Wanasayansi wa Marekani wamegundua kuwa minyoo wenye umbo la neli wanaoishi kwenye bahari yenye kina kirefu katika ghuba ya Mexico wanaweza kufikia umri wa miaka 300, na kama wakipata chakula cha kutosha, huenda wakaishi kwa miaka mingi zaidi.
Minyoo hao wanaojificha kwenye neli zao wanaonekana kama mimea yenye machaka mengi inayokua juu ya miamba au mchanga. Mazingira ya bahari yenye kina kirefu ni salama kwa minyoo hao, kwani hakuna maadui wengi. Kabla ya hapo, wanasayansi waligundua minyoo wenye umri wa miaka 250 katika kina chenye mita 300 hadi mita 950 katika ghuba ya Mexico. Hivi karibuni wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Temple cha Marekani wametafiti minyoo wa aina nyingine wanaoishi katika kina chenye kilomita 1 hadi 3, na kugundua kuwa wana maisha marefu zaidi, ambao baadhi wana umri wa zaidi ya miaka 300.
Hadi sasa rekodi ya mnyama mwenye uti wa mgongo kwenye nchi kavu aliyeishi maisha marefu zaidi ni kobe mkubwa aliyeishi katika visiwa vya Galapagos mwenye umri wa miaka 177, na mamalia aliyeishi maisha marefu zaidi ni nyangumi mwenye kichwa kinachofanana na pinde mwenye umri wa miaka 211. Mnyama mwenye umri mkubwa zaidi ni chaza wa Actic mwenye umri wa miaka 507.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |