Wakenya wengi wakwama ughaibuni
Serikali ya Kenya Jumanne ilisema kuna maelfu ya Wakenya ambao wamekwama katika nchi mbalimbali za kigeni wanaoteseka kutokana na hali ngumu ya maisha kufuatia masharti makali ya kupambana na virusi vya Corona ulimwenguni.
Katibu katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni, Bw Macharia Kamau, anasema miongoni mwa wale waliokwama ng'ambo ni wagonjwa waliosafiri kutafuta matibabu na jamaa walioandamana nao.
Wengine ni watalii, wanafunzi na Wakenya wengine ambao wako katika nchi za kigeni bila vibali.
Inaaminika wengi waliokwama katika nchi za kigeni wakitafuta matibabu kwa magonjwa mbalimbali, wako nchini India ambapo shughuli zote zilisitishwa kama njia ya kupambana na ueneaji virusi vya corona.
Akizungumza Jumatatu wiki hii katika kikao cha wanahabari Nairobi, Bw Macharia alisema serikali ina wasiwasi kuhusu hali ya Wakenya walio India. Alisema kuna zaidi ya Wakenya 64 waliokuwa wameenda kutafuta matibabu, ila wakakwama India.
Alifichua kwamba, kuna wagonjwa wengine ambao kwa bahati mbaya walifariki, lakini hakuna jinsi jamaa zao wanaweza kusafirisha miili hadi nyumbani.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |