Mapishi ya vyakula vya kichina yanajulikana sana duniani. Takwimu zinaonesha kuwa aina za mapishi ya vyakula vya kichina zimefikia zaidi ya laki moja. Katika maendeleo ya historia ndefu, sehemu mbalimbali za China zimekuwa na aina tofauti za mapishi ya vyakula zenye ladha maalumu za kisehemu. Miongoni mwao, kuna aina 8 maarufu kabisa, yaani mapishi ya vyakula vya Shandong, Sichuan, Guangdong, Jiangsu, Zhejiang, Fujian, Hunan na Anhui. Ladha za aina hizo ni tofauti, kwa mfano, vyakula vilivyopikwa kwenye mikahawa ya mkoani Sichuan huwa vina ladha ya pilipili hoho, na vile vilivyopikwa mjini Shanghai huwa vina ladha ya sukari zaidi. Jiaozi ina historia zaidi ya miaka elfu nchini China, ni chakula kinachopendwa na wachina wengi. Watu hujaza nyama au mboga ndani ya gamba la jiaozi, halafu kupika jiaozi kwa maji ya kuchemka.