Watafiti wa Uingereza wametoa makala kwenye gazeti la Maumbile wakisema wamegundua njia mpya ya kuinua uzalishaji wa ngano kwa asilimia 20 katika maabara yao. Ngano ni chakula muhimu duniani, hivyo ugunduzi wao huenda ukainua uwezo wa kuhakikisha usalama wa chakula duniani.
Watafiti wa taasisi ya Rothamsted na Chuo Kikuu cha Oxford wamezalisha kemikali tangulizi ya kemikali nyingine iitayo Trehalose 6 Phosphate (T6P). T6P ni kemikali muhimu inayodhibiti ukuaji wa mimea.
Watafiti hao wamepanda ngano katika maabara yao, na baada ya ngano kuchanua, walimwagilia kemikali tangulizi kwenye ngano kila baada ya siku 5. Baada ya kuvuna, watafiti wamepima uzito wa ngano na kiasi cha wanga na protini, na kugundua kuwa ukubwa na uzito wa ngano wote umeongezeka kwa asilimia 20.
T6P pia inaweza kuinua uwezo wa ngano wa kukinga ukame. Watafiti hawakumwagilia maji baadhi ya ngano katika siku 10 baada ya mbegu kuchipuka na kutoa mizizi, badala yake walimwagilia maji yenye kemikali tangulizi ya T6P katika siku ya 9, baadaye walimwagilia maji kama kawaida, na mwishowe ngano hizi bado zilivunwa.
Watafiti wamesema kemikali tangulizi waliyoizalisha inaweza kuichochea ngano kutoa T6P nyingi zaidi, na kuleta uzalishaji mkubwa. T6P inafanya kazi katika mimea mingi, hivyo njia hii huenda ikatumiwa katika mazao mengi zaidi.
Dr. Matthew Paul kutoka taasisi ya Rothamsted amesema watafiti wataendelea kufanya majaribio katika mashamba mbalimbali ili kutafiti athari ya mazingira tofauti kwa kemikali walizozalisha.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |