Arsenal wameapa kumwadhibu vikali mshambuliaji wao matata Alexandre Lacazette baada ya kuibuka kwa ripoti kwamba nyota huyo mzawa wa Ufaransa alipatikana akivuta gesi ya Nitrous Oxide almaarufu 'Laughing Gas' iliyokuwa imejazwa ndani ya puto. Gazeti la Daily Star nchini Uingereza lilichapisha makala zenye picha zilizoonyesha Lacazette akiwa na puto lenye gesi hiyo mdomoni. Baadaye, mchezaji huyo wa zamani wa Olympique Lyon, Ufaransa aliwatumia wanasoka wenzake wa Arsenal video iliyochukuliwa akivuta gesi hiyo kupitia mitandao ya kijamii. Ingawa msemaji wa Arsenal, ameshikilia kwamba tukio hilo ni "suala la kibinafsi" litakaloshughulikiwa na klabu katika kiwango cha "ndani kwa ndani", huenda Lacazette "akapata adhabu". Ni wiki moja pekee imepita tangu Lacazette apatikane miongoni mwa wanasoka wengine wa Arsenal waliokiuka kanuni mpya za afya zinazodhibiti maambukizi zaidi ya virusi vya corona. Lacazette, 28, alionekana akiwa karibu sana na mwanamume mmoja aliyekuwa akimwoshea gari lake jijini Londo, Uingereza. Hivyo, alivunja kanuni inayotaka mtu kudumisha umbali wa hadi mita mbili kati yake na mwingine.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |