Cameroon leo imethibitisha kuwa na kesi ya kwanza ya virusi vya korona (COVID-19), na kuifanya kuwa nchi ya nne baada ya Nigeria, Senegal na Afrika Kusini kuripoti kesi ya ugonjwa huo hii leo katika kanda ya Afrika kusini mwa Sahara.
Wizara ya Afya ya Umma ya Cameroon imethibitisha kesi ya kwanza ya maambukizi ya virusi vya korona (COVID-19) hii leo. Wizara hiyo imesema, mgonjwa huyo ni mwanaume raia wa Ufaransa aliyewasili Yaounde Februari 24. Mgonjwa huyo kwa sasa amewekwa kwenye sehemu maalum katika Hospitali ya Yaounde kwa matibabu, pia imeutaka umma kuwa makini na kuheshimu kanuni za usafi.
Nchini Afrika Kusini, serikali imepeleka jopo la wataalam na madaktari wa magonjwa ya kuambukiza kufanya uchunguzi mkoani KwaZulu-Natal, ambako mgonjwa wa kwanza wa COVID-19 aligunduliwa. Mgonjwa huyo alirejea nchini Afrika Kusini akitokea nchini Italia.
Nayo serikali ya Nigeria imeyataka mashirika yote ya ndege yanayoendesha safari za kimataifa na kikanda kuwapa abiria na wahudumu fomu ya kuripoti afya kabla ya kuwasili katika viwanja vya ndege ili kufahamu hali ya afya ya watu wanaoingia nchini humo. Alhamisi iliyopita, Wizara ya afya ya Nigeria ilithibitisha kumkuta mgonjwa wa COVID-19 aliyeambukizwa virusi kabla ya kuingia nchini humo.
Nchini Senegal, Wizara ya Afya na Mipango ya Jamii ya nchi hiyo Jumatano ilitoa taarifa ikisema, hadi kufikia usiku wa siku hiyo, nchi hiyo ilikuwa imeshuhudia kesi nne za virusi vya korona, na wagonjwa wote ni raia wa kigeni. Rais Macky Sall wa Senegal amekubali kutenga dola za kimarekani milioni 2.4 kukabiliana na maambukizi hayo.
Wakati huohuo, nchi nyingine za Afrika kusini mwa Sahara ambazo hazijaripoti kesi za COVID-19 zimejiandaa kukabiliana na ugonjwa huo.
Alhamisi, serikali ya Kenya ilianzisha kituo cha karantini na matibabu kwa ajili ya kesi zinazoshukiwa kuwa na maambukizi ya COVID-19 mjini Mombasa, huku nchini Zimbabwe, Wizara ya Afya ya nchi hiyo ikiimarisha nguvu ya ukaguzi kwenye vituo vyote vya forodha. Nayo serikali ya Zambia imethibitisha kuanzisha mfuko wa dharura ili kukabiliana na matukio yanayoweza kutokea ghafla kuhusiana na COVID-19 na pia kuimarisha hatua za kukinga na kuzuia virusi hivyo.
Kwa mujibu wa mkurugenzi wa Kituo cha Kudhibiti na Kukinga Magonjwa cha Afrika CDC John Nkengasong, kimeanzishwa kikosi kazi cha kukabiliana na COVID-19 chenye wataalam kutoka nchi tano za Senegal, Kenya, Morocco, Nigeria na Afrika Kusini. Wataalam hao wamepewa majukumu ya kusimamia hali ya maambukizi ya COVID-19, kukinga na kudhibiti, na kushughulikia kazi za hospitali na usimamizi wa maeneo ya makazi.
Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Afya ya Umma iliyo chini ya CDC Afrika Tajudeen Raj amesema kuwa China imetoa msaada kwa kikosi kazi hicho, na kwamba China CDC imepeleka mshauri mwandamizi wa kiufundi katika kituo hicho ili kushirikiana kwa karibu na wataalam wa Afrika, haswa kuunga mkono kazi za kupambana na COVID-19 barani Afrika.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |