Roboti iitwayo Atlas iliyotengenezwa na Kampuni ya Boston Dynamic ya Marekani ina uwezo mkubwa, sasa imejifunza kuruka sarakasi kwa kubiruka nyuma kama wachezaji.
Roboti hiyo ni moja kati ya roboti za kisasa zaidi duniani, ina urefu wa mita 1.8 na uzito wa kilo 150, ina kichwa, mwili, mikono na miguu, macho yake yana sensa mbili, na inaweza kutembea kwa miguu kama binadamu.
Hivi karibuni kampuni ya Boston Dynamic imetoa video ikionesha kuwa roboti hiyo inaruka juu ya masanduku kadhaa, kuruka na kubiruka juu ya sanduku la mwisho, halafu kuruka sarakasi kwa kubiruka nyuma kutoka kwenye sanduku hilo.
Video hii yenye urefu wa sekunde 54 imewashangaza watu wengi. Mtu mmoja aliuliza, "Atlas atashiriki kwenye mashindano ya awamu ijayo ya Olimpiki?" Na mtu mwingine ameonesha wasiwasi wake, akisema "Roboti hii imenishangaza na kunitisha, mambo yanayosimuliwa kwenye filamu yamebadilika kuwa hali halisi ndani ya muda mfupi."
Kampuni ya Boston Dynamic imefahamisha kuwa Atlas inaweza kusafisha nyumba, kupeleka sanduku, kutembea kwenye ardhi iliyofunikwa na theluji, kunyanyuka baada ya kuanguka, kusimama kwa mguu mmoja, na kutembea juu ya nguzo.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |