Promota wa Fury, Frank Warren amesema bondia Tyson Fury ambaye anashikilia taji la WBC la uzani wa juu ambalo Mwingireza Anthony Joshua hana amepangiwa kuzidunda na Deontay Wilder wa Marekani kwa mara ya tatu mnamo Oktoba 2020. Fury alimlima makonde Wilder kwa njia ya 'Knock-Out' katika raundi ya saba jijini Las Vegas mnamo Februari mwaka huu. Hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Fury kumzidi maarifa Wilder baada ya wawili hao kuambulia sare mnamo 2018 jijini Los Angeles. Naye Joshua, hataweza kutetea mataji yake ya kimataifa ya IBF, WBA, WBO na IBO katika uzani wa juu baada ya pigano dhidi ya Kubrat Pulev wa Bulgaria kuahirishwa. Wawili hao walipangiwa kuchapana katika uwanja wa Tottenham Hotspur jijini London, Uingereza mnamo Juni 20, 2020. Kwa mujibu wa Matchroom Boxing ambao ni mapromota wa Joshua, tarehe mpya ya kuandaliwa kwa ndondi hizo itatolewa hivi karibuni, japo watajitahidi kuhakikisha kwamba pigano hilo bado linaandaliwa ugani Tottenham.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |