Mahakama kuu ya Uingereza imeidhinisha kupeleka mwili wa msichana aliyefariki akiwa na umri wa miaka 14 nchini Marekani na kuuhifadhi kwenye baridi kali.
Msichana huyu alifariki mwezi Oktoba mwaka huu kutokana na saratani. Kabla ya kufariki, alisikia kuwa kuna teknolojia ya kuhifadhi mwili kwenye baridi kali, hivyo alitaka mwili wake uhifadhiwe kwa njia hii, na iko siku atafufuka tena.
Wazazi wake walioachana wana maoni tofauti kuhusu matakwa yake. Mama anakubali, lakini baba anapinga. Baba yake alisema hata mtoto wake akifufuka katika miaka 200 ijayo, atasikitika kwa sababu labda atasahau mambo yote, na hatakuwa na jamaa yeyote.
Hivyo msichana huyu aliiomba mahakama kutoa idhini ya kumruhusu mama yake kuchukua mwili wake ili kutimiza ndoto yake.
Teknolojia ya kuhifadhi kwenye baridi kali ni kuweka viumbe, viungo na seli katika mazingira zaidi ya nyuzi 100 chini ya sifuri, na baadhi ya viumbe vinaweza kufufuka baada ya kuyeyuka.
Lakini wataalamu wengi wanashuku teknolojia hii, wakisema hakuna ushahidi wowote unaothibitisha kwamba binadamu anaweza kufufuka.
Prof. Barry Fuller wa Chuo Kikuu cha London amesema teknolojia hii ina mustakabali mzuri, lakini kwa sasa bado ni vigumu kuhifadhi baadhi ya viungo kikiwemo figo kwenye baridi kali. Hivyo ana mashaka kuhusu kama binadamu aliyehifadhiwa kwenye baridi kali atafufuka au la.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |