Kundi la 20 la madaktari wa China linaendelea kutoa huduma za afya katika hospitali ya urafiki ya China na Uganda mjini Kampala, ikiwa ni sehemu ya moango wa serikali ya China wa kuendelea kusaidia Afrika kuboresha sekta yake ya afya.
Kundi hilo la madaktari 9 wanatoa matibabu kwa vitengo 8 vikiwemo upasuaji, magonjwa ya kuambukiza na akiupanja.
Kwenye kipindi chetu cha daraja hivi leo Ronald Mutie anaripoti kuhusu madaktari hao na kazi zao huko Uganda.
Hapa ni katika hospitali ya Urafiki ya Uganda na China katika mji mkuu Kampala.
Wagonjwa wanasubiri ikwenye foleni na wengine tayari wamepokea matibabu na wanatoka kuelekea nyumbani.
Kama ilivyo kwenye nchi nyingi zinazoendelea, uwekezaji kwenye sekta za afya unasalia kuwa wa chini ya asilimia tano ya pato la kitaifa inayopendekezwa na shirika la Afya duniani WHO.
Lakini kupitia ushirikiano na nchi nyingine, Uganda inajitahidi kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa njia ya kisasa na gharama nafuu zaidi.
Mojawepo wa juhudi hizo zinaonekana kupitia kwa ushirikiano na China ambayo imekuwa ikituma kundi la madaktari hapa tangu mwaka 1983.
Pia China imesaidia ujenzi wa hospitali hii na kuchangia baadhi ya vifaa.
Dkt. Wang Hu ndiye mkuu wa ujumbe wa madaktari wa kikosi cha awamu ya 20.
"Mimi ni mtaalam wa kushughulikia uvimbe na nchini china nafanya kazi katika kitengo cha kutibu uvimbe Hospitali ya mkoa wa Yunan. Nina uzoefu wa kufanya upasuaji kwenye eneo la kati yam domo na shingo. Nimefurahi sana kuja hapa kufanya kazi na madaktari wa Uganda lakini pia kuhudumia wenyeji. Ni hisia muhimu kwetu kufanya kazi hapa ikizingatiwa kuwa miaka 36 iliopita madaktari wa China walianza kuja Uganda kutoa huduma na imekuwa ni histori ndefu "
Siku moja iliopita Daktari Wang amemfanyia upasuaji mgonjwa aliyekuwa na uvimbe shingoni.
Leo anapitia kwenye wodi kumjulia hali.
Hali yake ni zuri na ataondoka kwenda nyumbani muda wowote.
Daktari Wang anaeleza kuwa muda wa kufanya upasuaji umepungua na vifaa wanavyotumia kutoka china ni vya kisasa.
"Tumeotoa uvimbe wa kilo sita, ulikuwa mkubwa sana. Vifaa na bidha za upasuaji zimetoka China bila malipo.Wakati wa upasuaji kwa huyu mgonjwa alitokwa na damu kidogo sana. Pia muda wa upasuaji ulikuwa mfupi kama dakika 45 hivi ikilinganishwa na kitambo ambapo upasuaji ungechukua saa moja na nusu.
Namatovu Josephine ni dada yake.
"Nilimleta hapa jumatao kwa sababu alikuwa na uvimbe kwenye shingo. Daktari wa China alimfanyia upasuaji. Jana usiku amekohoa na kuumwa kidogo lakini sasa amepata nafuu. Daktari wa kichina amemfanyia upasuaji vizuri. Nasubiri nione vile atakavyokuwa lakini natarajia kwenda nyumbani kesho"
Kwa jumla kundi la madaktarai wa china wanatoa huduma katika vitengo 8 vikiwemo Acupuncture upasuaji wa aina mbalimbali Magonjwa ya Kuambukiza na kutoa huduma za jamii.
Akiupancha ni aina ya matitabu maalum ya China ambapo mtaalam anadunga sindano kwenye maeneo tofauti mwilini ili kupunguza na kuponya maumivu.
Kwenye chumba cha matibabu ya akiupancha nampata Daktari Xu Hong akimtibu Anthony Ntesijayo mwenye umri wa miaka 60.
"Kila siku natoa matibabu kwa watu 15. Watu wengi wa Uganda hawajafahamu vizuri kuhusu matibabu ya akiupancha. Wanaamini tu kwamba unapodungwa zile sindano maumivu yanaisha lakini hiyo sio kweli. Akiupancha sio kwa ajili ya maumivu ya mwili tu, lakini inaweza kutumika kutibu homa, kiharusi, kumwa na kichwa na magonjwa mengine mengi. Lakini wengi wa wagonjwa wanakuja hapa kwa sababu ya uchungu mwilini tu. Nadhani tutatoa ufahamu zaidi kwa wenyeji ili waelewe mchakato wa matibabu ya akiupancha"
Anthony ni miongoni mwa wagonjwa zaidi ya 300 wanaokuja hapa kila mwezi kupata aina hii ya matibabu ya kichina.
Anasema ingawa akiupancha sio maarufu nchini Uganda lakini athari zake zimemsaidia kupata nafuu haraka.
"Nimekuwa nikiumwa kwa miaka kumi hivi, Naumwa sana na mikono na miguu. imekuwa ikiniuma kwa muda mrefu lakini nilipofika hapa sasa naanza kupata nafuu. nakuja Ijumaa kwa sababu siku nyingine nashughulika kutafutia jamii yangu chakula. matibabu yote ya acupuncture Napata bila malipo."
Kulingana na shirika la afya duniani WHO maisha ambayo mtu anatarajiwa kuishi wataki wa kuzaliwa nchini Uganda yaliongezeka kutoka miaka 45.7 hadi miaka 62.2 kwa wanaume na miaka 50.5 hadi miaka 64.2 kwa wanawake katika kipindi cha 1991 hadi 2014.
Uganda pia ilitimiza mojawepo wa malengo yake ya milenia katika sekta ya afya ya mtoto; kati ya 1990 na 2015, kiwango cha vifo vya watoto chini ya tano kilishuka kutoka 187 hadi 55 kwa kila watoto 1,000 walio zaliwa.
Hata hivyo mzigo wa magonjwa nchini Uganda unaongozwa na magonjwa ya kuambukiza, ambayo ni zaidi ya 50%.
Hayo ni pamoja na Malaria, VVU / UKIMWI, Kifua kikuu, magonjwa ya kupumua, magonjwa yanayoweza kuzuiwa kwa chanjo ambayo yanaongoza kwa usababishaji wa vifo.
Pia kuna kuna ongezeko la magonjwa yasiyoweza kuambukiza kama vile ya kiakili.
Daktari Xia Li amekuja kushirikiana na wenzake hapa kukabili maradhi yanayoambukizwa.
"Nimekuja kusaidia kwenye kliniki ya magonjwa ya kuambukiza. Hasa mimi nashughulikia magonjwa kama vile HIV, kifua kikuu. Tunafanya kazi kwa kushirikiana na madaktari wenyeji na naona inasaidia kwa sababu kutibu magonjwa ya kuambukiza hapa ni vigumu ikilinganishwa na China. Kila wiki naenda siku nne kwenye kliniki ya HIV na kifua kikuu. Kwenye kliniki ya HIV nahudumua watu 30 kwa siku na watu 20 kwenye kliniki ya kifua kikuu. Hakuna tatizo la mawasiliano kwa sababu karibu asilimia 90 ya wagonjwa wanaweza kuzungumza kiingereza vizuri"
Na kama ilivyo na wachina wengi ambao hawajawahi kutembelea Afrika, mara ya kwanza wazazi na marafiki wa daktari Xia Li walikuwa na wasiwasi.
Lakini baadaye alipofika na kuwaeleza hali halisi walimtia moyo kufanya kazi huko.
Anasema.
"Kabla sijaondoka jamaa zangu walikuwana wasiwasi kuhusu usalama wangu, na jinsi nitaendesha maisha ya kawaida kila siku kwa sababu niko mbali na nyumbani. Lakini nilipofika hapa nilianza mara moja kuwasiliana nao kwa njia ya wechat. Lakini nilipofika hapa nilianza mara moja kuwasiliana nao kwa njia ya wechat na kuwaonesha wazazi wangu mazingira ya huku na wakasema ni mazuri zaidi kuliko walivyofikiria.mara nyingi niliwaambia hadithi kuhusu kazi na vile ninayofanya kazi. Baadaye walinitia moyo na kunitaka nifanye kazi zaidi kuwasaida wagonjwa"
Kuwepo kwa madaktarai hawa hapa Uganda ni sehemu ya juhudi za China za kushirikiana na Afrika kuboresha sekta ya afya.
Pia ni sehemu ya hataua 8 zilizotangazwana Rais wa China Xi Jinping katika kikao cha ufunguzi cha Mkutano wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika Beijing Septemba mwaka 2018.
Lengo la madaktari hao mbali na kutoa huduma zao ni kupitisha utaalam wa China kwa madaktari wenyeji.
Dkt Daniel Mugabi ni mmoja wa madaktari kwenye hospitali hii wanaonufika moja kwa moja na mafunzo kutoka kundi la madaktari wa China.
"Nimefurahia kufanya kazi nao, tunapokuwa kwenye chumba cha upasuaji wanafuata hatua kwa hatua wkitufunza jinsi ya kufanya upasuaji. Tunapopata changamoto wakati wa upasuaji wanatusaidia na pia wametusaidia na madawa ambayo hatukuwa nayo. Hadi sasa kwa pamoja tumefanyia upasuaji wagonjwa watano. Kuna wengine kwenye ratiba na tutaendelea kushirikiana. Nina bahati sana kufanya kazi nao"
Kila mwaka hospitalihii inahudumia zaid ya wagonjwa 150,000.
Kuna madaktari bingwa 36 na manesi 102.
Emmanuel Batibwe, Mkurugenzi wa Hospitali ya Urafiki ya Uchina na Uganda anasema wana mipango ya kuongeza vitanda kutoka 100 hadi 250.
Pamoja na mipango hiyo,
"Tunapanga kuanza kupeleka baadhi ya madaktarai wetu nchini China kupata ujuzi wa kutibu magonjwa mbali mbali. Kwa sasa wamekuja na madawa ya thamani ya shilingi bilioni 3 na tunawaongezea bilioni 2. Tunafanya kazi chini ya mkataba kati yetu na serikali yua China ambapo madaktari wa China wanatoa msaada wa matibabu katika upasuaji, magonjwa ya kuambukiza na pia msaada wa kiufundi."
Kulingana wizara ya fedha, Uganda ilitenga shilingi trilioni 2.6 kwa sekta yake ya afya kwa kipindi cha fedha cha mwaka 2019/20.
Lakini wakati huo huo hospitali nyingi za serikali zinakabiliwa na upungufu wa wauguzi wa kuhudumia zaidi ya watu milioni 42 nchini humo.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |