Unajua watu wa Mexico, Australia na Thailand wanafanana katika jambo gani? Wote wanachukulia lava na pupa wa nyuki kuwa chakula kitamu. Baada ya kupikwa au kukaushwa, chakula hiki kinakuwa kaukau kama kokwa, licha ya hayo, kina protini nyingi zaidi kuliko nyama ya ng'ombe. Utafiti uliofanywa na watafiti wa Chuo Kikuu cha Copenhagen unaonesha kuwa pupa hasa pupa wa nyuki dume ni chakula kizuri kwa binadamu.
Kwa kawaida wafugaji wa nyuki wanatoa baadhi ya pupa wa nyuki dume kwenye masega yao ili kuwazuia wasiambukizwe na utitiri. Kufanya hivyo hakutaathiri uzalishaji, kwani nyuki wafanyakazi wanazalisha asali na kuchavusha mazao ya kilimo badala ya nyuki dume. Aidha, bei ya pupa wa nyuki ni nafuu. Mambo hayo yamewafanya pupa wa nyuki kuwa chakula kizuri.
Kula chakula hiki bado kunakabiliwa na matatizo kadhaa. Kwanza, ni vigumu kutoa pupa wa nyuki kwenye masega kwani ni laini na ni rahisi kuharibika. Pili, pupa wana mafuta mengi na ni rahisi kuoza. Lakini wanasayansi wanasema tatizo hili linaweza kutatuliwa, kwani pupa wanaweza kuhifadhiwa kwenye friji kwa miezi 10.
Prof. Annette Bruun Jensen wa Chuo Kikuu cha Copenhagen anasema asali ya nyuki inapendwa na watu wengi duniani, na pupa wa nyuki wanawahimiza watu wa nchi za magharibi kukubali kula wadudu.
Utafiti huo kuhusu lishe za pupa wa nyuki umetolewa kwenye gazeti la Journal of Apicultural Research.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |