Rais Ismail Omar Guelleh wa Djibouti na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Bw. Mahamoud Ali Youssouf kwa nyakati tofauti wamekutana na waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Wang Yi ambaye yuko ziarani nchini Djibouti.
Kwenye mazungumzo yao, rais Guelleh amesema, uhusiano kati ya Djibouti na China umeendelezwa kwa kina na kupata mafanikio makubwa. Amesema Djibouti inaishukuru serikali ya China na wananchi wake kwa kuunga mkono maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini humo, na pia inatarajia kushiriki kwenye ujenzi wa "Ukanda Mmoja, Njia Moja", na kutekeleza miradi ya Hatua Nane zilizotolewa kwenye Mkutano wa kilele wa Beijing wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika FOCAC.
Kwa upande wake, Bw. Wang Yi amesema China na Djibouti siku zote zinaheshimiana, kuungana mikono na kusaidiana, na zimekuwa mfano wa kuigwa wa ushirikiano wa kunufaishana kati ya nchi kubwa na ndogo. Amesema China itaendelea kupanua ushirikiano na Djibouti kwenye sekta mbalimbali, na pia itaendelea kuunga mkono maendeleo ya Djibouti kadri iwezavyo.
Bw. Wang Yi pia alikutana na mwenzake wa Djibouti Mahamoud Ali Youssouf na kubadilishana maoni kuhusu uhusiano na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |