Kutumia simu ya mkononi au kompyuta siku nzima kunaweza kuathiri mawazo ya binadamu? Hivi karibuni watafiti wa Russia wamefanya uchunguzi na kuthibitisha kuwa kutumia tovuti za SNS kupita kiasi kunabadilisha mawazo ya binadamu.
Watafiti wawili wa Chuo Kikuu cha Ualimu cha Moscow wamewahoji wanafunzi 1,100 wa vyuo vikuu vya Russia. Matokeo yanaonesha kuwa asilimia 73 ya wanafunzi wanaotumia tovuti za SNS kwa muda usiozidi saa moja kila siku wanafikiri familia ni muhimu zaidi katika maisha yao, asilimia 65 ya wale wanaotumia tovuti hizi kwa saa kadhaa pia wanafikiri hivyo, na ni asilimia 56 tu ya wale wanaotumia tovuti hizi kwa muda mrefu sana kila siku wanafikiri hivyo.
Aidha, uchunguzi unaonesha kuwa miongoni mwa wanafunzi wanaotumia tovuti za SNS kwa muda mfupi zaidi, asilimia 10 wanaona maadili ni sifa nzuri zaidi, lakini hakuna mtu yeyote kati ya wale wanaotumia tovuti hizi kwa muda mrefu zaidi anayefikiria hivyo.
Watafiti hao wawili wanaona pengine ni rahisi zaidi kwa vijana kukubali mawazo ya pekee yanayovuma kwenye mtandao wa Internet, na kuacha baadhi ya mawazo ya jadi.
Prof. Andrei Manoilo wa Chuo Kikuu cha Moscow alipozungumzia utafiti huo amesema tovuti za SNS bado ni njia nzuri ya kuwasiliana na jamaa na marafiki, watu wanatakiwa kuzitumia kwa muda mwafaka, na kutofikiri maisha halisi kwa mawazo yanayovuma kwenye mtandao.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |