Vifaru weupe ni moja kati ya wanyama walioko hatarini zaidi duniani. Miongoni mwa vifaru hao, wale wa aina ya kaskazini wamebaki watatu tu duniani, ambao sasa wanahifadhiwa kwa makini nchini Kenya.
Hivi karibuni kikundi cha watafiti kinachoundwa na Prof Katsuhiko Hayashi kutoka Chuo Kikuu cha Kyushu cha Japan na watafiti kutoka Ujerumani kimeanzisha utafiti ili kuwaokoa vifaru hao wanaokaribia kutoweka kwa teknolojia ya kiviumbe. Watafiti hao wanajaribu kuzalisha mayai ya vifaru jike kwa kutumia seli zao za iPS, kuyaunganisha mayai na mbegu za uzazi za vifaru dume zilizohifadhiwa zamani kwenye friji, halafu kuweka zaigoti miilini mwa vifaru wa aina nyingine wenye uhusiano wa karibu na vifaru weupe wa kaskazini, na kuzaa vifaru.
Seli za iPS ni seli shina zinazogeuka kutoka seli za mwili kwa hatua maalum. Seli shina zina uwezo wa kukua na kuwa seli za aina mbalimbali. Mwezi Oktoba mwaka jana, watafiti wa Chuo Kikuu cha Kyushu walifanikiwa kuzalisha mayai ya panya nje ya mwili kwa kutumia seli za iPS za panya, kuyaunganisha na mbegu za uzazi na kuzalisha panya wachanga wenye afya nzuri. Lakini ni vigumu zaidi kuzalisha mayai ya vifaru weupe kuliko panya.
Watafiti wamesema, kama majaribio yao yakifanikiwa, matumizi ya seli za iPS yataleta uwezekano mkubwa zaidi katika mambo mengine.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |