Kamati ya Tuzo za Nobel ya Norway jana ilimtangaza Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed kama mshindi wa tuzo ya Nobel ya amani mwaka 2019 kwa juhudi zake za kutatua mgogoro wa mpaka na majirani zao Eritrea.
Akitoa tangazo hilo huko Oslo mwenyekitit wa kamati Berit Reiss-Andersen amesema wakati Abiy Ahmed amekuwa waziri mkuu Aprili 2018, aliweka wazi kwamba anataka kurejesha mazungumzo ya amani na Eritrea na mbali na hapo Bw. Abiy pia ameanzisha mageuzi muhimu nchini Ethiopia ya kuinua viwango vya maisha ya watu nchini.
Wakati huohuo ofisi ya waziri mkuu wa Ethiopia nayo imetoa taarifa ikisema ushindi wa tuzo ya Nobel wa Bw. Abiy ni ushuhuda usio na mwisho, wa juhudi zake kubwa za kuleta umoja, ushirikiano na kuishi kwa pamoja ambazo amekuwa akizipigania. Taarifa hiyo imeongeza kuwa tuzo hiyo pia inaonesha kuwatambua wadau wote waliojitahidi kuleta amani na maelewano nchini Ethiopia na katika kanda za Mashariki na Kaskazini mashariki mwa Afrika.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |