Watu wanaoishi na ulemavu wa ngozi nchini Kenya, wameomba kutambuliwa katika zoezi la kuhesabu watu linaloendelea nchini humo. Wakingozwa na mwenyekiti wao Ddt. Isaac Mwaura watu hao wamesema pia kuhesabiwa kwao kutakisaida chama chao kuwafuatilia na kuhakikisha wanapata nafasi na huduma za serikali kama raia wengine.
Issac Mwaura ambaye pia ni Seneta, ni mtetezi wa watu wanaoishi na ulemavu wa ngozi nchini Kenya. Kwenye zoezi la sensa linaloendelea nchini humo, ameongeza sauti yake kutaka watu wanaoishi na ulemavu huo wajumuishwe zaidi katika jamii na serikali na haki zao ziliindwe zaidi.
Kama ilivyo katika nchi nyingi za Afrika, watu wenye ulemavu wa ngozi hubaguliwa na hata kuuwawa kutokana na imani za kishirikina. Tangu mwaka wa 2009 chama cha watu wenye ulemavu wa ngozi nchini Kenya kimekuwa kikipigania kupitia bunge haki za kutambuliwa na pia kupata bila malipo baadhi ya bidhaa za matumizi maalum kama vile mafuta.
Katika bajeti ya mwaka 2019 na 2020 serikali ya Kenya ilitenga dola milioni moja kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa ngozi na kwa jumla dola milioni 2 kwa hazina ya watu wanaoishi na ulemavu. Pia mashirika mbali mbali pamoja na serikali zinatoa misaada yao kupitia baraza la kitaifa la albino, bila kufahamu idadi kamili baadhi ya waathirika hukosa huduma muhimu zinazotolewa bila malipo na baraza hilo.
Ingawa sio watu wengi wenye ulemavu wa ngozi walio katika nafasi za uongozi, lakini kutokana na kampeni za chama chao sasa watoto wengi wanajiunga na vyuo vikuu kusomea taaluma mbali mbali.
Takwimu zilizotolewa na baraza la kitaifa la albino zimeonyesha kuwa, hadi sasa kuna watu 3,500 hivi wenye ulemavu wa ngozi nchini Kenya.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |