• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Ushirikiano wa mambo ya fedha wachangia maendeleo ya kasi ya ushirikiano kati ya China na Afrika

    (GMT+08:00) 2018-08-27 08:13:38

    Mwezi Desemba mwaka 2015, kwenye mkutano wa kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika FOCAC uliofanyika Johannesburg, Afrika Kusini, rais Xi Jinping wa China alitangaza kuinua kiwango cha uhusiano kati ya China na Afrika kuwa uhusiano wa wenzi wa ushirikiano wa kimkakati wa pande zote. Pia alitoa mipango 10 mikubwa ya ushirikiano katika sekta za viwanda, kilimo, miundombinu, fedha, maendeleo yasiyoleta uchafuzi wa mazingira, kurahisisha biashara na uwekezaji, kuondoa umaskini na kuboresha maisha ya watu, afya, utamaduni, amani na usalama. Katika kipindi cha leo, tunakuletea maelezo kuhusu ushirikiano wa mambo ya fedha kati ya pande hizo mbili.

    Kutokana na Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika na pendekezo la "Ukanda Mmoja na Njia Moja", katika miaka ya hivi karibuni ushirikiano katika mambo ya fedha umeendelea kwa kasi, na kuchangia maendeleo ya kasi ya ushirikiano kati ya pande hizo mbili katika nyanja mbalimbali. Hivi sasa China ni nchi inayowekeza zaidi katika nchi za Afrika, na kutoa mchango muhimu kwa ajili ya maendeleo ya uchumi wa nchi hizo. Mkurugenzi wa kituo cha utafiti wa mambo ya China cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaamu cha Tanzania ambaye pia ni mwanzilishi wa kituo hicho Bw. Humphrey P. B. Moshi anaona ushirikiano wa mambo ya fedha umenufaisha nchi za Afrika. Anasema,

    "Mwaka huu wa 2018, China imetimiza miaka 40 ya mageuzi yaliyoanza mwaka 1978 ya uchumi na kufungua mlango kwa ajili ya ushirikiano na mataifa ya nje. Sisi waafrika wamenufaika sana na mafanikio ya China katika miaka 40 iliyopita, ni kutokana na mafanikio yao ya kiuchumi yamewawezesha, na sasa wao wenyewe wamekuwa wawekezaji wakubwa, na wanakuja kuwekeza Afrika. "

    Naibu mkuu wa Chuo Kikuu cha Biashara na Nje cha China Bw. Ding Zhijie anaona ushirikiano wa mambo ya fedha ni muhimu kwa pande zote mbili, na ni hatua muhimu ya kusaidiana kiuchumi. Anasema,

    "Ushirikiano wa mambo ya fedha kati ya China na Afrika una mustakabali mzuri. Kwanza, uzoefu wa maendeleo ya uchumi wa China haswa mambo ya fedha katika miaka zaidi ya 40 iliyopita unaweza kuigwa na nchi za Afrika. Pili, China ina akiba kubwa ya fedha za kigeni, huku nchi za Afrika zikihitaji sana uwekezaji haswa katika sekta ya miundombinu, hivyo kuendeleza ushirikiano wa mambo ya fedha kutanufaisha uchumi wa China na nchi za Afrika. Na tatu, napendekeza kuhimiza sarafu ya China iwe fedha ya kimataifa, ili kupata fedha nyingi zaidi kuisaidia Afrika kuendeleza uchumi."

    Ili kuhimiza ushirikiano wa mambo ya fedha kati ya China na Afrika, China kwa nyakati tofauti ilianzisha mfuko wa maendeleo ya China na Afrika, na mfuko wa ushirikiano wa uzalishaji kati ya pande hizo mbili. Mbali na hayo China imejitahidi kutumia vizuri benki kubwa za China, ikiwemo Benki ya ununuzi na mauzo ya bidhaa ya China TEIBC. Naibu mkuu wa Benki hiyo Bw. Xie Ping amesema, hadi sasa benki hiyo imetoa mikopo kwa miradi zaidi ya 600 ya nchi 47 za Afrika, na kuunga mkono ushirikiano kati ya China na Afrika kuendelea kwa kina na kwa upana. Anasema,

    "Wakati tunapounga mkono ushirikiano kati ya China na Afrika, tunazingatia mahitaji halisi ya nchi za Afrika, na kuzisaidia hususan katika ujenzi wa miundombinu. Pia tumezisaidia nchi za Afrika kuwaelimisha watu ufundi wa kazi, na kupatia uzoefu na teknolojia. Zaidi ya hayo, tunazingiatia uhifadhi wa mazingira wakati tunapozisaidia kuendeleza uchumi, na kuzihimiza kampuni za China kuhifadhi uwiano wa viumbe na mazingira barani Afrika."

    Ushirikiano kati ya benki ni sehemu muhimu ya ushirikiano wa mambo ya fedha kati ya China na Afrika. Mwaka 2008 Benki ya viwanda na biashara ya China ICBC ilinunua asilimia 20 ya hisa ya Benki ya Standard ya Afrika Kusini. Naibu mjumbe wa kwanza wa ICBC barani Afrika Bw. Sun Gang amesema, madhumuni ya benki hiyo kununua hisa hizo ni kurahisisha shughuli zake za fedha barani Afrika, na katika miaka 10 iliyopita, benki hizo mbili zimetoa mikopo kwa miradi zaidi ya 30 mikubwa barani Afrika kwa pamoja. Anasema,

    "Tuna njia mbili za kufanya shughuli barani Afrika. Tunatoa mikopo ya moja kwa moja kwa miradi mikubwa haswa ujenzi wa miundombinu kama vile barabara, reli na vituo vya uzalishaji wa umeme. Njia nyingine ni kupitia Benki ya Standard, na tumetoa mikopo na huduma za fedha kwa miradi mingi barani Afrika kupitia benki hiyo."

    Ushirikiano wa fedha kati ya China na Afrika umeleta manufaa halisi kwa uchumi na watu wa Afrika. Katika miaka kadhaa iliyopita, China imetoa mikopo na uwekezaji kwa miradi mingi mikubwa barani Afrika, kama vile reli inayounganisha Nairobi na Mombasa, kituo cha kuzalisha umeme cha Karuma nchini Uganda na mradi wa gesi wa Tanzania, ambavyo vimeleta mabadiliko makubwa kwa maisha ya watu. Lakini baadhi ya vyombo vya habari vinasema mikopo ya China inaongeza mizigo ya Afrika, na kudhuru madaraka ya nchi za Afrika. Mkurugenzi wa kituo cha utafiti wa sera za Afrika cha Kenya Bw. Peter Kagwanja anasema,

    "Mtu ambaye hana deni, huyu ni maskini. Jambo muhimuni kwamba deni hilo ulilo nao ulifanya nini, ulinunua ng'ombe na mbuzi, au ulienda kunywa chang'aa. Sasa hili deni wachina kwa waafrika ni deni muhimu, kwa sababu linaenda kwa maendeleo ambayo vizazi vya sasa na vijao watafaidika. Wazungu walituuza sisi watumwa kama bidhaa, wamezoea miaka mingi. Sijui kwa nini wanaongea hivyo. Kuinuka kwa uchina ni manufaa makubwa kwa Afrika."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako