

Kwa sababu ya kuzikwa kipande cha mfupa wa mwanzilishi wa dini ya Buddha, hekalu hilo lilipata waumini wengi na umaarufu duniani. Kutokana na vitabu vya zamani, jumla walikuwako wafalme wanane wa Enzi ya Tang waliwahi kuchukua sehemu ya mwili wa Sakyamuni hadi kwenye kasri ya kifalme na kuabudu, na walitoa zawadi nyingi kwa hekalu hilo. Lakini kutokana na vita, mitetemeko ya ardhi, hali ya ustawi wa hekalu hilo baadaye ukatoweka kabisa.

Mwaka 1981, pagoda yenye matabaka 13 iliporomoka kutokana na mvua. Mwaka 1987, mkoa wa Shanxi ulishirikisha wataalamu wa mambo ya kale kufanya uchunguzi juu ya msingi uliobaki wa pagoda, na wakagundua ukumbi huo uliokuwa chini ya ardhi kwa miaka 1,113. Eneo la ukumbi huo ni mita za mraba 31.48, ndani yake vilikuwako vitu vingi vya Enzi ya Tang, licha ya kipande cha mfupa wa Sakyamuni, pia viko vyombo vya kauri, vitambaa vya hariri vya Enzi ya Tang. Kwa mujibu wa takwimu za historia, vitambaa vya hariri vilivyoko ndani ya ukumbi huo ni vya hali ya juu. Uzi wa dhahabu wa kushonea una unene wa milimita 0.1 na ulio mwembamba sana una milimita 0.66 tu ambao ni mwembamba kuliko unywele. Ndani ya sanduku lililosukwa kwa matawi ya miti kiliwekwa kitambaa cha hariri, ingawa unene wa kitambaa chenyewe kilichokunjuka una sentimita 23 tu lakini kina matabaka 780.

Ndani ya ukumbi huo pia zimegunduliwa vyombo vingi vya dhahabu na fedha, na vya kauri.

Ili kutunza hekalu na vitu vyake vilivyochimbuliwa, yamejengwa makumbusho. Kwa kushirikiana na wataalamu wa Ujerumani, wataalamu wa China wamefankiwa kupata teknolojia ya juu kuhifadhi vitabaa vya hariri. Mwaka 2002 kipande cha mfupa wa mwanzilishi wa dini ya Buddha, Sakyamuni, kilipelekwa Taiwan kwa makusudi ya kuabudiwa. Katika muda wa mwezi mmoja, waumini waliokwenda kuabudu walifikia milioni 4.

Utamaduni wa Sanxingdui

China ina ardhi kubwa na ilipokuwa katika zama za kale, kulikuwa na madola mengi madogo madogo. Mkoa wa sasa wa Sichuan ulikuwa ni Dola la Shu lililopo. Katika miaka ya 70 ya karne iliyopita, vitu vilivyofukuliwa katika Sanxingdui mkoani humo vilishangaza watu wa dunia. Mwaka 1986 wataalamu wa mambo ya kale waligundua mashimo makubwa mawili yaliyozikwa vitu vya thamani kubwa zaidi ya 1000 kwa ajili ya tambiko. Vitu vya utamaduni ambavyo vilikuwa vimelala kwa miaka 3000 chini ya ardhi vimefukuliwa.

Ndani ya vitu vilivyogunduliwa, vitu vya ajabu vilikuwa ni vinyago vya kuvaa usoni vya shaba nyeusi, vinyago hivyo karibu vyote vina njusi nene, macho makubwa, mgongo wa pua ulioinuka sana, mdomo mpana na kutokuwa na kidevu. Uso unaonekana si kama kucheka wala kukasirika. Sura za vinyago zilitofautiana sana na sura halisi za watu wa zama zile, lakini sura za vinyago zinamaanisha nini?

Katika mashimo hayo mwaili pia iligunduliwa sanamu ya mwili mzima ya shaba nyeusi. Sanamu hiyo ina kimo cha sentimita 170, ni sanamu kubwa kabisa ya shaba nyeusi duniani. Wataalamju wanaona kuwa Sanamu hiyo ilionekana si ya mtu wa kawaida, na iligunduliwa katika shimo la kufanyia tambiko.

Licha ya vinyago na sanamu, pia viligunduliwa vitu vingi vya bakora ya dhahabu, meno ya ndovu na "mti wa ajabu". Bakora ya dhahabu ina urefu wa mita 1.42, juu yake kuna michoro na ndege wawili na samaki wawili. "mti wa ajabu" una urefu wa mita nne na una matawi tisa katika matabaka matatu, na kwenye kila tawi alisimama ndege mmoja. Kutokana na utafiti, ndege hao haimaanishi ndege wa kawaida, bali ni ndege wa mungu wanaowakilisha jua.

Wataalamu wamegundua kuwa vitu vilivyofukuliwa vina mtindo wa Dola la Shu lakini pia vina mtindo wa Misri, na vikombe vya mvinyo vina mtindo wa Kimagharibi. Hii ikimaaisha kuwa Dola la Shu lilikuwa na mawasiliano na nchi za nje.

Kaburi la Mfalme Zhu Yuanzhang I

Kaburi la Mababu wa Enzi ya Ming lilikuwa ni kaburi lililojengwa na mwanzilishi wa Enzi ya Ming, Zhu Yuanzhang, kwa ajili ya mababu zake, ni kaburi la kwanza kabisa katika Enzi ya Ming (1368-1644). Zhu Yuanzhang alizaliwa mwaka 1368 katika ukoo maskini vijijini na kufa mwaka 1398. Ili asilale na njaa, aliwahi kuwa sufii katika hekalu fulani. Baadaye alishiriki katika uasi wa wakulima ulioanzia mwaka 1271 hadi 1368. Kwa sababu ya uhodari na ujasiri wake katika mapambano hatua kwa hatua akawa kiongozi wa waasi kutoka askari wa kawaida, na mwishowe mwaka 1368 alikuwa mfalme wa enzi yake ya Ming.

Baada ya Zhu Yuanzhang kuwa mfalme alijenga kaburi kwa ajili ya babu yake, baba wa babu yake na babu wa babu yake, alizika nguo na kofia za watu hao ndani ya kaburi.

Kaburi hilo liko kando ya Ziwa la Hongze, ambalo ni moja kati ya maziwa makubwa manne ya maji baridi nchini China. Kaburi hilo lilijengwa kwa miaka 28. kutokana na maandishi ya historia, katika sehemu ya kaburi kuna kuta za tabaka tatu za kuizungukia sehemu ya kaburi, madaraja matatu, kumbi, vibanda na nyumba, kwa jumla kuna vyumba karibu elfu moja. Mpaka sasa kuna barabara ya kufikia kwenye kaburi, barabara hiyo ina urefu wa mita 250 kutoka kusini hadi kaskazini, na pembeni mwa barabara kuna sanamu za wanyama na maofisa, jumla ya sanamu hizo ni 42 ambazo mbili mbili zinakalibiana pande mbili za barabara.

Mwaka 1680 kaburi hilo lilizama ndani ya ziwa kutokana na mafuriko makubwa. Mwaka 1963 sehemu ya ziwa la Hongze ilipata ukame, sanamu nyingi zilionekana, sanamu hizo kila moja ina kimo cha mita zaidi 3 na uzito tani 10. kumbi ziliporomoka, lakini kutokana na uchunguzi, wataalamu wamethibitisha kuwa vitu vingi ndani ya kaburi havijaharibika.

Baada ya ukame uliotokea mwaka 1963, ukame mwingine pia ulitokea mwaka 1993, na 2001. Hasa ukame uliotokea mwaka 2001 ukuta wa ulionekana kwa sehemu kubwa kuliko miaka yote iliyokuwa na ukame. Ingawa majengo juu ya ardhi yameharibika, lakini ukubwa na ufahari wa kaburi hilo bado unaonekana wazi.

Kaburi la Mababu wa Enzi ya Ming II

Kaburi la mfalme wa kwanza wa Enzi ya Ming (1368-1644), Zhu Yuanzhang ni moja ya makaburi makubwa ya kale duniani.

Zhu Yuanzhang alizaliwa mwaka 1368 katika ukoo maskini vijijini na kufa mwaka 1398. Ili asilale na njaa, aliwahi kuwa sufii katika hekalu fulani. Baadaye alishiriki katika uasi wa wakulima ulioanzia mwaka 1271 hadi 1368. Kwa sababu ya uhodari na ujasiri wake katika mapambano hatua kwa hatua akawa kiogozi wa waasi kutoka askari wa kawaida, na mwishowe mwaka 1368 alikuwa mfalme wa enzi yake ya Ming.

Kaburi la mfalme huyo Zhu Yuanzhang lilianza kujengwa katika miaka alipokuwa mfalme na lilimalizika baada ya mtoto wake kurithi kiti chake cha ufalme, jumla lilitumia miaka 25. Kwa kuwa mwanzoni Zhu Yuanzhang aliufanya mji wa Nanjing kuwa mji mkuu, kaburi lake lilijengwa huko, lakini baadaye mtoto wake alichagua Beijing kuwa mji mkuu. Kwa hiyo, miongoni mwa makaburi ya wafalme wa Enzi ya Ming, ni kaburi hilo tu lililojengwa kaika Nanjing, mengine yote yalijengwa kwenye vitongoji vya Beijing. Ukuta wa kuzunguka kaburi la Zhu Yuanzhang una urefu wa kilomita 22.5 ambao ni sawa na thuluthi mbili ya urefu wa ukuta wa mji wa Beijing. Kutokana na uharibifu wa hali ya hewa katika miaka mia sita, mbao zote za majengo kwenye sehemu za kaburi ziliozwa, lakini hata hivyo kutokana na misingi ya mawe ukubwa wa majengo unaweza kuonekana wazi. Mtindo wa majengo unafanana na ule wa makaburi mengine ya wafalme wa Enzi ya Ming ila eleo lake ni kubwa zaidi. Kwa hiyo ni wazi kwamba makaburi ya wafalme wengine wa Enzi ya Ming yaliyojengwa katika Beijing yote yaliiga mtindo wa kaburi hilo la mfalme wa kwanza wa enzi hiyo, Zhu Yuanzhang.

Tofauti na maburi mengine ya Enzi ya Ming ni kuwa njia ya kufikia kaburi ni njia ya kupindapinda badala ya kunyooka. Baadhi wanasema kwamba Zhu Yuanzhang alitaka kujionyesha wazo lake tofauti na wengine katika ujenzi wa makaburi, baadhi wanasema kuifanya njia iwe ya kupindapinda ni kwa ajili ya kurefusha njia ya kufikia kaburi. Njia hiyo ilianza kutoka kibanda kikubwa chenye jiwe la kaburi, paa la kibanda hicho limeharibika kabisa, zilizobaki sasa ni kuta nne tu. Ndani ya kibanda hicho kuna jiwe refu kubwa lenye maandishi yaliyoandikwa na mtoto wake, yakieleza sifa za baba yake Zhu Yuanzhang, jumla maneno 2746. Kwenye sehemu ya kati ya njia, pande mbili zilipangwa sanamu za wanyama wawili wawili sawa kukabiliana, sanamu hizo ni za simba, ngamia, ndovu, farasi n.k., jumla aina 12 na kwenye njia inayoelekea kaskazini zilipangwa sanamu za maofisa na askari zenye ukubwa kama kitu halisi.

Mfalme Zhu Yuanzhang alizikwa pamoja na mkewe katika ukumbi ulio chini ya ardhi. Kuhusu mahali ukumbi huo ulipo watu walikuwa na mawazo tofauti. Ili kuzuia wizi wa mali za kaburini, mazishi yalifanywa kwa ujanja kutoka milango yote 13 ya mji kwa wakati mmoja, na mazishi yote yalikuwa sawa ili kubabaisha ya kweli, kwa hiyo wapi maiti ya mfalme Zhu Yuanzhang ilipo ilikuwa fumbo katika miaka mingi. Kuanzia mwaka 1997, wataalamu wa mambo ya kale walifanya uchunguzi mara nyingi kwa teknolojia ya juu katika eleo la mita 20,000, wakapata data zaidi ya 20,000, na wishowe wamehakikisha ukumbi ulipo wenye maiti ya mfalme. Wataalamu wa kusimamia ukaguzi huo wanasema kwamba ukumbi wa maiti ya Zhu Yuanzhang uko chini ardhi kwa mita kumi kadhaa, na ukumbi huo uko salama bali haukuwahi kuibiwa kama uvumi ulivyosemwa miaka mingi.

Kulingana na makaburi ya wafalme waliotangulia, handaki lililochimbwa chini ya ardhi la kupeleka jeneza ukumbini licha ya kutonyooka tena linaachana na mstari wa kulenga ukumbi moja kwa moja, sababu yake haifahamiki hadi leo. Mtindo huo pia uliigwa na wafalme waliofuata wa Enzi ya Ming katika ujenzi wa makaburi yao. Kwa mfano, kaburi la Ding lililokuwa limechimbuliwa miongoni mwa makaburi 13 ya wafalme wa Enzi ya Ming katika vitongoji vya Beijing, handaki lake la kupeleka jeneza kwenye ukumbi wa maiti liliachana na ukumbi kwa upande wa kushoto, kinyume na kaburi la Zhu Yuanzhang. Kadhalika, wataalamu wa mambo ya kale wamegundua kwamba juu ya kilima cha kaburi sehemu kiasi cha 60% hivi ilijengwa kwa mikono, yaani kwenye sehemu hiyo yalipangwa mawe makubwa mengi. Kutokana na uchunguzi, mawe hayo hapo awali yalikuwa chini ya kilima, mawe hayo licha ya kutia uzuri wa kilima cha kaburi hilo, tena yanaweza kuzuia mmomonyoko wa udongo na wizi wa kaburi. Kitu cha ajabu ni kwamba wataalamu wa mambo ya kale wamegundua kumbe sanamu za wanyama zote zilichongwa kwa visukuku vya viumbe vilivyokuwa na miaka milioni 300 iliyopita, na baadhi hata vinaweza kuonekana kwa macho na baadhi vinaweza kuonekana kwa kusaidiwa na kioookuzi. Kutokana na ugunduzi huo, sanamu hizo licha ya kuwa na thamani ya kihistoria, kisanaa tena zina thamani kubwa za kisayansi.

Makaburi 13 ya Enzi ya Ming

Zhu Yuanzhang, mfalme wa kwanza wa Enzi ya Ming, aliufanya mji wa Nanjing kuwa mji mkuu, alipokufa alimrithisha kiti cha enzi yake mjukuu wake badala ya wanawe. Kutokana na hayo mtoto wake wa nne, Zhu Li alizusha vita kutaka kunyakua utawala wa enzi hiyo, na mwishowe alifanikiwa. Alipouteka mji mkuu Nanjing, yule mjukuu aliyerithishwa ufalme alikuwa ametoroka na hakujulikana wapi alikokwenda, hadi sasa suala hili bado ni fumbo. Baada ya kushika utawala, Zhu Li aliona kwamba mji wa Nanjing ulikuwa si salama, akauacha Nanjing na kufanya Beijing kuwa mji mkuu. Mfalme Zhu Li alianza kujenga kaburi lake alipokuwa katika utawala wake. Baada ya kuchunguza chunguza mwishowe aliamua sehemu ya magharibi viungani mwa Beijing kujenga kaburi lake. Hapo ni sehemu yenye mandhari nzuri na milima ya kijani, akalipatia kaburi lake jina la "Kaburi la Chang Ling". Toka mwaka 1409 kaburi la Zhu Li lilipoanza kujengwa hadi 1644 Enzi ya Ming ilipomalizika, katika miaka zaidi ya 200, jumla wafalme 13 wa Enzi ya Ming walizikwa katika sehemu hiyo.

Ni kama mpangilio wa ujenziwa kaburi la mfalme wa kwanza wa Enzi ya Ming, Zhu Yuanzhang, kwamba katikati ya sehemu ya makaburi 13 kuna njia ya kupeleka jeneza. Mbele ya lango kuu la sehemu kya makaburi kuna mlango mkubwa wa uliogengnezwa kwa mawe tupu ya marumaru, hadi leo mlango huo umekuwa na miaka 450. Baada ya kupita mlango huo kuna lango kuu la sehemu ya makaburi. Hili ni lango ambalo mfalme lazima alipite alipokwenda kutambika. Kuanzia pande mbili za lango hili ulijengwa ukuta wenye kilomita 40 uliozunguka sehemu ya makaburi mlimani. Ukuta huo una vipito 10 licha ya lango kuu. Nyakati zile kila kipito kilikuwa kikilindwa na askari wengi ili kuhakikisha usalama wa shemeu ya makaburi. Katika sehmu ya makaburi, kulikuwa na nyumba za wasimamizi, ambao kazi yao ni kushughulika na mambo ya kutoa heshima kwa marehemu:kuna nyumba za watunza bustani ambao kazi yao ilikuwa ni kushughulika za tambiko, na nyumba za walinzi ambao kazi yao ni kulinda sehemu ya makaburi.

Kwa ajili ya kuhifadhi kaburi lisiibiwe, wafalme licha ya kubuni hadithi nyingi za kuwatisha wezi wa mali ya makaburi, nao pia walificha sana makaburi yao yenyewe. Kwa hiyo ilikuwa ni vigumu kuupata ukumbi wa kuwekea maiti ndani ya kaburi la Ding Ling ulikuwa haujulikani, na haukujulikana mpaka mwezi Mei mwaka 1956 wataalamu wa mambo ya kale walipoanza kulichimbua kaburi hilo. Kutokana na juhudi hatimaye waligundua kaburi. Ukumbi wa kuwekea maiti ndani ya kaburi la Ding Ling una mita za mraba 1195 ambao umegawanyika katika sehemu tano, yaani ya mbele, ya kati, ya nyuma, ya kulia na kushoto. Ukumbi huo ulijengwa kwa mawe matupu. Mbao zilitandikwa sakafuni ili gari la kubeba jeneza lilipoingia ndani ya ukumbi huo lisiharibu sakafu, mbao hizo mpaka sasa bado zipo. Katikati ya ukumbi huo kuna viti vitatu vya mawe vinavyoashiria madaraka, sehemu ya nyuma ya ukumbi huo ni muhimu, kwani katika sehemu hiyo jukwaani yamewekwa majeneza matatu. Kati ya majeneza hayo matatu, la katikati ni kubwa zaidi ambalo ni la mfalme, mengine mawili pembeni ni majeneza ya malkia wawili. Pembeni kuna masanduku 26 ya kafara na majagi makubwa ya kauri. Kutoka katika kaburi la Ding Ling vimepatikana vitu vya utamaduni zaidi ya 3000, miongoni mwa vitu hivyo, kuna vitambaa vya hariri, nguo, mapambo na vyombo vya dhahabu na vya kauri ambavyo vyote vina thamani kubwa katika kufanya uchunguzi wa sanaa za Enzi ya Ming.

Sanda Iliyotengenezwa kwa Vito

Katika Enzi ya Han Magharibi nchini China yaani kuanzia mwaka 206 kabla ya kuzaliwa Kristo hadi mwaka 8, watu waliamini maiti wangeweza kuhifadhiwa bila kuoza. Kutokana na mawazo hayo, wafalme na matajiri wa enzi hiyo walitumia sanda zilizotengenezwa kwa vito kuhifadhi maiti zao. Mwaka 1968 katika mji wa Mancheng, mkoani Hebei, kaskazini mwa China wataalamu wa mambo ya kale kwa mara ya kwanza waligundua sanda kama hiyo.

Katika wilaya ya Mancheng mkoani Hebei umbali wa kilomita 200 kutoka Beijing lilikuwepo kaburi moja alimozikwa mfalme wa kwanza wa Dola la Zhongshan katika Enzi ya Han, Liu Sheng, na mkewe Dou Wan kwa pamoja. Kutokana na maandishi ya kihistoria, Liu Sheng alipata ufalme wa Dola la Zhongshan mwaka 154 K.K. na alitawala kwa miaka 42. Huyo ni mfalme wa kwanza katika dola hilo.

Kaburi hilo lilijengwa kwenye kilima kimoja kizima. Ndani ya kaburi hilo kuna mapango mengi yaliyotumika kwa kazi mbalimbali kama vile kulala, sebule na muziki. Kwa hiyo kaburi hilo ni kama kasri kubwa mlimani.

Kutokana na namna mapango yalivyopangwa kibusara, inaonesha kwamba kaburi hilo lilikuwa limesanifiwa kwa makini kabla ya kuchimbwa, na kazi hiyo ilikuwa ngumu sana. Uchongaji wa mapango hayo makubwa kwenye mlima wa mawe hata sasa ungehitaji muda wa mwaka mzima kwa watu zaidi ya mia moja na vyombo vya kazi vya kisasa.

Ndani ya kaburi kulikuwa na vitu vingi vya kafara, ambavyo viliwekwa kwa mpangilio mzuri, na miongoni mwa vitu hivi vyombo vya udongo ni vingi zaidi, vingine ni vya shaba, chuma na fedha. Lakini vilivyostaajabisha zaidi ni "sanda iliyotengenezwa kwa vito vilivyounganishwa kwa nyuzi za dhahabu".

"Sanda" hiyo ilitengenezwa kwa kuunganisha vipande vya mawe vyenye maumbo ya mstatili, mraba, pembe tatu n.k. na kila kipande kwenye kona kuna tundu kwa ajili ya kupitisha uzi wa dhahabu. Sanda hiyo ina sehemu ya kichwa, nguo, suruali, glavu na viatu. Ina urefu wa jumla ya mita mbili na vipande vya mawe 2498, nyuzi za dhahabu kiasi cha gramu 1100. kwenye sehemu ya kichwa kuna vizibo vya macho, pua, masikio na kinywa. Na kwenye sehemu ya kiuno kuna kikasha cha kufunika sehemu za siri.

Kutokana na maelezo ya wasomi, utengenezaji wa sanda kwa vipande vya mawe ni mgumu sana, kwanza mawe yahitajika kukatwa vipande vidogo na vyembamba kulingana na mwili kwa ukubwa tofauti na halafu kutoboa matundu ili kuunganishwa pamoja. Kwa kupima, baadhi ya nyufa kati ya vipande vizima ni milimita 0.3 tu, huu ni ufundi mkubwa kweli.

Kwenye pango la mke wa mfalme Liu Shen, imegunduliwa sanda nyingine ya mawe ambayo pia ina sehemu tano kama ya kichwa, nguo, suruali, glavu na viatu ila tu ni fupi kidogo ikilinganishwa na sanda ya mume wake. Sanda hizi mbili ni nzima hadi sasa, ambapo ni mara ya kwanza kupatikana zikiwa nzima. Ugunduzi wake umetufahamisha zaidi sanda ya vipande vya mawe katika Enzi ya Han.

Mbali na sanda za vito, kutoka kaburi la Liu Sheng pia zimegunduliwa sindano za tiba na beseni zenye neno "tiba", ambazo ni vitu halisi vinavyothibitisha hali ya utibabu na akyupancha katika siku za kale nchini China. Upanga aliokuwa nao kiunoni mfalme Liu Sheng unaonesha kufuliwa mara kadhaa, na umeonesha ufundi mkubwa wa kuyeyusha chuma cha pua katika siku za kale.

Kutokana na thamani kubwa ya kaburi hilo la Enzi ya Han, mwaka 1988 liliorodheshwa kwenye kumbukumbu za taifa.

Utamaduni wa Dola la Yelang

"Ujeuri wa Yelang" ni usemi unaojulikana kwa wote wa China. Usemi huo ulitokana na hadithi iliyotokea miaka 2000 iliyopita katika Dola la Yelang, kusini magharibi mwa China. Dola hilo liliwahi kustawi kwa miaka mia moja hivi, lakini baada ya muda huo likatoweka haraka kama kimwondo. Mwanzoni mwa karne hii wataalamu wa mambo ya kale walifumua siri za dola hilo.

Mwezi Septemba mwaka 2001 makaburi 108 ya dola la Yelang yaligunduliwa katika wilaya ya Hezhang, mkoani Guizhou, kusini magharibi mwa China. Dola la Yelang lilikuwa la kabila dogo lililokuwa katika karne ya tatu K.K. hadi karne ya kwanza. Dola hilo lilikuwa na ustawi mkubwa na jeshi lake hata lilikuwa na askari laki moja. Kutokana na kuwa dola hilo lilikuwa milimani na likijitenga na sehemu nyingine, kwa hiyo mfalme wa dola hilo alipokutana na mjumbe wa Enzi ya Han Magharibi alimwuliza, "Dola lako na langu Yelang lipi ni kubwa?". Mfalme wa Dola la Yelang aliuliza hivyo kwa kutojua kwamba Enzi ya Han Magharibi ni dola kubwa kiasi gani. Tokea hapo "ujeuri wa Yelang" umekuwa usemi wa kudhihaki mjeuri, lakini kwa upande mwingine umethibitisha kwamba kweli Dola la Yelang lilikuwepo.

Lakini dola hilo lilitoweka ghafla, na historia yake na utamaduni wake umekuwa mafumbo katika historia ya China. Ugunduzi wa makaburi ya dola la Yelang uliopatikana katika mwaka 2001 umekuwa mkubwa kabisa katika mwaka huo nchini China.

Makaburi yote yalikuwa karibu sawa, na si makubwa, kila moja lina urefu wa mita tatu na upana wa kiasi cha mita moja. Kitu cha ajabu kilichogunduliwa ndani ya makaburi hayo ni kuwa kila maiti imefunikwa na kitu kama beseni ya shaba kwenye kichwa na miguu. Wataalamu wanaona kuwa mila ya kufunika maiti kwa beseni ya shaba inaonesha kuwa watu wa Dola la Yelang walikuwa na imani kwa vitu vya kusafishia, na baadhi ya wataalamu wanaona kuwa mila hiyo inahusika na imani ya dini fulani.

Makaburi yaliyogunduliwa wilayani Hechang yamewapatia watu wa leo ufunguo wa kufungua siri za utamaduni wa dola hilo, lililokuwepo miaka elfu mbili iliyopita.

Vyombo vya Kauri na China

Neno "China" katika Kiingereza lina maana ya taifa la China na pia lina maana ya vyombo vya kauri, lakini kuna uhusiano gani kati ya China na vyombo vya kauri?

Uchunguzi wa mambo ya kale umethibitisha kwamba vyombo vya kauri nyeupe tulivyo navyo hivi leo vilitokana na vyombo vya kauri nyeusi, na vyombo vya kauri nyeusi vilitokana na vyombo vya udongo. Vyombo vya kauri nyeusi vilikuwa na tabia ya vyombo vya udongo kama vyombo vya kauri nyeupe. Vyombo hivyo vya kauri nyeusi vilivyokuwa vya zamani sana viligunduliwa kutoka magofu ya Longshan wilayani Xia katika mkoa wa Shanxi, ambavyo hadi leo vimekuwa na miaka 4200.

Vyombo halisi vya kauri vilianza hasa katika Enzi ya Han Mashariki, enzi ambayo ilianzia mwaka 23 hadi 220. Mwanzoni vilianza kutengenezwa katika sehemu ya akusini mwa China mkoani Zhejiang, baadaye ufundi huo ulienea hadi kaskazini na ukapata maendeleo makubwa na kutokea ufundi wa kutengenezea vyombo vya kauri nyeupe. Tofauti iliyopo kati ya kauri nyeusi na nyeupe ni kiasi cha chuma ndani ya udongo. Udongo wenye kiasi kidogo cha chuma unaonekana mweupe baada ya kuchomwa na wenye kiasi kikubwa utaonekana wa kijivujivu au mweusi kidogo. Awali, vyombo vya kauri vilikuwa havina rangi lakini baada ya kutokea kwa vyombo vya kauri nyeupe watu wakapaka rangi tofauti za kioo lakini rangi tawala huwa nyeupe, hivyo rangi tofauti huonekana wazi na kupendeza zaidi. Kwa hiyo, kutokea kwa kauri nyeupe kuna maana kubwa katika maendeleo ya vyombo vya kauri.

Katika enzi za Tang na Song yaani toka karne ya 10 hadi mwanzoni mwa karne ya 13, ufundi wa kutengenezea vyombo vya kauri uliendelea mbele kwa hatua nyingine kubwa. Vyombo vya kauri vyenye rangi tatu vilianza kutengenezwa katika kipindi hicho. Vyombo hivyo vilipakwa rangi tatu maalumu za kioo kabla ya kuchomwa, na wakati wa kuchomwa ndani ya tanuru rangi hizo zikabadilika kikemikali na zikawa na rangi nyingi zaidi, matokeo yake ni kama picha za kuchorwa za mtindo wa Kichina, rangi hizo zinajulikana kama rangi tatu za Enzi ya Tang.

Katika Enzi ya Ming, enzi ambayo ilianzia mwaka 1368 hadi 1644 na Enzi ya Qing iliyoanzia mwaka 1644 hadi 1911 ufundi wa kutengenezea vyombo vy akauri ulifikia kwenye kiwango kikubwa kwa idadi au kwa ubora. Mji uliopo kusini mwa China uitwao Jingdezhen ulikuwa "mji wa kauri" hasa uliojulikana katika enzi hizo unaendelea na sifa yake hadi leo, na takriban vyombo vyote vya kauri vya hali ya juu vinatengenezwa katika mji huo. Vyombo vya kauri vya China vilianza kusafirishwa hadi nchi za nje katika karne ya 8, kabla ya hapo njia ya hariri iliyojulikana kote duniani ilikuwa ikiunganisha biashara za China na nchi za nje. Katika karne hiyo ya 8 pamoja na kusafirisha nje vyombo vya kauri, China ikajulikana duniani kwa jina jingine la "nchi ya kauri".

Mwanzoni vyombo vya kauri viliuzwa katika Asia tu, baada ya karne ya 17 vikaanza kuwa mapambo ya fahari ndani ya kasri ya kifalme katika Ulaya ya Magharibi. Baada ya Ureno kufungua njia ya usafiri baharini, vyombo vya kauri vya China vikaanza kuwa zawadi kubwa katika Ulaya nzima. Katika zama hizo mtindo wa sanaa uitwao Rococo ulioenea katika Ulaya ulilingana na sanaa za kauri za China, hii ilikuwa sababu ya vyombo vya kauri kuenea sana katika Ulaya nzima. Kutokana na takwimu isiyokamilika, katika karne ya 17 vyombo vya kauri vya China vilivyosafirishwa nchi za nje vilifikia laki 2 kila mwaka na ilipofika karne ya 18 viliongezeka hadi milioni. Vyombo vya kauri viliuzwa kote duniani, kadhalika neno "china" pia likaenea pamoja na vyombo hivyo katika Uingereza na bara la Ulaya. Neno "china" likawa na maana mbili, yaani vyombo vya kauri na jina la nchi. Ingawa hatuwezi kubainisha kwamba toka lini neno "china" limekukwa jina la nchi, lakini tuna uhakika kwamba ndio sababu ya ufundi wa kutengenezea vyombo vya kauri vinavyowapendeza sana watu wa dunia umeungaisha vyombo vya kauri pamoja na jina la nchi, China.

Kaburi la Enzi ya Han kwenye Mawangdui

Katika miaka ya 70 kaburi moja la Enzi ya Han lililopo kwenye Mawangdui mjini Changsha liligunduliwa. Kaburi lilo lilishangaza dunia nzima kwa maiti iliyopatikana ndani ya kaburi ni maiti pekee duniani yenye miaka 2000 bila kukauka. Pamoja na maiti pia vilifukuliwa vitu vingi vya thamani.

Miaka mingi wenyeji wa mji wa Changsha walikuwa wanasimulia kuwa huko kuna kaburi la kale, lakini kaburi hilo halikuthibitishwa mpaka mwaka 1971. watu walitoboa tundu kwa mtarimbo chini ya ardhi kwa zaidi ya mita kumi, hewa iliyotoka kutoka tundu inapalia pua, na iliwaka kwa kibiriti bila kuzimika.

Jeneza ilifungwa kwa matope meupe ya jasi yenye unene wa mita moja na baada ya matope ni sehemu ya makaa yenye uzito kiasi ya kilo 5000. Jeneza lina matabaka manne, na tabaka la nje lina urefu karibu mita 7, upana mita 5 na kimo mita 3.

Baada ya kufumua jeneza, ndani yake ni maiti ya mwanamke ambayo haujakauka, ngozi bado laini, mikono na miguu inaweza kupindika, na hata alama za vidola vya mikono na miguu inaonekana wazi. Kwa uchunguzi, mwanamke huyo alizikwa katika karne ya pili K.K. yaani mwanzoni mwa Han Magharibi.

Ugunduzi wa "maiti ya mwanamke yenye miaka elfu mbili bila kuoza" ulishangaza dunia nzima. Wataalamu, watalii, wapiga picha walimiminikia mjini Changsha. Pamoja na maiti, pia viligunduliwa vitu vingi vya vitambaa vya hariri, vyakula, dawa, sanamu za mbao, ala za muziki. Kati ya vitu hivyo, vitambaa vya hariri vilikuwa vingi na vilisifiwa kuwa ni "ghala kubwa la hariri la Han Magharibi (206 K.K.- 25 K.K.)".

Ugunduzi wa kaburi la Mawangdui umetoa mchango mkubwa, hasa maiti iliyokamilika na vibao vyenye maandishi. Kwa hiyo ugunduzi huo unasifiwa kuwa ni "ugunduzi mkubwa duniani katika karne ya 20".

Mapango ya Dunhuang

Mapang ya Dunhuang yaliyochongwa katika mlima Mingsha, kaskazini magharibi mwa China, ni hazina kubwa ya sanaa, na ni makubwa kabisa kupita mapango yote mengine matatu nchini China. Kwenye mapango hayo zimechongwa sanamu nyingi za Buddha ambazo ni kumbukumbu zenye umri wa miaka elfu moja na enzi zaidi ya kumi za China. Mapango hayo bado mazima mpaka leo.

Mapango ya Dunhuang yako katika kitongoji cha Mji wa Dunhuang, mkoani Gansu, kaskazini magharibi mwa China. Katika Mlima Minshan upande wa mashariki kwenye genge lenye urefu wa kilomita mbili kutoka kusini hadi kaskazini yalichongwa mapango kwa safu tano kutoka juu hadi chini, na hayo ndiyo mapango maarufu ya Dunhuang duniani.

Mapango hayo yalichongwa kuanzia mwaka 366. siku moja sufii mmoja aliyejulikana kama Lezun alitembelea Dunhuang akagundua mwangaza mkali mlimali Minshan, kwenye utusitusi aliona kama kuna mabuddha wengi kwenye mwangaza huo. Sufii Lezun akafikiri, "Hapa hakika ni mahali patakatifu!" Basi akawaagiza watu kuchonga pango la kwanza la kuwekea sanamu ya Buddha. Tokea hapo mapango yalikuwa yanaongezeka zaidi na zaidi katika enzi kadhaa, hadi karne ya saba ya Enzi ya Tang, mapango yamefikia zaidi ya elfu moja. Kwa hiyo mapango ya Dunhuang pia yanaitwa "Mapango Elfu Moja ya Buddha".

Mapango ya Dunhuang yamedhihirisha sana ya ujenzi wa kale, picha za kuchorwa ukutani na sanamu za kuchongwa. Katika e4nzi kadhaa nchini China watu walichonga mapango na sanamu za mabuddha, na kuchora picha nyingi ukutani ndani ya mapango. Ingawa karne nyingi zimepita, na kuharibiwa na binadamu, hadi leo yako mapango karibu 500 na picha zenye eneyo la mita elfu 50 na sanamu zaidi ya elfu 2. Kama picha zote zingeunganishwa pamoja ungefikia urefu wa kilomita 30.

Kutokana na mapango ya Dunhuang kuwa katika sehemu isiyofikika kwa urahisi, hayakuwa maarufu sana katika miaka mingi iliyopita. Lakini mwanzoni mwa karne ya 20 baada ya kugunduliwa hodari ya vitabu, mapango hayo yakapata umaarufu haraka kote duniani, na kwa ajili hiyo wizi mkubwa wa vitu vya utamaduni utokea huko.

Mwaka 1900, mtunzaji wa mpango Wang Daoshi alipokuwa akifuta mavumbi, kwa bahati nzuri aligundua chumba kilichokuwa na vitabu vya msahafu. Chumba hicho kina urefu na upana wa mita tatu, kilikuwa kimeshehena vitu elfu 50 zikiwemo misahafu, tarazo, picha za kuchorwa n.k. ambazo ni adimu sana duniani. Hivi ni vitu kuanzia karne ya 4 hadi 11, ambavyo vinahusu na historia, jiografia, siasa, makabila, mambo ya kijeshi, lugha, fasihi, sanaa, dini, madawa na ufundi katika Asia ya Katikati, Asia ya Kusini na Ulaya, vinajulikana kama "ensaiklopidia ya zama za kale".

Mtunzaji Wang Daoshi alifurahi mno kwa kuona vitu vingi vyenye thamahi kubwa ambapo alichukua baadhi kuziuza ili ajipatie faida. Kutokana na vitu hivyo kuenea uraiani, vitu vingi ndani ya pango hilo vikatoweka bila kujulikana. "Wapelelezi" wa nchi mbalimbali walipopata habari walikwenda huko. Kutokana na udhaifu wa serikali ya Enzi ya Qing, "wapelelezi" hao kutoka nchi za Urusi, Uingereza, Ufaransa, Japan na Marekani walipora karibu misahafu elfu 40 na picha na sanamu nyingi, ambapo ni hasara kubwa mno. Hivi leo Uingereza, Ufaransa, Russia, India, Ujerumani, Denmark, Sweden, Korea ya Kusini, Finland na Marekani zote zina thuluthi mbili ya vitu kutoka kwenye mapango ya Dunhuang. Pamoja na ugunduzi wa uchumba kilichokuwa na misahafu na vitu vya thamani, wasomi wa China walianza kufanya utafiti. Msaka 1910, maandishi ya kwanza kuhusu utafiti wa vitu vya mapango ya Dunhuang yalichapishwa na kuanzia hapo taasisi ya maandishi ya Dunhuang ikaasisiwa. Katika muda wa zaidi ya miaka kumi kadhaa, wasomi wa nchi nyingi wamekuwa wakifanya utafiti kuhusu sanaa ya Dunhuang, na wasomi wa China ndio waliopata mafanikio zaidi katika utafiti wao. Mapango ya Dunhuang ni hazina ya utamaduni wa China. Serikali ya China ya leo siku zote inatiliamaanani hifadhi yake. Mwaka 1950, serikali ya China imeorodhesha mapango hayo kwenye kumbukumbu za kitaifa. Mwaka 1978 mapango kya Dunhuang yameorodheshwa na UNESCO kwenye kumbukumbu za urithi wa utamaduni wa dunia. Hivi leo, chini ya mlima ulio mkabala na mapango ya Dunhuang yamejengwa maoneshi ya sanaa za mapango, na baadhi ya vitu vimetengenezwa kwa kuiga vitu halisi ya mapango. Watalii kutoka nchi za nje wanasema, "Hii ni hazina kubwa kabisa miongoni mwa sanaa za dini ya Buddha zilizopo duniani hivi leo."

Nyongeza kuhusu Vtu Vlivyofukuliwa katika Kaburi la Mfalme Qinshihuang

Miaka sita baada ya kugundua sanamu za askari na farasi katika kaburi la mfalme wa kwanza wa Enzi ya Qin, Qinshuhuang, mwaka 1980 wataalamu wa mambo ya kale waligundua farasi na mkokoteni wa shaba.

Vitu hivyo viligunduliwa na mtaalamu wa mambo ya kale Yang Xude kwenye mahali palipo chini ya ardhi kwa mita 7.

Kwa kuelekezwa na wataalamu wa mambo ya kale, waanyakazi walichimba kwa makini, walitumia kiasi cha mwezi mmoja mwishowe walipata mikokoteni miwili, farasi wanane, na mikono miwili ambayo yote ni ya shaba kwenye mahali palipo chini ya ardhi kwa mita 7.8.

Vitu hivyo vilichukuliwa pamoja na udongo wenye ujazo wa mita moja kwa kufungwa na mbao na kisha kuchukuliwa kwa winchi, na baada ya kupelekwa kwenye jumbo la maonesho wataalamu wa mambo ya kale walitumia karibu miaka miwili kuzisafisha sanamu hizo kabla ya kuzionesha hadharani.

Sanamu za mikokoteni na farasi ni nusu ya vitu vya kweli, lakini namna ya kutengeneza sanamu hizo zilikuwa ni fumbo.

Sanamu za Askari na Farasi katika Kaburi la Malme Qinshihuang Zilitengenezwaje

Mwaka 1989, wataalamu wa mambo ya kale waligundua matanuri 21 kwenye sehemu ya Mji wa Xi'an, matanuri hayo yalikuwa na miaka 2100. makaburi hayo, kwa makadirio, yanaweza kuchoma sanamu za udongo 7350 hadi 8400.

Wataamu wamegundua kwamba sanamu hizo zilitengenezwa kwa vyombo, ila vichwa ambavyo kabla ya kuchomwa vilikukwa vimechongwa tayari na kisha kupakwa rangi. Matengenezo ya sanamu za askari na farasi kwa ajili ya kaburi la mfalme Qinshihuang walitokea wasanii wengi, na sasa walioweza kuthibitishwa wako 85.

Sufuria ya Kale Iliyo Kubwa Kabisa Duniani Ilitengenezwaje

Mwezi Machi, 1939, kwenye shamba moja karibu na kijiji cha Wuguancun mkoani Henan, katikati ya China sufuria kubwa ya kale iligunduliwa. Sufuria hiyo ina uzito kilo 875, kimo sentimita 133, urefu sentimita 110 na upana sentimita 78. lakini sufuria kubwa kama hivi ilitengenezwa kwa ajili ya matumizi gani? Na ilitengenezwa vipi? Kwa mujibu wa ungunzuzi, sufuria hiyo ilitengenezwa na mfalme wa Enzi ya Shang kwa ajili ya kumfanyia mama yake tambiko. Hapo mwanzo wataalamu waliona kuwa sufuria kubwa kama hivi ilitengenezwa kwa sehemu sehemu na baadaye kuziunganisha pamoja, lakini uchunguzi uliofanywa hivi karibuni wataalamu wanaona kuwa sufuria hiyo ilisubuliwa katika chombo cha udongo, na madini iliyoyeyushwa ilimiminwa pole pole kutoka miguu mitatu ya sufuria hiyo. Hivyo ndivyo sufuria hiyo ilivyotengenezwa.


1 2 3 4