Maua yanatoa asali ili kuwavutia vipepeo, na vipepeo wanasaidia kuchavusha maua. Je, ni vipepeo au maua yaliyotangulia duniani mapema zaidi?
Kikundi cha watafiti cha kimataifa kimechambua mabaki ya mbawa za wadudu na kugundua kuwa vipepeo na nondo walitangulia duniani miaka milioni 50 kabla ya mimea aina ya Angiosperm yaani mimea inayochanua kuja duniani.
Kabla ya hapo, wanasayansi walifikiri maua yalitangulia duniani kabla ya vipepeo katika mwanzoni mwa zama ya Cretaceous ambayo ni zaidi ya miaka milioni 100 iliyopita. Lakini katika miaka ya hivi karibuni vipimo vya DNA vilionesha kuwa wadudu hao huenda walitangulia mapema zaidi.
Watafiti wa Chuo Kikuu cha Utrecht cha Uholanzi na Chuo cha Boston cha Marekani wamepata mabaki kadhaa ya mbawa za vipepeo na nondo kaskazini mwa Ujerumani. Mabaki hayo yanaonesha kuwa vipepeo na nondo walikuja mwishoni mwa zama ya Triassic na mwanzoni mwa zama ya Jurassic. Wale aina ya Glossata walikuja miaka milioni 212 iliyopita, miaka milioni 50 kabla ya mimea inayochanua kuja duniani.
Lakini vipepeo walikula nini kabla ya maua kuwepo? Watafiti walisema huenda walikunywa majimaji kutoka kwenye majani yaliyokatika na mbegu zisizopevuka za mimea aina ya Gymnospermous ikiwemo misonobari na mivinje. Baada ya maua kuja duniani, vipepeo na mimea wakawa na uhusiano wa kunufaishana.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |