Tanzania ni moja ya nchi zilizojaliwa kuwa na vivutio vingi ambavyo kwa kweli si rahisi kupatikana katika sehemu nyingine duniani. Kwenye sehemu mbalimbali za nchi hiyo kuna wadudu, mimea na wanyama ambao wanahifadhiwa vizuri. Shughuli za uhifadhi wa viumbe hao zimekuwa zikiendelea kwa muda mrefu.
Lakini hivi karibuni habari kutoka mkoani Tanga, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo kulikuwa na habari ya kufurahisha, wadau wa shughuli za uvuvi walipitisha mapendekezo ya wataalamu wa utafiti wa mambo ya majini yaliyosukuma mbele juhudi za uhifadhi wa mazingira na viumbe. Wataalam hao walipendekeza eneo la bahari mkoani humo liwe hifadhi na eneo lililotengwa kwa ajili ya samaki aina ya Silikanti.
Silikanti ni samaki anayeishi kwenye maji ya kina kirefu na kwa sasa anasadikiwa kupatikana kwenye ukanda wa bahari ya Afrika. Mnyama huyo wa majini ni wa kihistoria na anafananishwa zaidi na wanyama wenye uti wa mgongo wa kwanza kuishi nchi kavu. Kwa umbile, Silikanti ni samaki mwenye mapafu mawili na ni mmoja kati ya samaki wakubwa baharini. Samaki huyu pia ana mapezi mawili yanayofanana na miguu, akiwa anaishi kwenye mapango chini kabisa ya sakafu ya bahari kuanzia kina cha maji ya meta 40 hadi 50 na nyuzi joto za kati ya 14 na 22.
Kwa mara ya kwanza Silikanti alivuliwa kwa bahati mbaya nchini Tanzania mwezi Septemba mwaka 2003 huko Kilwa, mpaka sasa zaidi ya samaki 41 wa aina hiyo wamevuliwa katika bahari ya Hindi eneo la Tanzania kwa kutumia nyavu zinazotegwa na wavuvi kwenye kina kirefu.
Kumbukumbu zinaonesha kuwa samaki huyu ni miongoni mwa viumbe waliotoweka miaka milioni 350 iliyopita, lakini katika miaka ya hivi karibuni kabla ya samaki huyo kuvuliwa nchini Tanzania, kulikuwa na ripoti kuwa alivuliwa nchini Afrika Kusini kwa kunaswa kwenye nyavu za kukokota. Kuvuliwa kwa samaki huyu huko Afrika Kusini kulifanya dunia ifahamu kuwa Silikanti amerejea tena duniani.
Kuvuliwa kwa samaki wa aina hiyo nchini Tanzania, kuliwafanya watafiti wa masuala ya bioanuai kutoka nchi mbalimbali kuanza kufanya utafiti kuhusu eneo la bahari la Kigombe mkoani Tanga alikovuliwa samaki huyo, hivyo ikaonekana kuwa kuna umuhimu wa kuhifadhi eneo ili kuwalinda samaki hawa adimu.
Katika kuifanikisha lengo hilo, mwaka 2003 Tanzania iliunda kamati ya taifa ya Silikanti ili kufuatilia namna gani uhifadhi wa samaki huyo ufanyike. Juhudi hizo za serikali ya Tanzania pia zilizihusisha taasisi nyingine zilizoingia katika jukumu hilo la kutafuta njia za uhifadhi wa Silikanti ikiwa ni pamoja na Idara ya Uvuvi Baraza la Mazingira Tanzania, Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Idara ya Mambo ya Kale, Mamlaka ya Bandari, Polisi wanamaji, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kitivo cha Sayansi za Bahari na Teknolojia ya Maji, Taasisi ya utafiti wa bahari ya Zanzibar pamoja na wadau wengine wanaohusika na uhifadhi wa bahari.
Mchakato wa kuhifadhi eneo la bahari ya Tanga ulianza mapema mwaka 2007 ambapo tafiti mbalimbali za viumbe wa baharini zilifanywa na wataalam watafiti waliobobea wa Tanzania na nje ya nchi, wakiongozwa na Dk Tony Ribbink. Dk Ribbink anayetoka Afrika Kusini akiwa ni Mkurugenzi wa mpango wa kuhifadhi Silikanti unaoitwa ACEP. Dk Ribbin hawezi kusahaulika katika utafiti wa Silikanti nchini Tanzania kwani yeye alitumia muda wake mwingi kufanya utafiti na kazi nyingi zinatohusiana na samaki wa aina hiyo akiwa nchini Tanzania.
Hata hivyo baadhi ya wavuvi wadogo wadogo wa eneo hilo, waliwashangaza watafiti kwa kusema walikuwa wakiwavua samaki wa aina hiyo mara kwa mara, lakini hawakujua kama ni samaki adimu aliyepoteza katika sehemu nyingine duniani. Hata hivyo wamepongeza juhudi za kulifanya eneo la bahari kuwa hifadhi, kwa hatua hiyo itasaidia kuhifadhi mazingira ya bahari na kuongeza idadi ya samaki aina ya Silikanti.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |