Mwanariadha mahiri mzawa wa Somalia na raia wa Uingereza, Mohamed Muktar Jama almaarufu Mo Farah, amesema yuko tayari kuwaonyesha wapinzani wake kivumbi katika michezo ijayo ya Olimpiki. Farah 36, ndiye mtimkaji anayejivunia kwa ufanisi mkubwa zaidi katika ulingo wa riadha kwenye historia ya taifa la Uingereza. Amethibitisha kwamba atashuka ugani kuwania nishani ya dhahabu katika mbio za mita10,000 jijini Tokyo, Japan michezo hiyo itakapofanyika mwakani. Farah alistaafu miaka miwili iliyopita na akajibwaga katika mbio za masafa marefu za marathon, ambako hajafanikiwa kujinyakulia nishani yoyote. Mwanariadha huyo aliambulia nafasi ya nane katika kivumbi cha Chicago Marathon, mwishoni mwa mwaka uliopita wa 2019. Michezo ijayo ya Olimpiki itampa Farah jukwaa maridhawa la kutia kibindoni nishani ya 11 ya dhahabu katika historia ya kushiriki kwake mbio za mita 10,000.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |