• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Rwanda yatarajia kuongeza mauzo kupitia Alibaba

    (GMT+08:00) 2018-11-02 10:42:02

    Serikali ya Rwanda imesema itatumia fursa ya makubaliano kati yake na kampuni ya Alibaba kuuza bidhaa zaidi kwenye soko la China na hivvyo kusaidia maelfu ya vijana wake kupata ajira.

    Rais wa nchi hiyo Paul Kagame ameongoza hafla ya kusaini makubaliano ya ushirikiano kati ya serikali na kampuni ya Alibaba iliofanyika kwenye mji mkuu Kigali.

    Ronald Mutie anaripoti.

    Wacheza ngoma za kitamaduni nchini Rwanda wakimkaribisha rais Paul Kagame na mwenyekiti wa kampuni ya Alibaba Jack Ma.

    Ni kwenye hafla ya kutiwa saini kwa mikataba ya maelewano kati ya serikali ya Rwanda na kampuni hiyo ya Alibaba, ambayo yatawezesha Rwanda kuuza bidhaa na huduma zake kwenye mtandao wa Alibaba.

    Rwanda ndio ya kwanza barani Afrika kuingia kwenye jukwaa la biashara ya mtandaoni duniani eWTP.

    Mikataba mitatu iliotiwa saini ni pamoja na kuweka bidhaa zaidi za Rwanda kama kahawa na vinyago kwenye mtandao wa alibaba na kutangaza vivutio vya utalii vya Rwanda kwenye mtandao maarufu wa Fliggy unaotumiwa na mamilioni ya watalii nchini China.

    Rais Paul Kagame akizungumza kwenye hafla ya kusaini makubaliano hayo anampongeza Jack Ma kwa imani yake katika biashara za Rwanda na kuwasaidia hasa vijana kupata jukwaa muhimu duniani la kuuza bidhaa zao.

    "Jukwaa la biashara ya mtandaoni duniani linafungua ukurasa mpya katika biashara ya mtandaoni na utalii kwa Rwanda, huku pia ikiimarisha uwezo na ushindani miongoni mwa wajasiriamali wetu. Wazalishaji wa Rwanda sasa wataweza kuuza moja kwa moja kwa kundi kubwa la wateja na kuepuka masharti mengi yenye gharama. Hiyo itaongeza uzalishaji na kuwaletea faida zaidi"

    Alibaba ikiwa na zaidi ya wateja nusu bilioni ndio kampuni kubwa zaidi duniani ya kuuza bidhaa mtandaoni.

    Pia ndio mtandao unaotumiwa na mamilioni ya wateja wa China kununua bidhaa za ubora wa hali ya juu kutoka kote duniani.

    Mbali na kupata wateja kwa haraka, wakulima na wadau wa kahawa nchini Rwanda pia wanapokea malipo ya juu kwa kilo moja ya bidhaa hiyo, ikilinganishwa na masoko kama vile Marekani.

    Kwa Mfano, Jack Ma anasema kilo moja ya kahawa ya Rwanda inamletea mkulima dola 8 ikiuzwa Marekani lakini ikiuzwa kupitia alibaba inamletea dola 12.

    "Kuanzia leo tutaifanya dunia ibadili mawazo yake kuhusu Rwanda na Afrika kwa jumla. Tunafurahi sana kuona kwamba tunauza kahawa ya Rwanda ndani ya muda mfupi. Tunataka kuthibitisha kuwa kama Rwanda inaweza kufanikiwa basi kwa nini sio nchi nyingine za Afrika "

    Kabla ya kutiwa saini kwa makubaliano haya tayari Rwanda ilikuwa imeanza kuuza kahawa yake kupitia kwa Alibaba.

    Na matokeo yake yanatia moyo, anasema mkurungezi wa halmashauri ya maendeleo ya Rwanda Bibi Clair Akamanzi.

    "Matumizi ya kahawa ya wachina yanaongezeka kwa asilimia 15 kwa mwaka ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 2 tu kote duniani. Shehena ya kwanza ya kahawa tuliopeleka China ilikuwa ni pakiti 1, 800 za gramu mia tano na baadhi ya kahawa hizo ziliuzwa zote siku ya kwanza. Marafiki zetu wachina wanaponunua kahawa ya Rwanda kupitia kwa mtandao wa Alibaba, watakuwa wananunua kahawa inayojulikana kwa ubora wake wa juu. Pia wazalishaji wa kahawa wa Rwanda wanapokumbatia mtandao wa Alibaba, nataka kuwahakikishia kuwa hilo ni soko linalokua kwa haraka na lenye manufaa ya muda mrefu.."

    Ushirikiano wa pande mbili pia unahusu mlipo ya mtandaoni kupitia kwa Alipay ambayo ndio jukwaa kubwa zaidi duniani la kulipia bidhaa na huduma kwa kutumia simu.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako