Paka ni wanyama wanaofugwa na watu wengi duniani. Wakilinganishwa na wanyama wengine, ni rahisi zaidi kwa paka hao kupata ugonjwa wa figo, lakini zamani watu walikuwa hawajui sababu yake.
Hivi karibuni watafiti wa Chuo Kikuu cha Tokyo, Japan wamegundua kuwa hali hii inatokana na protini aina ya AIM kutofanya kazi kwenye damu ya paka.
Kabla ya hapo watafiti waligundua kuwa uwezo wa mafigo ya binadamu au panya unaposhuka, protini aina ya AIM kwenye damu huanza kufanya kazi, kuingia kwenye mafigo, kusaidia kuondoa sumu kwenye neli, na kuboresha uwezo wa mafigo.
Lakini protini hiyo kwenye damu ya paka ni tofauti na zile za binadamu au panya. Paka wakipata ugonjwa wa figo, protini hiyo haitafanya kazi, na kusababisha ugonjwa wake kuzidi kuwa mbaya.
Watafiti wamerekebisha jeni za baadhi ya panya na kuwafanya wawe na jeni zinazofanana na zile za paka, halafu waliwafanya kupata ugonjwa wa kushindwa kwa figo. Panya hao wote walikufa ndani ya siku 3, lakini asilimia 70 ya panya wenye jeni za kawaida waliopata ugonjwa bado wako hai baada ya siku 5. Na panya wenye jeni zilizorekebishwa wakipigwa sindano ya protini ya AIM ya kawaida, watapona kwa kasi, na idadi ya vifo itapungua kwa kiasi kikubwa.
Watafiti wamesema utafiti huo huenda utasaidia kurefusha maisha ya paka.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |