Siku hizi, kuna watoa maoni wengi wametumia methali ya Kiswahili ya "Tembo mbili wakipigana zinazoumia ni nyasi" kueleza wasiwasi wao kuwa kama China na Marekani zinapopambana, nchi za Afrika zitaumia.
Lakini kwa maoni yangu, wasiwasi huo hauna msingi. Katika historia ya mawasiliano kati ya China na Afrika, China haijawahi kujigamba kama Tembo, sembuse kuchukulia nchi za Afrika kama nyasi na kuzikanyaga. Kinyume chake, China siku zote imetetea kuwa nchi zote kubwa ama ndogo, yenye nguvu ama dhaifu, tajiri ama maskini ni sawa katika jumuiya ya kimataifa, na zinapaswa kuheshimiana, kutendeana kwa usawa na kusaidiana kwa dhati. Kwani katika mtazamo wa China, katika enzi ya utandawazi inayopendekeza ujenzi wa jumuiya ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja, nchi yoyote haiwezi kuwa kisiwa, wala haiwezi kujigamba kuwa juu ya nyingine. Maambukizi ya virusi vya corona yanayoendelea duniani yamethibitisha jambo hilo vya kutosha.
Tangu virusi vya corona vilipuke China, nchi za Afrika na mashirika ya kikanda yametoa uungaji mkono wa kisiasa kwa China kwa njia mbalimbali. Mabalozi wa nchi 13 za Afrika Mashariki mapema mwezi huu walitoa taarifa ya pamoja wakiipongeza China kwa kufanikiwa kuzuia kuenea kwa virusi, jambo ambalo limehakikisha usalama na afya ya wanafunzi wa nchi za Afrika waliopo China, na ni mchango kwa binadamu wote. Serikali, makampuni na asasi za kiraia za nchi nyingi za Afrika pia zimechanga pesa taslimu na msaada wa vitu kwa China. Hivi sasa maambukizi yanaenea na kulipuka katika nchi mbalimbali duniani, China imetoa ushirikiano wa kimataifa kwa haraka na kutoa msaada kwa nchi za Afrika na mashirika ya kikanda kadri iwezavyo. China imetoa vifaa vya kupima virusi vya corona na vifaa vya kujikinga na virusi kwa Kituo cha Kudhibiti na Kukinga Magonjwa Afrika CDC, na pia kufanya mkutano kwa njia ya video na maofisa na wataalam wa nchi 24 za Afrika. Wakati huohuo, vikosi vya msaada vya China vilivyopo Zanzibar, Tanzania, Rwanda, Eritrea na sehemu nyingine barani Afrika pia vimeshiriki kwenye juhudi za kupambana na virusi vya corona, wakitoa mafunzo kwa wauguzi na madaktari kwa nchi hizo. Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation la Kenya, China pia itasaidia kujenga Afrika CDC itakayogharimu dola za kimarekani zaidi ya bilioni 78 nchini Kenya, ikiwa ni sehemu ya hatua muhimu za kusaidia bara hilo kupambana na magonjwa ya kuambukiza.
Hadi sasa, nchi na sehemu 41 barani Afrika zimeripoti kesi za maambukizi ya virusi vya corona zaidi ya elfu moja, na kutoa changamoto kubwa kwa mifumo ya matibabu iliyo dhaifu ya Afrika. China kujitahidi kuzisaidia nchi mbalimbali duniani zikiwemo za Afrika kupambana na virusi vya corona haitarajii kupokea pongezi au shukrani, bali inafahamu kuwa hakuna nchi inayoweza kuepuka na maambukizi hayo, na umoja ni njia pekee inayoweza kushinda virusi hivyo ambavyo ni adui wa pamoja wa dunia nzima.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |