Hivi karibuni kompyuta laki 2 katika nchi na sehemu zaidi ya 100 duniani zimeambukizwa kirusi cha WannaCry, nyaraka zote kwenye kompyuta huzuiwa na haziwezi kutumika mpaka watu walipe.
Mhandisi wa mtandao wa Internet mwenye umri wa miaka 22 kutoka Uingereza asiyetaka kutaja jina lake aligundua kuwa kirusi hiki kimekuwa kikijaribu kutembelea tovuti isiyokuwepo yenye jina la ajabu, hivyo alisajili tovuti hii kwa kutumia pauni 8.5, ili kutafiti data husika za kirusi hiki. Lakini jambo la kushangaza lililotokea, maamubukizi ya kirusi hiki yalisita baada ya tovuti hii kusajiliwa.
Mhandisi huyu amechambua sababu ya kirusi hiki kutembelea tovuti hii. Kama tovuti hii isingekuwepo, inamaanisha kirusi hiki bado kisingetambuliwa na wafanyakazi wa usalama wa Internet, na kingeweza kuenea bila vizuizi vyovyote; lakini kama tovuti hii ipo, inamaanisha wafanyakazi wa usalama wa Internet wametambua uwepo wa kirusi hiki na kuchukua hatua za kukizuia, hivyo inatakiwa kirusi hiki kuacha kuenea ili kuepusha data nyingi zaidi zisipatikane na wafanyakazi hao.
Mhandisi huyu amesema hakujua kama kusajili tovuti hii kungezuia kuenea kwa kirusi hiki, kwani alifanya hivyo kwa bahati tu.
Kampuni ya Maabara ya Kaspersky ya Russia imesema kirusi hiki kimetumia software ya kudukua ya "Eternal Blue" inayotoka kwenye benki ya silaha za mtandao wa Interent ya Idara ya Usalama ya Marekani NSA. Mwezi Aprili mwaka huu, shirika la wadukuzi Shadow Brokers lilidokeza baadhi ya software zinazotumika kudukua za NSA ikiwemo "Eternal Blue".
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |