Hatimaye mashabiki wa mshambuliaji wa timu ya Uingereza Liverpool Mohammed Salah wameonyesha furaha yao baada ya kuhakikishiwa kuwa mshambuliaji huyo wa Misri atashiriki katika michuano ya kombe la dunia , akiwakilisha nchi yake ya Misri.
Daktari wa timu ya taifa ya Misri amesema kuwa matibabu ya kiungo huyo wa mashambulizi hayatachukua zaidi ya wiki tatu huku taifa lake likitarajiwa kucheza mechi yake ya kwanza dhidi ya Uruguay mnamo tarehe 15 mwezi Juni.
Salah, 25, alikutana na daktari huyo pamoja na rais wa shirikisho la soka nchini Misri Hany Abu Rida nchini Uhispania siku ya Jumatano.
Shirikisho hilo baadaye lilituma ujumbe wa Twitter likisema: Baada ya kukutana na Abu Rida pamoja na daktari wa timu ya taifa nchini Uhispania leo, Shirikisho la soka linathibitisha kuwa Salah atashiriki katika kombe la dunia, Mungu akipenda. Awali mshambuliaji huyo hakuwa katika hali ya kuweza kuzungumza zaidi na wanahabari wakati alipowasili nchini Uhispania kwa matibabu ya bega lake.Alipata jeraha katika mechi ya fainali ya vilabu bingwa ambapo timu yake ililazwa 3-1 na mabingwa wa kombe hilo Real Madrid wiki moja iliopita.
Salah alipata jeraha hilo alipokuwa aking'ang'ania mpira na beki wa Real Madrid Sergio Ramos.
Alilazimika kutolewa huku kukiwa na hofu ya iwapo ataweza kuichezea Misri katika fainali za kombe la dunia nchini Urusi mwezi ujao.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |