Sokwe(chimpanzee), sokwe wadogo (bonobo) na sisi binadamu wote ni wa jamii ya nyani. Gazeti la Biolojia ya Kisasa la Marekani limetoa makala likisema sokwe wadogo wazee huenda wanahitaji kuvaa miwani kama binadamu wanavyofanya, kwani ni rahisi kwao kukosa uwezo wa kuona vitu vya karibu.
Kukosa uwezo huo kunasababishwa na kupotea kwa uwezo wa lenzi kwenye macho yetu. Kwa kawaida binadamu wanakabiliwa na tatizo hili kuanzia umri wa miaka 45.
Kikundi cha watafiti cha taasisi ya jamii ya nyani ya Chuo Kikuu cha Kyoto cha Japan kimetafiti sokwe wadogo pori 14 wenye umri wa miaka 11 hadi 45 wanaoishi nchini Jamhuri ya Congo. Matokeo yanaonesha kuwa sokwe wadogo wazee hawawezi kuona vizuri vitu vya karibu, hivyo wale wenye umri mkubwa zaidi wanapochana manyoya ya wenzi wao, wanakaa mbali zaidi na kunyoosha mikono yao zaidi.
Kikundi hiki kinasema wamegundua kuwa sokwe wadogo wanakabiliwa na tatizo la kuona kuanzia umri wa miaka 40, ambao unafanana na umri wa binadamu. Hii inamaanisha kuwa kukosa uwezo wa kuona vitu vya karibu si matokeo ya maisha ya kisasa wala kutazama skrini kwa muda mrefu kupita kiasi, bali ni mchakato wa kawaida wa kuzeeka wa mababu za pamoja za binadamu na sokwe mdogo.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |