Ethiopia inatarajia kuwa kitovu muhimu cha biashara ya mtandaoni barani Afrika baada ya kusaini makubaliano ya kuanzisha kituo cha biashara ya mtandao ya Kimataifa eWTP na kampuni ya Alibaba ya China.
Kituo hicho kitajengwa katika mji mkuu Addia Ababa na ni cha kwanza cha aina yake barani humo.
Hafla ya kusaini makubaliano hayo imehudhuriwa na waziri mkuu wa Ethiopia Aby Ahmed, mwanzilishi wa kampuni ya Alibaba Jack Ma miongoni mwa maafisa wengine wa ngazi ya juu kutoka pande zote mbili.
Kulingana na makubaliano hayo, kituo hicho cha eWTP kinakusudiwa kuwezesha biashara baina ya nchi mbalimbali na kutoa mafunzo kwa wajasiriamali hasa vijana.
Jack Ma, akihutubia washiriki wa uzinduzi huo anasema sasa ni wakati wa Afrika wa kujinufaisha na utandawazi kupitia biashara ya mtandaoni.
"Awali tulikuwa tunaamini mambo kama, made in China ama made in Amerika, lakini siku za baadaye tutaamini made in Internet. Awali Afrika ilijulikana kama eneo la kununua mali ghafi tu , lakini sasa tunaamini kuwa Afrika imejiunga na utandawazi na inachangia kuunda mfumo mpya wa biashara. Awali dunia ilitawaliwa na kampuni 6,000 kubwa duniani lakini sasa kupitia eWTP tunalenga kusaidia kampuni ndogondogo kati ya milioni 6 na 60 kujiunga kwenye biashara ya mtandaoni duniani hasa vijana.Naamini kuwa biashara ndogondogoo hapa nchini Ethiopia vijana na wajasiriamali, watajiunga na biashara za kote duniani na kufanya ushirikiano kutokana na uwezeshaji wa biashara na uchumi wa kidijitali"
Ethiopia ni nchi ya pili barani Afrika kuanzisha kituo cha eWTP baada ya vituo sawa na hicho kuanzishwa pia nchini Malaysia, Ubelgiji na Rwanda.
Mpango mkubwa wa kwanza wa ushirikiano wa eWTP nchini Ethiopia utakuwa ni kuanzisha kituo ya cha biashara cha dijitali kutumika kama lango la bidhaa za Ethiopia kwenda China.
Bwana Getahun Mekuria ni waziri wa uvumbuzi na teknolojia
"Leo ni siku muhimu kwa uchumi unaokuzwa kupitia mifumo ya dijitali hapa nchini Ethiopia. Kituo kipya cha kibiashara kitakachojengwa hapa kitatumika kuuza bidhaa kwa jumla na pia reja reja. Awamu ya kwanza ya kituo hicho cha dijitali itahusisha ujenzi wa maeneo mbalimbali ya biashara, eneo la wazi la kufanya maonesho, kituo cha mafunzo kuhusu biashara ya kidijitali na kile cha Alibaba cha usimamizi wa hali ya juu. Ushirikiano wetu na Alibaba utasaidia kukuza biashara ya aina mpya sio tu nchini Ethiopia lakini pia na kote barani Afrika"
EWTP ilipendekezwa na Jack Ma lengo lake likiwa ni kuweka jukwaa la wazi la biashara za kibinafsi na uratibu kati ya mashirika ya kimataifa, serikali na vikundi vya kijamii vyenye biashara ndogo na za wastani.
Ethiopia ikiwa na zaidi ya watu milioni 100 ni ya pili kwa wingi wa watu barani Afrika.
Utamaduni wake wa kipekee na utalii vinavutia mamilioni ya wageni kila mwaka.
Lakini bado kutokana na kwamba haijapana na bahari uwezo wake wa kufanya biashara na nchi nyingine unasalia kuwa wa chini.
Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed anaona kwamba ushirikiano wa nchi yake na kampuni kama Alibaba utasaidia kufungua sio tu nafasi za ajira lakini pia nchi yenyewe kama kituo muhimu cha biashara ya aina mpya.
"Kupitia kwa mipango kama hii, Ethiopia na Jack Ma kupitia Alibaba, tutafanikisha maono yetu. nimemwakikishia Jack Ma leo kwamba nitakuwa kama afisa wa uwekezaji wa Alibaba hapa nchini Ethiopia na pia afisa wa mauzo kote barani Afrika. Ethiopia inatarajia kuendeleza na kufanikisha mipango ya kituo cha kibiashara ya mtandao yaani eWTP na uchumi wa dijitali kwa kuwekeza kwenye miundo mbinu husika"
Mbali na mipango kama huu wa eWTP, mfuko wa Jack Ma umeanzisha shindano la kutoa mitaji kwa wajasiriamali bora barani Afrika.
Shindano la kwanza limefanyika mwaka huu nchini Ghana ambapo dola milioni 10 zilitolewa kwa washindi mbalimbali.
Na jumatatu akiwa mjini Ethiopia Jack Ma ametangaza kuwa, mfuko wake utaongeza fedha za kusaidia wajasiriamali barani Afrika kutoka dola milioni 10 hadi dola milioni 100.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |