Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe ameliambia bunge la nchi hiyo kuwa Michezo ya Olimpiki ya Tokyo inaweza kuahirishwa kutokana na kuenea kwa virusi vya corona duniani. Hii ni mara ya kwanza kwa Waziri Mkuu huyo kutangaza kuwa mashindano hayo, yaliyopangwa kufanyika Julai 24, yanaweza kuahirishwa kutokana na kuongezeka kwa shinikizo kutoka kwa mashirikisho ya michezo duniani. Wakati huohuo, Canada imetangaza kuwa haitapeleka wanariadha wake kwenye mashindano hayo nay ale ya walemavu kutokana na mlipuko wa virusi vya corona. Kamati ya Olimpiki ya Canada imesema haitapeleka timu yake Tokyo isipokuwa kama michezo hiyo itaahirishwa mpaka mwakani. Nayo Kamati ya Olimpiki ya Australia imewataka wanariadha wake kujiandaa kwa mashindano ya olimpiki ya Tokyo yatakayofanyika msimu wa joto wa mwaka 2021.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |