Chanzo cha nyanya kiko katika milima ya Andes, bara la Amerika ya Kusini. Wenyeji wa huko waligundua nyanya pori na kuanza kulima mboga hii katika mwaka 500 k.k. Katika lugha ya kienyeji ya huko, neno nyanya lina maana ya tunda nene. Siku hizi matunda hayo manene yanaliwa kote duniani.
Lakini watu wengi wanalalamika kwamba ladha ya nyanya si tamu kama ya zamani. Tena siku hizi nyanya zinaweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu, hivyo wanashuku huenda jeni za nyanya zimerekebishwa.
Mtazamo wao si sahihi. Jeni za nyanya hazijarekebishwa. Mabadiliko ya ladha ya nyanya ni matokeo ya uzalishaji wa kilimo. Wateja wanapenda zaidi nyanya zenye sura nzuri, na wauzaji wanapenda nyanya zinazoweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu, hivyo wakulima wanalima aina za nyanya zenye sifa hizi kwa wingi zaidi. Lakini kwa bahati mbaya, nyanya zenye sifa hizi huwa na ladha mbaya.
Zamani nyanya zilikuwa na rangi mbalimbali zikiwemo kijani na nyekundu, lakini wateja wanapenda nyanya nyekundu, hivyo siku hizi karibu nyanya zote ni nyekundu. Nyanya nyekundu ina uwezo mdogo zaidi wa kuzalisha Chlorophyll, ambayo inahusiana na usanisinuru. Uwezo mdogo wa usanisinuru unamaanisha uzalishaji mdogo wa sukari, kwa hivyo ladha ya nyanya zenye sura nzuri si tamu.
Aidha, ili kusafirisha nyanya kwenda kwenye masoko ya mbali, wakulima wanalima zaidi nyanya ngumu badala nyanya laini. Hivyo siku hizi hata nyanya ikiwa imekomaa, bado inakuwa ngumu kama nyanya mbichi.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |