Nyota kibete nyeupe ni nyota ndogo na nzito yenye joto kubwa inayotoa mwanga meupe. Uzito wa nyota ya aina hiyo ukifikia mara 1.4 ya uzito wa jua, italipuka. Na ikilipuka yote, inabadilika kuwa nyota aina ya supernova Ia ambayo inatoa mwanga mkali sana.
Wanasayansi wana maoni tofauti kuhusu sababu ya kulipuka kwa nyota kibete nyeupe. Baadhi yao wanaona kwamba nyota mbili kibete nyeupe zinaungana pamoja na kuunda nyota mpya ambayo ni nzito sana na kusababisha mlipuko. Wengine wanaona nyota kibete nyeupe inavuta vitu kutoka kwenye nyota kubwa iliyoko karibu na mwishowe kulipuka.
Wanasayanasi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Australia wakishirikiana na wenzao wa Czech, Ujerumani, Hungary, Marekani na Canada, wamechunguza mabaki ya mlipuko wa nyota aina ya supernova Ia yaliyopewa jina la LP40-365 ambayo yanapita galaksi kwa kasi kubwa sana ili kuthibitisha uzito, joto na muundo wa kemikali wa mabaki hayo.
Wanasayansi wamegundua kuwa mabaki hayo yalitoka kwenye mfumo wa nyota mbili, ambako nyota kibete nyeupe ilivuta vitu kutoka kwenye nyota nyingine kubwa. Baada ya nyota hiyo kuvuta vitu vingi kupita kiasi, ililipuka na kuvunja mfumo huo. Mabaki yenye ukubwa unaofanana na nyota ndogo yalirushwa angani na kuruka kwa mamilioni ya miaka.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |