Beki Danny Rose wa Tottenham Hotspur amekashifu na kupinga vikali mipango ya vinara wa soka nchini Uingereza kuanza tena kivumbi cha Ligi Kuu ya taifa hilo kabla ya virusi vya homa kali ya corona kudhibitiwa kote duniani. Maafisa wa klabu zote 20 za EPL walikutana mnamo Mei 11, 2020, kujadili uwezekano wa kurejelewa kwa kipute hicho ambacho kiliahirishwa mnamo Machi 13 wakati wowote kuanzia Juni 12, 2020. Hadi kufikia Mei 11, 2020, zaidi ya watu 32,000 walifariki dunia nchini Uingereza kutokana na ugonjwa wa Covid-19. Beki huyo amesema, soka haistahili hata kuzungumziwa kwa sasa hadi wakati ambapo idadi ya visa vya maambukizi itashuka kabisa, kwani maisha ya watu yako hatarini. Mei 12, 2020, Chama cha Wachezaji wa Soka Duniani (PFA) kilifichua kwamba kimepokea malalamishi mengi kutoka kwa wanasoka ambao wana "hoja nzito" zinazopania kupinga hatua ya kuanza tena kwa mechi za msimu huu katika mataifa mbalimbali.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |