Tangu Kenya ijinyakulie uhuru wake mwaka wa 1963, hakuna mradi wowote uliopo kwa sasa ambao unaeza ukalinganishwa na mradi wa reli mpya ya kisasa ya SGR. Kufikia sasa, reli hii mpya imewahudumia mamilioni ya wakenya, kutoka Mombasa hadi Nairobi, na Nairobi hadi Mombasa. Awamu ya pili ya mradi huu inaendelea, kutoka Nairobi hadi Naivasha. Baadaye, reli hii itaenda hadi Kisumu. Tangu ujenzi wa mradi huu uanze, maelfu ya wakenya wamefaidika pakubwa mno kwa ajira. Kando na ajira, uchumi wa taifa la Kenya pia umepigwa jeki haswa ikizingatiwa kuwa usafiri wa bidhaa za biashara umerahishwa kupitia treni ya mizigo. Na kama anavyoelezea Rais Uhuru Kenyatta, mradi wa Ukanda mmoja, Njia moja una umuhimu mkubwa sana, si kwa Kenya pekee, bali bara zima la Afrika.
Nadhani ni swala la umuhimu mkubwa sana.Kwa sababu angalia malengo yake. Malengo yake ni yapi? Kwanza kabisa, malengo yake ni kufungua uchumi wetu kwa biashara. Lengo ni kuendeleza biashara kati yetu na kutuunganisha na mataifa ya Asia, sehemu za Uropa, mataifa ya Uarabuni, na kuunganisha bara la Afrika,kutoka Afrika Mashariki hadi Afrika Magharibi. Nina imani kuwa mradi huu una uwezo mkubwa wa kuwafaidi wahusika wote. Ndio sababu kuu tuko makini sana kama taifa, na bara zima la Afrika kwa jumla kushirikiana kwa karibu sana na China, kwenye mradi huu.
Kando na reli mpya ya kisasa, wachina pia wanajihusisha na ujenzi wa miradi mingini hapa Kenya na mataifa mengine Afrika. Yote haya yanahitaji ufadhili. Ili kuafikia matarijio yao, bara la Afrika limekuwa rafiki mkubwa na wa karibu sana na taifa la China, ambalo linafadhili miradi mikubwa. Rais Uhuru Kenyatta anaelezea kuwa, sekta za kibinafsi vile vile zimehusishwa pakubwa kwenye mradi huu wa Ukanda Mmoja, Njia moja. Anaelezea.
Tunafanya kazi na washirika waliostawi. Tangu China ianze kujihusisha na Kenya na Afrika, tumeshuhudia maendeleo mengi sana ya ujenzi kote barani Afrika. Nilivyosema hapo awali, tuna washirika waliostawi wanaojihusisha na baadhi ya miradi. Kando na hili, kuna baadhi ya miradi ambayo tunahusisha sekta za kibinafsi. Kwa hivyo uhusiano na ushirikiano mwema kati ya serikali na sekta za kibinafsi utarahisha baadhi ya mambo na kuhakikisha kwamba miradi mingi inamalizika kwa wakati unaofaa. Ufadhili wa miradi tuliyo nayo, utakuwa ushirikiano wa sekta za kibinafsi na serikali ili kuhakikisha kwamba miradi inakamilika hapa kenya na hata Afrika nzima.
Ushirikiano wa karibu kati ya mataifa mengi ya Afrika na taifa la China unatarajiwa kubadilisha na kuinua maisha ya waafrika wengi, haswa swala zima la miundo msingi.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |