• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • China yaeleza matumaini ya muafaka katika mgogoro wake wa kibiashara na Marekani

    (GMT+08:00) 2019-03-15 19:51:55

    Serikali ya China imeelezea kuwa changamoto zilizojitokeza katika biashara baina yake na Marekani haziwezi kuathiri mahusiano ya kibiashara na mataifa mengine.

    Hata hivyo, imeendelea kusisitiza kuwa na matumaini kwamba changamoto zilizojitokeza zitatatuliwa kwa manufaa ya ustawi wa kibiashara na mahuisuano ya pande zote mbili.

    Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa jijini hapa, Waziri Mkuu wa China Bw. Li Keqiang amesema China na Marekani wamekua washirika wa muda mrefu katika nyanja za biashara, maendeleo na diplomasia, hivyo wana matumaini mahusiano hayo yataendelea kudumishwa na kuleta tija.

    "Tumekuwa na mahusiano mazuri na Marekani kwa muda mrefu, sidhani kama changamoto hizi zitaleta athari kwa washirika wetu wengine, hata hivyo naamini bado kuna nafasi ya kuzungumza na kumaliza haya yote yaliyojitokeza," alisema Li.

    Alisisitiza kwamba nchi yake itaendelea kufuata mikataba na miongozo ya kimataifa katika nyanja zote za kimahusiano kwa manufaa ya pande zote zinazohusika.

    Kauli yake imekuja siku chache baada ya Marekani kufungulia mashitaka kampuni kubwa ya mawasiliano na usambazaji wa simu duniani ya Huawei yenye makao makuu yake nchini China kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha, kuzuia utekelezaji wa haki na wizi wa teknolojia.

    Katika mkutano wake na wanahabari ambao ulifanyika muda mfupi baada ya kuahirishwa kwa kikao cha bunge ambacho kilianza Jumanne iliyopita kwa lengo la kupokea ripoti ya kazi za serikali kwa mwaka 2018 na mapendekezo ya kazi za mwaka 2019, Waziri mkuu wa China Bw. Li Keqiang alisema mwaka huu serikali imedhamiria kuboresha zaidi mazingira ya wafanyabiashara kwa lengo la kukuza uchumi.

    Alisema serikali itaondoa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kati ya asilimia moja na tatu kwa wenye viwanda vikubwa na vya kati.

    "Pia tumeweka msisitizo kwenye kutengeneza ajira, kupambana na uzalishaji na uuzaji wa bidhaa zisizokidhi viwango na kuboresha utoaji huduma kwa umma," alisema.

    Katika vikao vilivyohitimishwa leo, wabunge pia walipitisha muswada wa sheria ya uwekezaji ambayo utawasaidia wawekezaji kutoka nje ya China kufanya biashara kwa uhuru bila vikwazo.

    Muswada huu utawezesha wawekezaji wa kigeni kuweza kuanza kutuma faida watakazozitengeneza hapa kwenda katika nchi zao.

    Hii ina maana kuwa, Serikali ya China haitaingilia biashara za wageni lakini pia sheria hii italinda wawekezaji wazawa kutodhurumiwa na kwamba hawatakua wanalazimika kuhamisha teknolojia zao kwa serikali.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako