Nchini China, kabla ya mwaka 1980, maneno ya “kununua nyumba”, na “mali za nyumba na ardhi” yalikuwa ni mageni kwa watu wa kawaida, kwani wakati ule China ilitekeleza utaratibu wa kugawa nyumba, kila mtu aliyefanya kazi katika kiwanda au idara ya serikali, aliweza kupata nyumba kutoka kwa kiwanda au idara, na kila mwezi alitoa kodi ya pesa kidogo tu, lakini aliyeishi kwenye nyumba siyo aliyemiliki nyumba hii. Kuanzia miaka ya 90 ya karne iliyopita, China iliacha kutekeleza utaratibu huo, na kuanza kuzifanya nyumba kuwa bidhaa za biashara, tangu hapo “kununua nyumba” kumekuwa kunafuatiliwa zaidi na raia wa kawaida. Miongoni mwa wateja wa nyumba wengi ni vijana, hasa vijana wanaojiandaa kufunga ndoa, ambapo wazazi wao wa familia zenye mapato ya kawaida wanakabiliwa na shinikizo kubwa. Hata hivyo watu wengi wanapenda kununua nyumba na kutopenda kupanga nyumba, kwani wanaona kununua nyumba kuna manufaa zaidi.