• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mambo yaliyojadiliwa sana mwaka jana na wana mtandao na watu wengine kwenye jamii ya China

    (GMT+08:00) 2014-02-18 16:50:13

    Hujambo msikilizaji na karibu katika kipindi cha China Machoni Mwetu, cha kwanza kabisa katika mwaka huu wa 2014. Mimi ni Fadhili Mpunji niko na mwenzangu Pili Mwinyi tayari kukuletea yale tuliyowaandalia leo, ambayo ni moja ya mambo yaliyojadiliwa sana mwaka jana na wana mtandao na watu wengine kwenye jamii ya China.

    Pili: Kwanza kwa kuwa hiki ni kipindi cha kwanza kwa mwaka huu ni vizuri tukiwatakia wasikilizaji wetu heri ya mwaka mpya. Kuvuka ni jambo la kushukuru kwa kuwa wengine mungu hakuwajalia

    Fadhili: Hapa Beijing jana tarehe 1 ilikuwa siku ya mapumziko na wengine walitumia siku hiyo kwa harusi na wengine kwa manunuzi. Leo tunachozungumizia kwenye kipindi hiki, kinahusiana na mambo ya manunuzi, naweza kusema, moja ni la ajabu na lingine ni la busara.

    Pili: Mwisho mwa mwaka jana neno "Tu Hao" liliienea kwenye mtandao wa internet hapa China. Neno hilo kwa kweli lina maana mbaya, lakini naweza kusema, ni kutokana na watu kupata utajiri kwanza, lakini kuendelea kuwa na mawazo ya zamani au kuwa na mawazo ya "kishamba". Mwezi Septemba neno hilo lilitajwa sana na watu hapa China, baada ya kuona kuwa kuna wimbi kubwa la watu kutumia pesa ovyo, kwa kuwa tu wana pesa bila hata kujali wanatumia vipi pesa hizo.

    Fadhili: Kwa sasa hapa China kuna sera moja inataekelezwa kwa nguvu, sera hiyo inahusu kufuatilia na kuhimiza maendeleo ya vijijini na wakulima. Kimsingi sera hii inamtajirisha mtu yoyote ambaye atafanya juhudi. Kuna sera nyingi za upendeleo ambazo kama mtu akipenda, awe mkulima au mfugaji, kama akifanya juhudi anaweza kupata maendeleo mara moja.

    Pili: Kwa sasa naweza kusema watu wa vijijini hapa China wameanza kuwa na maendeleo makubwa, hasa ya kifedha. Matokeo yake ni kuwa wengine wanataka kuonesha wale watu wa mjini kuwa wao ni watu sawa na wa mjini, wakati mwingine hata wao ni kuliko wa mjini. Wengine wanafanya hiyo kwa kuonesha uwezo wao wa kutumia pesa. Wengine unaweza kuona anaamua kununua kitu chenye thamani kubwa bila hata kujua matumizi yake, na wakati mwingine hata anaweza kuwaonesha watu kuwa ananunua kitu fulani ili kuonesha tu kuwa ana pesa za kununua kitu hicho.

    Fadhili: Nakumbuka zamani tulikuwa tunawatania baadhi ya watu kule Tanzania, tulikuwa tunasema kutokana na kutaka kuwaonesha watu kuwa wao una pesa nyingi, unaweza kuamua kukodi basi zima na ukazuia abiria wengine kupanda, ili kuwaonesha kuwa wewe unaweza kukodi basi zima, licha ya kuwa unaweza kukodi taxi. Sasa watu kama hao hapa China wanaitwa Tu Hao.

    Pili: Kwa sasa hapa China kuna mambo mengi tu ambayo kama unataka kuonesha ufahari, unaweza kuyafanya. Unaweza kununua shati zuri la dola 10, lakini kuna wengine watasema hili ni la kiwango cha chini wao watataka kununua shati la dola 50 au hata 100. Au kuna wengine wananunua magari makubwa ambayo yanafaa kutembea porini au kwenye mazingira mabaya. Magari kama haya huwezi hata kujua ni kwanini yapo kwenye miji kama Beijing. Lakini wenye nayo wanaonesha ufahari kwa kumiliki magari kama hayo, kwa kuwa wameona wamarekani au watu wa nchi za magharibi wanatumia magari hayo.

    Fadhili: Kuna wakati simu za Iphone zilipoingia hapa China, kuna moja ilikuwa na rangi ya dhahabu, watu walikuwa wanaiita simu hiyo "Tuhao" maana yake ni simu kwa ajili ya matajiri washamba. Kwa ujumla hali ya namna hii, hatuwezi kusema inatokea China peke yake, pia inatokea katika sehemu nyingine, hasa pale watu wanapotoka sehemu fulani na kuhamia sehemu nyingine.

    Pili: Kuna kundi lingine ambalo naweza kusema ni kundi muhimu zaidi, kundi la wanawake ambao kule nyumbani Tanzania tunawaita mama wa nyumbani. Lakini hapa si mama wa nyumbani wa kawaida. Hawa wanafanya kazi ya kulea mtoto nyumbani, hata naweza kusema kumlea mume, na wakati mwingine kama wazazi wanakaa nyumbani hata wazazi pia wanawatunza. Hawa wamepewa jina la "Dama". Hawa kwa kweli wana mchango mkubwa kwenye familia, na ile tafsiri ya jadi ya mama wa nyumbani labda haiwafai.

    Fadhili: Pili kwanza kuna sifa moja waliyonayo wanawake wa China, wao ni hodari sana kwenye udhibiti wa matumizi ya pesa. Pamoja na kuwa watu huwa wanasema wanawake wa China wanapenda pesa na wanapenda wanaume matajiri, walio wengi si wanawake wafujaji. Wanajitahidi sana kuhakikisha mume hatumii pesa ovyo, hata wao wenyewe hawatumii pesa ovyo. Hata kama ni matajiri wanakuwa waangalifu sana wa kutunza pesa.

    Pili: Hili lina ukweli, naweza kutoa mfano ambao tunaweza kuiga. Tumesema Tuhao wao kazi yao ni kufuja pesa, lakini hawa wanawake wanaoitwa Da ma, wao hutumia pesa kwenye mambo ya maana. Kwa mfano wananunua sana dhahabu. Ukiona wananunua unaweza kusema hawa ni wanawake watumbuaji, lakini ukweli ni kwamba wanachofanya ni kuwa wanataka thamani ya pesa ihifadhiwe kwenye dhahabu. Kwa hiyo hata kama dhahabu akiitunza kwa miaka kumi thamani yake haipungui.

    Fadhili: Naona wanawake wa namna hii wanatumia busara. Sababu ni kuwa kuna maeneo mawili au matatu ambayo wachina wanatumia kuwekeza. Kwanza wanawekeza kwenye soko la nyumba. Yaani wananunua nyumba zinazouzwa sasa halafu baada ya miaka 10 au 15 wanaiuza kwa bei kubwa. Wengine wananunua hisa na kuziuza baadaye kwa bei ya juu. Lakini tatizo ni kuwa usalama wa uwekezaji kwenye soko la nyumba ni kuwa unategemea sera za serikali kama serikali ikiamua kubadilisha sera inawezekana kila kitu kikabadilika na thamani ya pesa walizowekeza ikapotea ndani ya muda mfupi. Na soko la hisa linahitaji muda mwingi sana wa ufuatiliaji, na ujanja kuwekeza kwenye soko hilo, kwa hiyo ni busara kuwekeza kwenye dhahabu.

    Pili: Kwa kawaida watu wanaonunua vitu mara huwa wanaonekana kama ni watu wanaofuja pesa, lakini mfano huu unatuonesha kuwa si lazima kuwa kila mtu anayefanya manunuzi mara kwa mara ni mfuja pesa. Wengine wanatumia pesa kwa busara na kuziweka akiba ambayo baadaye inakuwa na amana yake.

    Fadhili: Nasikia wasichana wa China huwa wanafundishwa tangu wakiwa wadogo kuwa watakapoolewa kama mume akiwa maskini au kama familia itakuwa na matatizo ya pesa, basi inawezekana kabisa kuwa mwanamke anafanya uzembe katika kufanya kazi ya uhasibu. Kwa hiyo naweza kusema hawa tunaowaita Dama, ni wale ambao wamefuata vizuri mafunzo ya wazazi wao na kuangalia hali ya sasa inavyoendelea.

    Pili: Lakini hata tukiangalia hali ya jamii ya China kwa sasa na mabadiliko ya hali ya kijamii tunaweza kusema hata mazingira yenyewe yanahimiza watu kuwa na akili za kubana matumizi na kutunza pesa.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako