Mshambuliaji Chinedu Obasi ametoa tuhuma nzito za rushwa kwa Taifa lake akidai aliombwa hongo ili ateuliwe katika kikosi cha timu ya taifa ya Nigeria 'Super Eagles' kilichoshiriki Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 zilizofanyika Brazil. Obasi (33) ambaye kwa sasa hana timu anayochezea baada ya kuachana na AIK ya Sweden katika dirisha dogo la usajili mwezi Januari, amedai kuwa alishindwa kuwemo katika kikosi cha Super Eagles kilichoshiriki Fainali hizo mwaka huo baada ya kugoma kutoa rushwa kwa mtu/watu ambao hata hivyo ameshindwa kuanika majina yao hadharani. Hata hivyo tuhuma hizo za Obasi zimeonekana kupokelewa kwa hisia tofauti na wadau wa soka nchini Nigeria wakishangazwa na mshambuliaji huyo kulisema hilo baada ya miaka sita tangu fainali hizo zilivyochezwa. Likijibu tuhuma hizo, shirikisho la mpira wa miguu Nigeria (NFF) limedai kuwa Obasi ametoa kauli hizo kwa lengo la kumchafua Keshi ambaye kwa sasa ameshatangulia mbele ya haki ambaye ndiye alikuwa analiongoza benchi la ufundi la Super Eagles.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |