• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Upimaji wa hali ya HIV binafsi ni juhudi mpya za kupambana na HIV nchini Kenya

    (GMT+08:00) 2018-11-28 08:36:34

    Huku ulimwengu ukiadhimisha siku ya ukimwi duniani tarhe 1 desemba, nchi mbalimbali zimeendelea kuweka mipango ya kupambana na kuenea kwa ugonjwa huo.

    Nchini Kenya mwandishi wetu Ronald Mutie ametuandalia ripoti kuhusu jinsi upimaji binafsi wa HIV unasaidia kujitambua na kutoa matibabu kwa wale walioathirika.

    Je unaweza kujipima hali yako ya HIV ukiwa nyumbani?

    Ni swali ambalo kwa wengi linawajia kwa mshangao kwani labda hawajui kama kuna njia ya kufanya hivyo.

    Lakini hii ndio juhudi mpya ya kupambana na kuenea kwa HIV nchini Kenya.

    Sasa kwa kutumia vifaa maalum mtu yeyote anaweza kujipima hali yake akiwa faraghani na kuchukua hatua kulingana na matokeo yake.

    Shirika la kitaifa la kupambana na ukimwi na zinaa nchini humo NASCOP linaongoza juhudi hizo na sasa limefikisha vifaa hivyo kwa zaidi ya wakenya elfu nane.

    Meneja wa mipango kwenye shirika la NASCOP Bibi Mary Mugambi anaeleza mafanikio ya vifaa hivyo.

    "Imekuwa na mafanikio mazuri kwa sababu wale ambao wanaogopa kwenda hospitalini, wanaweza kujipima nyumbani. Wanawza kununua vifaa ambavyo vinauzwa kwa shilingi 500 (dola 5) usahihi wa vifaa vyetu ni asilimia 99 Njia ya kwanza ya kupima ni kwa kutumia damu ambayo unatoa kwenye kidole na kuweka kwenye kifaa na kumwagia kimunyifu halafu unasubiri matkeo baada ya dakika 5-10. Na njia nyingine ni ya kutumia chembe za mdomoni kufanyia upimaji na kusoma matokeo. "

    Bibi Mugambi amansema kwa sasa vifaa hivyo vinapatikana katika maduka 320 ya kuuza dawa kote nchini humo na asilimia 60 vinanunuliwa na wanaume.

    Lakini sio watu wote wanaopendelea njia hii ya kujipima binafsi hali ya HIV.

    Wengine kama Bwana Joseph Mwaura anaona kuwa kujipima bila kupata ushauri kabla, kunaweza kumletea mwathiriwa athari mbaya.

    "Sioni kama ni teknolojia zuri kwa sababu serikali haitapata idadi kamili ya wale wenye HIV. Na nikijipia nipate kwa mafano niko nayo, sitaweza kujipatia ushauri ikilinganishwa na kwenda hospitalini."

    David Ongechi anaona ni njia zuri ya kujitambua na kuanza matibabu kwa siri yako.

    "Mimi naona kama ni kitu mzuri kwa sababu watu wengine wanaogopa kwenda hospitali. Lakini ukijipima wewe mwenyewe unajua hali yako na kama umeathrika unaanza kumeza madawa."

    Lakini ili kuondoa hofu kama ya bwana Mwaura, shirika la NASCOP limeweka mipango ya kuwezesha watu kujipima na pia kupata msaada wakati wowote wanapohitaji.

    Pia maelezo ya huduma za kujipma hali ya HIV zinaweza kupatikana kwenye app ya Be Sure ambayo ina lahaja sita

    Bibi Mary Mugambi.

    "Wakati mtu amepata virusi vya Ukimwi tunamwingiza kwenye mpango wa utunzaji na hapo ndio tutaanza matibabu. Anaaza kupewa ARV na tunapeana ushauri kuhusu kula lishe bora, kuishi na virusi, kupima wapenzi au mpenzi mwenzake na watoto. Na pia tumewekamifumo ya kutoa misaada inayoweza kusaidia mtu akiwa nyumbani kwa njia ya kupiga simu au kutazama video"

    Taakwimu zinaonyesha kwamba watu milioni 1.5 kati ya milioni 42 nchini Kenya wana virusi vya HIV.

    Lakini pia karibu robo ya idadi ya watu hawajapima kuhakikisha hali yao.

    Njia mpya hii ya kujipima hali ya HIV huenda ikasaidia kukusanya taakwimu kamili, lakini bado kuna changamoto.

    Bibi Esther Chude ni mkurungezi wa wa chama cha wauzaji madawa nchini Kenya ambacho kilishirikiana na serikali kuanzisha mpango huu.

    "Changamoto yetu imekuwa kwanza ni bei ya vifaa hivyo na ya pili ni kwamba tunahitaji kuwajulisha watu wengi iwezekanavyo kuhusu huduma hii na hivyo tunatafuta washirika wa kutusaidia kufikia watu wengi."

    Maudhui ya siku ya ukimwi duniani mwaka huu ni "Jijue hali yako" na hapa nchini Kenya mashirika husika yanatoa wito hasa kwa wanaume kupimwa au kujipima ili kujua hali yao.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako