Kikundi cha utafiti cha Chuo Kikuu cha Tokyo cha Japan kimetoa ripoti kikisema matetemeko makubwa ya ardhi huenda yanahusiana na mvuto wa mwezi, yana uwezekano mkubwa zaidi wa kutokea wakati mvuto wa mwezi unapokuwa mkubwa.
Mtaalamu wa fizikia ya matetemeko ya ardhi wa Chuo Kikuu cha Tokyo Prof. Satoshi Ide na wenzake wametafiti matetemeko ya ardhi yenye ukubwa wa zaidi ya 5.5 kwenye kipimo cha Richter yaliyotokea katika miaka 20 iliyopita na mawimbi ya baharini wakati huo. Matokeo yanaonesha kuwa miongoni mwa matetemeko 12 ya ardhi yenye ukubwa wa zaidi ya nyuzi 8.2, 10 yalitokea wakati mawimbi ya baharini yalipokuwa makubwa, ambayo yanamaanisha kuwa mvuto wa mwezi ulikuwa mkubwa. Tetemeko kubwa lililotokea mwaka 2004 huko Sumatra, Indonesia na lililotokea mwaka 2011 nchini Japan yote yameonesha uhusiano huo.
Kikundi cha utafiti kimesema mvuto wa mwezi huenda ukasababisha mabadiliko ya mawimbi ya baharini, na kuathiri shinikizo kwenye gamba la dunia. Urefu wa mawimbi ukiinuka kwa mita moja, shinikizo chini ya bahari litaongezeka kwa kPa 10. Ingawa mabadiliko hayo ni madogo sana yakilinganishwa na nishati inayotolewa kwenye matetemeko ya ardhi, lakini huenda yakawa pigo la mwisho linalosababisha matetemeko hayo.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |