Nyota wa zamani wa Chelsea, Solomon Kalou ameiomba radhi klabu yake ya Hertha Berlin, baada ya kugundulika alivunja kanuni ya kuepuka mikusanyiko dhidi ya wachezaji wenzake katika kipindi hiki cha kujilinda na maambukizi ya virusi vya corona. Kalou alichapisha kipande cha video katika ukurasa wake wa Facebook, ambayo ilimuonesha akivunja kanuni hiyo ya kuepuka mikusanyiko, baada ya kumshika mkono mchezaji mwenzake wakati wanafanyiwa vipimo, video ambayo hata hivyo ameifuta. Timu yake Hertha Berlin ya Ujerumani, imeamua kumchukulia hatua za kinidhamu kwa kumsimamisha mchezaji huyo raia wa Ivory Coast, kutohudhuria mazoezi na mwendelezo wa baadhi ya michezo ya Bundasliga. Baada ya kupigwa rungu hizo, Kalou ameonesha kuwa hakukusudia kufanya hivyo, ambapo ameamua kuomba radhi kwa kitendo hicho na kwamba alifanya kwa furaha, baada ya majibu ya vipimo kuwa mazuri. Baada ya Kalou kuonesha uungwana huo, kinachosubiriwa ni mapokezi ya klabu yake juu ya msamaha huo kama itamruhusu kuendelea na mazoezi katika kipindi hiki ambacho wachezaji wamereja mazoezi kumaliza mechi zilizobaki za Ligi Kuu nchini humo.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |