• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Serikali ya kaunti nchini Kenya yafanya mikakati ya kuimarisha kilimo ili kupambana na atahri hasi za ugonjwa wa Corona

    (GMT+08:00) 2020-04-06 08:58:02

    Serikali za kaunti nchini Kenya zinachukua hatua mbalimbali za tahadhari ili kukabiliana na athari za maambukizi ya virusi vya Corona. Serikali ya kaunti ya Nandi imezindua matrekta kwa ajili ya wakulima kufanya upanzi ili kuwa na chakula cha kutosha wakati huu wa maambukizi ya virusi vya Corona. Khamis Darwesh anaripoti.

    Serikali ya kaunti ya Nandi nchini Kenya, ikiongozwa na Gavana Stephen Sang imeanza mikakati ya kuimarisha kilimo katika eneo hilo kama njia mojawapo ya kujitayarisha na athari za ugonjwa wa Corona, ikizingatiwa kuwa maambukizi ya virusi vya Corona yameleta athari hasi katika uchumi duniani.

    Kaunti ya Nandi imezindua matingatinga ya kulima wakati ambapo wakulima wengi wamesitisha shughuli za kilimo kutokana na hofu ya kupata maambukizi ya virusi vya Corona.

    Gavana wa kaunti ya Nandi Stephen Sang amesema ipo haja ya wakulima kurudi mashambani kwa sababu sasa ni wakati wa upanzi. Ili kuliwezesha hilo, Gavana Sang anasema serikali yake imenunua matrekta yatakayowasaidia wakulima kutayarisha mashamba yao ili kuhakikisha kuwa kuna chakula cha kutosha.

    "Huu ni msimu wetu wa kupanda, na iwapo tutapoteza msimu wetu huu wa upanzi ambao utadumu kwa muda wa miezi miwili ijayo, basi kuna uwezekano wa kuwa na uhaba mkubwa wa chakula nchini katika kipindi cha miezi sita ijayo."

    Mwezi wa Aprili na Mei kwa kawaida ndio msimu wa upanzi kwa wakulima katika kaunti ya Nandi, na iwapo upanzi hautafanyika katika msimu huu basi janga la njaa huenda likaikodolea macho nchi.

    Gavana Sang ametoa wito kwa wakulima kurudi mashambani ili kuepuka ukosefu wa chakula nchini.

    "Tunachofanya kama kaunti ya Nandi ni tunawaambia watu wetu kuwa tunafanya kazi masaa 24 kujitayarisha kupambana na janga hili la maambukizi ya virusi vya Corona. Hata hivyo tunataka ninyi mrudi katika mashamba yenu."

    Mkulima Mathew Kosgei ni mmojawapo wa wanaounga mkono na kuipongeza kaunti ya Nandi kwa hatua hii ya kununua matrekata na kuwataka wakulima kurudi mashambani kwa upanzi.

    "Tutumie nafasi hii ambapo kuna ugonjwa twende shamba kwa sababu unajua shamba utalima peke yako na watoto wako. Hata mtu akiomba jembe umrushie kwa mbali kwa sababu hauwezi kujua alikotembea."

    Waziri wa kilimo katika kaunti ya Nandi Dkt Kiplimo Lagat alisema serikali ya Nandi imenunua matrekta ili kuwawezesha wakulima kufanya kilimo cha biashara na sio kilimo cha kujikimu tu.

    "Vifaa hivi spesheli vinafaa kuwasaidia wakulima kufanya kilimo ambacho kilikuwa sio cha biashara kama vile kilimo cha viazi. Vifaa hivi ni vya kipekee na vitawasaidia wakulima kufanya kilimo cha biashara na kuzalisha mazao kwa wingi."

    Matingatinga hayo yatasambazwa kwa vikundi vya wakulima na yanatarajiwa kuongeza kwa kiasi kikubwa kiwango cha uzalishaji wa mahindi, viazi na mazao mengine ili kuwe na chakula cha kutosha nchini wakati huu wa ugonjwa wa virusi vya Corona.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako