Zaidi ya raia 12,000 wa DRC wakimbilia Zambia
Zaidi ya watu 12,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamekimbilia nchi jirani ya Zambia kutafuta hifadhi kutokana na machafuko Kusini Mashariki mwa nchi yao.
Umoja wa Mataifa unaonya kuwa, hali ya wakimbizi hao ni mbaya, na wanakosa mahitaji muhimu kwa sababu ya uhaba wa fedha lakini pia kuondelea kuongezeka kwa wakimbizi hao.
UNHCR inasema inahitaji Dola za Marekani Milioni 236 Kuwasaidia wakimbizi hao.
Tangu mwezi Agosti pekee, zaidi ya wakimbi 8,000 wameingia nchini Zambia wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Mdororo wa usalama nchini DRC umesababisha raia wengi kuyahama makazi yao.
Hayo yanajiri wakati ambapo chama kikuu cha upinzani nchini DRC, UDPS kinasema hakimtambui Waziri Mkuu Bruno Tshibala kama mwanachama na kiongozi ndani ya chama hicho.
Hatua hii inakuja baada ya Tshibala ambaye amewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho kusema kuwa anaandaa mkutano wa chama hicho kumteua kiongozi mpya wa UDPS baada ya kifo cha Ettien Tshisekedi mapema mwaka huu.
Kiongozi wa sasa wa chama hicho ni Felix Tshisekedi.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |